KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Monday, May 31, 2010

Ajeruhiwa Akiamulia Ugomvi wa Mume na Mke

MWANAUME mmoja aliyetambulika kwa jina la Samson amejeruhiwa katika sehemu zake za usoni wakati akijaribu kuamulia ugomvi uliokuwa ukiendelea kati ya mume na mkewe ambao ni majirani zake.
Mwanaume huyo amejeruhiwa katika ugomvi uliokuwa ukiendelea kati ya mume na mke katika nyumba waliyokuwa wamepanga huko maeneo ya Yombo jijini Dar es Salaam.

Chanzo chetu cha habari kilidai kuwa, ugomvi kati ya wanandoa hao ulianza majira ya saa 2 za usiku jana ndani ya chumba chao walichopanga katika nyumba hiyo.

Alidai kuwa walianza kusikia mwanaume akiongea kwa jazba akimfokea mke wake kwa chanzo ambacho hawakikufahamu mapema kwa wakati huo.

Alidai kuwa kutokana na hasira alizonazo mume wa dada huyo alianza kumpa kichapo mke wake na mwanamke huyo akisikika kuugulia na kilio cha mbali ili hali watu wasisikie kama alikuwa analia ndani humo.

Kadri dakika zilivyozidi kusogea mwanamke huyo uvumilivu ulimshinda na alianza kusikika akitoa sauti ya kilio kuashiria kibano alichokuwa akikipata kilikuwa kimemkolea.

Ndipo kelele za mwanamke huyo ziliwafanya baadhi ya wasamaria kwenda kugonga mlango wao ili waweze kumsaidia mwanamke huyo.

Mke huyo alijitahidi na aliweza kuufungua mlango na kutoka nje na alipotoka nje mume wake alimkamata na kumrudisha ndani na ndipo wasamaria wakaingia ndani humo kumtaka mume huyo aache kumpiga kwakuwa kwa muda huo ulikuwa ni muda wa watu kupumzika.

Samson aliingia ndani humo kwa lengo la kugombelezea ugomvi huo na mume huyo hakuwa tayari kusikiliza la mtu na ndipo wakati Samson yupo katika pilika pilika ya kumnusuru mwanamke huyo kuepukana na kipigo hicho, mume huyo aliamua kumrushia stuli Samson ambayo ilitua barabara kwenye sehemu zake za uso.

Mume huyo hakutosheka alipasua chupa ya bia na kumpiga nayo Smason usoni na kumjeruhi vibaya.

Kwa kuwa Samson alishajeruhiwa aliamua kujinusuru kwenye ugomvi huo kuachia wengine wakagombelezee na yeye kwenda zahanati ya karibu kwa matibabu.

Chanzo cha ugomvi kwa wanandoa hao hakikufahamika hadi tunaondoka eneo la tukio.

Askofu wa Ireland ajiuzulu Nigeria


Makao makuu ya kanisa la Kikatoliki Vatican imekubali hatua ya kujiuzulu kwa askofu wa Ireland aliyekuwa Nigeria kutokana na shutuma za kumdhalilisha kijinsia binti mmoja huko Niger Delta.

Richard Burke, askofu wa mji wa Benin, amekubali kuwa na uhusiano wa kimapenzi na binti huyo lakini amekana kwa binti huyo kuwa na umri mdogo uhusiano huo ulipoanza.

Katika taarifa iliyotolewa kwenye gazeti la kikatoliki la Ireland amesema, " Sababu ya kujiuzulu ni kutokuwa mwaminifu katika kiapo changu cha useja."

Askofu huyo amejiuzulu baada ya madai hayo kutolewa mwaka jana.

Dolores Atwood alidai kunyanyaswa kijinsia na askofu Burke wakati alipokuwa padri huko Warri kusini mwa Nigera kwenye mji wa Niger Delta.

Hata hivyo, amesema uhusiano wao ulianza mwaka 1989 alipokuwa miaka 40 na binti akiwa na umri wa miaka 21.

Amesema kwenye taarifa yake, " Nilijibu haraka iwezekanavyo kwamba sijawahi hata siku moja maishani mwangu kumnyanyasa mtoto kijinsia. Huu bado ni msimamo wangu. Huu ni ukweli."

Askofu Burke pia alimwomba radhi Bi Atwood na kuomba msamaha katika vituo vyake vya kanisa huko Warri na Benin.

Kanisa hilo limesema limekubali kujiuzulu kwake ambapo pia limetaja jopo litakalochunguza udhalilishaji wa watoto
uliofanywa na viongozi wa kikatoliki huko Ireland.

Mahakama ya ICC 'yabadili mwenendo'


Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema, mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita (ICC) imefanikiwa kulazimisha serikali kubadili mwelekeo wao tangu iundwe miaka minane iliyopita.

Ban Ki-moon ameuambia mkutano unaofanyika Uganda unaojadili kuhusu mahakama hiyo iliyopo Hague kwamba imepunguza uwezekano wa watu kuepuka adhabu na kuweka misingi mipya juu ya haki za waathiriwa.

Lakini ametoa wito wa nchi wanachama kushirikiana.

ICC ina kesi tano zinazoendelea, zote zikiwa kutoka barani Afrika. Mpaka sasa hakuna aliyepatikana na hatia ya madai ya kuhusika na uhalifu wa kivita.

Bw Ban aliwaambia viongozi, " Kwa wakati ule wachache wangeamini kwamba mahakama hii ingekuwa hapa ilipo, inafanya kazi vizuri, inafanya utafiti na kuendesha mashtaka ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu.

"Katika karne hii mpya ya uwajibikaji, wale wanaofanya uhalifu mkubwa zaidi dhidi ya binadamu watashughulikiwa ipasavyo."

Bw Ban amesema wakati sasa umepita wa dunia kuchagua baina ya amani na haki- sasa mataifa yanatakiwa kukabiliana nayo bega kwa bega.

Lakini mwandishi wa BBC Karen Allen kwenye mji mkuu wa Uganda, Kampala, amesema hatua ya kutoa hati za kukamatwa dhidi ya viongozi waliopo madarakani, akiwemo Rais Omar al-Bashir wa Sudan kwa madai ya uhalifu wa kivita mjini Darfur, imezua wakosoaji wengine kusema mashtaka kama hayo yanakatisha tamaa harakati za kuleta amani katika eneo hilo.

Viongozi kutoka zaidi ya nchi 100 wanashiriki mkutano huo, kujadili mafanikio ya ICC na kutoa mapendekezo ya kuimarisha sheria zake.

Ufaransa imekusudia kuipa Afrika msukumo mpya wa biashara


Ufaransa imekusudia kuipa Afrika msukumo mpya wa biashara katika mkutano wa siku mbili unaofunguliwa mjini Nice.

Rais Nicolas Sarkozy ndio mwenyeji wa mkutano unaohusisha Afrika na Ufaransa kwa mara ya kwanza.
Viongozi 38 wa Afrika na watendaji 250 wa biashara wanahudhuria mkutano huo.

Viongozi wa kijeshi kutoka nchi mbili zilizokuwa koloni la Ufaransa, Guinea na Niger, ni miongoni mwa nchi zinazohudhuria.

Ufaransa inachuana na China na mataifa mengine yanayoibuka kwa kutafuta masoko Afrika.

Matatizo ya uharamia, ugaidi na mabadiliko ya hali ya hewa ni miongoni mwa yatakayojadiliwa.

Nchi za Afrika zinataka ziwe na nguvu zaidi katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa na kongamano la G20, kwahiyo pia kutakuwa na mjadala wa namna ya kufanikiwa kutekeleza hayo.

Kundi la Civil liberties limesema miongoni mwa wakuu wa nchi 38 wa Afrika walioalikwa ni viongozi wawili tu ambao hawakuweza kushutumiwa kuhusika na kukiuka haki za binadamu.

Madagascar-ikiwa bado katika mgogoro wa kisiasa haikualikwa, na Zimbabwe ilikataa kupeleka mjumbe wake baada ya Ufaransa kumzuia Rais Robert Mugabe kuhudhuria mkutano huo.

Gazeti la France Le Monde limeripoti, katika hatua ya kuonyesha kuwa Ufaransa haijahusisha nchi zinazozungumza kifaransa peke yake, Rais Sarkozy atafanya mazungumzo ya pamoja na viongozi wa Nigeria na Afrika Kusini, nchi mbili zinazozungumza kiingereza na zenye uzito barani humo.

Wakili kufikishwa mahakamani Rwanda


Wakili mmoja wa Marekani leo anatarajiwa kufikishwa mahakamani nchini Rwanda kwa tuhuma za kufahamu njama za mauji ya kimbari nchini humo mwaka 1994.

Wakili huyo Peter Erlinder, ambaye pia anatuhumiwa kwa kukana mauaji hayo, alisafiri nchini humo wiki jana na akipanga kumwakilisha kiongozi wa upinzani Victoire Ingabire.

Ingabirie anakabiliwa na tuhuma za kuchochea hisisa za mauaji ya kimbari.

Lakini waziri wa mambo ya nje Bi Louise Mushikiwabo, amesema kuwa Bw. Erlinder hana idhidni ya kuendesha kazi yake nchini humo na kwamba yuko tu mjini Kigali, kujitangaza na kuendesha kile alichotaja kuwa siasa zake kali.

Kwa mujibu wa waziri huyo, Rwanda imepiga marufuku propaganda kuhusu mauaji ya kimbari, ili kuzuia kutokea tena kwa mauaji kama hayo.

Viongozi wa Asia wakutana Korea Kusini


Viongozi wa Uchina, Japan na Korea ya Kusini wamekubaliana kufanya kazi pamoja katika kusuluhisha mzozo juu ya kuzama kwa manuari ya kijeshi ya Korea ya Kusini.

Baada ya kumalizika kwa mkutano wao nchini Korea ya Kusini, viongozi wa mataifa hayo wamefanya mkutano na waandishi wa habari.

Viongozi wote watatu walikubaliana kuwa kuzama kwa manuari ya Korea ya Kusini, ambapo watu 46 walipoteza maisha yao mwezi March, ni changamoto kubwa kwa usalama na utulivu wa eneo hilo.

Waziri Mkuu wa Japan,Yukio Hatoyama, ameahidi kumuunga mkono Rais wa Korea ya Kusini, Lee Myung-bak na ameongeza kuwa anakubaliana kikamilifu na ushahidi kuwa manuari hiyo ilililipuliwa na kombora la torpedo lililofyatuliwa na nyambizi ya Korea ya Kaskazini.

Msimamo wa Uchina baado haujabainika wazi. Kwenye mkutano huo na waandishi wa habari, Waziri Mkuu wa Uchina, Wen Jiabao, alituma salamu za rambi rambi kwa familia za mabaharia waliouwawa, na akazungumzia umuhimu wa kutuliza hali ya wasiwasi iliyopo, lakini hakusema chochote kuhusu msimamo wake juu ya suala la Korea ya Kaskazini kuhusishwa na shambulizi hilo.

Utawala wa Beijing unadhaniwa kuhofia kumchokoza mshirika wake wa siku nyingi katika vita baridi duniani, huku Pyongyang ikikanusha vikali madai ya kuhusika na shambulizi la kombora dhidi ya manuari ya jirani wake, Korea ya Kusini.

Saturday, May 29, 2010

50 Cent Choka Mbaya, Ukimuona Huwezi Kumtambua

Kwa kuiangalia picha yake unaweza usiamini na hata utakapoambiwa hii ni picha ya 50 Cent jinsi alivyo sasa unaweza usiamini, lakini ukweli ni kwamba picha hii ni ya 50 Cent kama alivyo sasa baada ya kupungua kilo 25 ndani ya wiki 9.
Picha mpya za mwanamuziki milionea wa Marekani 50 Cent zimetolewa na kuwafanya watu wabaki midomo wazi kwa jinsi ambavyo imekuwa vigumu kumtambua kwa jinsi alivyopungua kilo 25 ndani ya wiki tisa.

50 Cent amejikondesha kwa kunywa maji na juice pekee ili aweze kuigiza kwenye filamu mpya ambayo jikoni ambayo inamuelezea nyota wa mpira wa miguu ambaye anaugua ugonjwa wa kansa.

50 Cent ambaye ana umri wa miaka 34 amekonda sana na amepungua uzito wake toka kilo 97 hadi kilo 72.

50 Cent amejikondesha ili kuleta uhalisia wa mgonjwa wa kansa katika filamu ya "Things Fall Apart", filamu hiyo 50 Cent ndiye nyota wa filamu na prodyuza msaidizi.

Wakati picha mpya za 50 Cent zilipowekwa kwenye mitandao jana watu wengi waligoma kuamini na kusema kwamba picha hizo ni uzushi tu wa kwenye mitandao.

Lakini 50 Cent ambaye jina lake halisi ni Curtis Jackson alijitokeza na kuthibitisha kuwa picha hizo ni za kweli.

50 Cent alisema kuwa baada ya kumaliza kuigiza kwenye filamu hiyo ataanza kula kama kawaida kurudisha mwili wake wa zamani.

Jose Mourinho Atua Real Madrid

Wababe wa Hispania Real Madrid, wamefanikiwa kumnyakua kocha wa mabingwa wa ulaya Inter Milan ya Italia, Jose Mourinho.
Baada ya kutwaa makombe matatu msimu huu, kocha wa Inter Milan, Jose Mourinho ameitosa timu hiyo na kuhamia kwa timu tajiri duniani ya Real Madrid ya Hispania.

Tovuti ya Real Madrid ilitoa taarifa leo kuwa makubaliano yamefikiwa kati ya Inter Milan na Real Madrid hivyo Mourinho ndiye atakayekuwa kocha mpya wa Real Madrid.

Awali kabla ya makubaliano hayo kufikiwa, Inter Milan iligoma kumuachia Mourinho ikitaka ilipwe fidia ya euro milioni 16 kwa Mourinho kukatisha mkataba wake ambao umebakiza miaka miwili.

Rais wa Real Madrid Florentino Perez alienda Milan kukutana na mwenyekiti wa Inter Milan Massimo Moratti ili kufikia muafaka juu ya suala hilo la Mourinho. hata hivyo maafikiano yaliyofikiwa na klabu hizo hayakuwekwa wazi.

Jose Mourinho atatambulishwa kwa wapenzi wa Real Madrid siku ya jumatatu saa saba mchana kwa saa za Tz kwenye uwanja wa Real Madrid wa Santiago Bernabeu.

Wahindi Walalamikia Ukubwa wa Kondomu

Utafiti uliofanyika nchini India umeonyesha kuwa wanaume wengi nchini India hawafurahishwi na ukubwa wa kondomu unaotambulika duniani kwakuwa kondomu hizo ni kubwa sana kulinganisha na ukubwa wa nyeti zao.
Utafiti huo uliowashirikisha wanaume 1,000 wa nchini India ulionyesha kuwa kondomu zenye ukubwa unaotambulika kimataifa huwapwaya wanaume wengi wa nchini India.

Utafiti huo uliweka wazi kuwa zaidi ya nusu ya wanaume walioshiriki utafiti huo walikuwa na uume ambao ulikuwa ni mfupi kulinganisha na ukubwa wa kondomu.

Utafiti huo uliofanyika kwa miaka miwili uliweka wazi kuwa asilimia 60 ya wanaume nchini India wana uume wenye urefu kati ya sentimeta tatu hadi tano pungufu ya ukubwa wa kondomu unaotambulika duniani.

Matokeo ya utafiti huu yamepelekea makampuni ya kutengeneza kondomu nchini India yatakiwe kutengeneza kondomu zenye ukubwa tofauti tofauti.

Matokeo ya utafiti huu yametiliwa mkazo kwakuwa India ndiyo nchini inayoongoza duniani kwa idadi kubwa ya watu walioathirika na virusi vya Ukimwi.

Mzee Pwagu Afariki Dunia


Muigizaji mahiri nchini Tanzania, Rajab Kibwana Hatia au maarufu kwa jina la Pwagu ambaye alitamba sana redioni kwenye mchezo wake wa Pwagu na Pwaguzi, amefariki dunia jana akiwa na umri wa miaka 87.
Mzee Pwagu alifariki jana ijumaa kwenye hospitali ya Amana jijini Dar es Salaam baada ya kuugua muda mrefu maradhi ya uzeeni.

Mzee Pwagu alitamba sana redioni kwenye miaka ya 60 hadi 80 katika kipindi cha redio kilichokuwa kikirushwa hewani na redio ya taifa Redio Tanzania Dar Es Salaam (RTD) akimshirikisha rafiki yake Ali Said Keto ambaye yeye alikuwa maarufu kwa jina la Pwaguzi.

Mzee Pwagu ambaye alizaliwa mwaka 1923 mjini Tabora atakumbukwa zaidi kwa juhudi zake za kuinua sanaa za maigizo nchini.

Mzee Pwagu ndiye aliyekuwa muanzilishi wa kundi la Kaole ambalo limetoa wasanii wengi wanaotamba hivi sasa kwenye anga la filamu Tanzania kama vile Ray na Kanumba.

Mazishi ya Mzee Pwagu yatafanyika leo kwenye makaburi ya Kigogo jijini Dar es Salaam.

MUNGU AMLAZE MZEE PWAGU MAHALI PEMA PEPONI -- AMEN

Wanaume wapendanao waachiwa Malawi


Wanaume wawili wanaofanya mapenzi ya jinsia moja nchini Malawi waliofungwa baada ya kufanya sherehe ya uchumba wamesamehewa na Rais Bingu Wa Mutharika.

Bw Mutharika, akizungumza wakati katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa alipotembelea nchi yake, amesema ameamuru waachiliwe huru haraka iwezekanavyo.

Steven Monjeza na Tiwonge Chimbalanga walihukumiwa kifungo cha miaka 14 jela mapema mwezi huu kwa kufanya vitendo kinyume cha maumbile na vitendo vya aibu.

Kesi hiyo iliibua malalamiko kutoka nchi za kimataifa napia mjadala juu ya mapenzi ya jinsia moja ndani ya Malawi.

Bw Ban ameusifu uamuzi wa Rais kuwa ni wa "kijasiri."

Amesema, "Sheria hii iliyopitwa na wakati irekebishwe popote ilipo."

'Utamaduni wa chuki'
Waandishi wanasema Malawi ni jamii yenye msimamo mkali sana ambapo viongozi wa dini huhusisha mapenzi ya jinsia moja na ushetani.

Bw Mutharika amewaachia huru kwa misingi ya haki za binadamu.

Baada ya kukutana na Bw Ban alisema, "Wanaume hawa wawili wametenda uhalifu dhidi ya mila zetu, dini zetu na sheria zetu."

"Hata hivyo, kama mkuu wa nchi nawasamehe na hivyo waachiwe haraka iwezekanavyo bila masharti yeyote."


Steven Monjeza, 26, na Tiwonge Chimbalanga, 20, walikuwa gerezani tangu walipokamatwa Desemba 2009 baada ya kufanya sherehe ya uchumba, kabla ya mipango ya kufunga ndoa mwaka 2010.

Gift Trapence, kutoka kituo cha kutetea maendeleo ya watu, amefurahiswa na uamuzi huo.

Amesema, "Tumefurahi sana na tunamsifu Rais kwa ukomavu wake, lakini bado tuna safari ndefu kumaliza mila hizi za chuki."

Sheria za kikoloni
Mashirika ya kutoa misaada na haki za binadamu yamekuwa yakishinikiza serikali yake kuheshimu haki ya wachache.

Wanaume hawa wawili wametenda uhalifu dhidi ya mila zetu, dini zetu na sheria zetu.
Bingu Wa Mutharika, Rais wa Malawi
Serikali ya Uingereza, mfadhili mkuu wa Malawi, ilisema ilishtushwa na hukumu hiyo, na Marekani iliuelezea kama hatua moja nyuma katika harakati za kupigania haki za binadamu.

Siku ya Jumamosi, mwanamuziki wa miondoko ya Pop Sir Elton John aliandika barua ya wazi kwa Bw Mutharika kupitia gazeti la Uingereza la The Guardian akiomba waachiwe huru.

Wanaume hao wawili wamehukumiwa kwa sheria ya zamani ya kikoloni wakati Malawi ilipokuwa ikitawaliwa na Uingereza.

Makoloni mengi yaliyokuwa ya Uingereza yana sheria sawa na hiyo inayopinga mapenzi ya jinsia moja: India ilibadilisha sheria hiyo ya kuwapinga mwaka jana.

Walinda amani 2000 kuondolewa Congo


Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepiga kura ya kuruhusu kuondolewa kwa kiasi cha wanajeshi wake 2000 wanaolinda amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Hata hivyo, baraza hilo limeahirisha uamuzi kuhusu kuondolewa kikamilifu kwa kikosi chake chenye wanajeshi 20, 500, hadi mwaka ujao,kama alivyoagiza Rais wa Congo, Joseph Kabila.

Wajumbe wote 15 wa baraza kwa kauli moja walipitisha azimio la kuwaondoa wanajeshi hao "haswa katika maeneo ambayo hali ya usalama inaruhusu".

Umoja wa Mataifa pia uliamua operesheni zake za kawaida kuendelea nchini Congo hadi mwezi June mwaka wa 2011.

Kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini Congo ambacho hujulikana kama MONUC, kuanzia mwezi July kitafahamika kama (UN Organisation Stabilisation Mission in DR Congo) MONUSCO.

Azimio hilo linaruhusu MONUSCO kuwa na wanajeshi 19,815, waangalizi wa kijeshi wapatao 760, na polisi mchanganyiko wapatao 1400.

Unyanyasaji wa kimapenzi

Wanajeshi wa Umoja wa Mataifa wamekuwa na rekodi yenye utata katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, pamoja na madai ya kuhusika na dhulma za kimapenzi, usafirishaji wa dhahabu kimagendo na kuwatoroka waasi wakati wa mapigano.

Askari wa kulinda amani waliwasili katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo mwaka wa 1999, wakati huo wakianza kushughulikia mapigano ya wenyewe kwa wenyewe nchini kote.


Tangu kumalizika kwa mapigano mwaka wa 2003, wamekuwa wakipambana na wanamgambo wa makundi mbali mbali, ambao wamekuwa wakiiba madini yenye thamani kubwa mashariki mwa nchi.

Wengi wa wanamgambo hao sasa aidha wamenyanganywa silaha, au kujumuishwa katika jeshi la Congo, huku wengine wakibakia kama majangili wenye silaha.

Rais Kabila anaamini kuwa jeshi lake la taifa lina uwezo wa kushughulikia matatizo yaliyobaki na amesema anataka wanajeshi wa Umoja wa Mataifa wawe wameondoka nchini humo mwishoni mwa mwaka wa 2011.

Hata hivyo, baadhi ya wadadisi wanaamini kuwa eneo hilo baado halina usalama, na halitoweza kuhimili athari za kuondoka kwa wanajeshi hao wa kulinda amani.

Unyanyasaji wa kimapenzi ni shida ya kipekee, ambapo zaidi ya wanawake 8,000 walibakwa wakati wa mapigano, mwaka wa 2009, kulingana na repoti ya Umoja wa Mataifa.

Hali hiyo ilisababisha kikosi cha MONUC kuwasindikiza wanawake wanapokwenda sokoni.

Umoja wa Mataifa umeamua kuwa mustakbala wa wanajeshi wake utaamuliwa kutokana na mafanikio yatakayopatikana mashariki mwa nchi na uwezo wa serikali ya Congo wa kuwalinda raia wake, pamoja kudhibiti nchi nzima.

"Hatua ya kuwalinda raia lazima ipewe umuhimu" Umoja wa Mataifa ilisema katika azimio lake, na kuongeza kuwa iliwaruhusu walinda amani wake kutumia "nguvu zao zote" kutekeleza azimio hilo.

Mataifa 200 kupunguza silaha za nuclear

Mataifa takriban 200, wanachama wa mkataba uliotia sahihi ya upunguzaji wa silaha za Nuclear (npt) yameafiki mpango wa jitihada za kulifanya eneo la Mashariki ya kati lisilo kuwa na silaha hizo.
Kwenye mkutano uliofanywa kwenye makao makuu ya Umoja wa mataifa mjini New York wajumbe waliitisha mkutano mnamo mwaka 2012 utakaohudhuriwa na mataifa ya mashariki ya kati-ikiwemo Iran kuunda eneo huru ya bila silaha za nuclear.

Waraka huo ulioafikiwa kwa sauti moja uliitaka Israel nayo isahihishe mkataba wa kupinga nuclear.

Lakini Rais Barack Obama aliyekubali mpango huo amepinga kuitenga Israel kwa kusema kuwa hilo linaweza kuathiri juhudi za kuishawishi nchi hiyo isihudhurie mazungumzo ya mwaka 2012.

Baadaye Afisa wa Israel aliutaja waraka huo kama uzandiki. Alisema kuwa, Israel imetajwa, il hali waraka haukutaja nchi kama India,Pakistan na Korea ya kaskazini ambazo zina zana za nuclear, pamoja na Iran ambayo inajitahidi kujenga silaha kama hizo, afisa wa ngazi ya juu aliliambia shirika la habari la Ufaransa(AFP)

Waraka huo wenye kurasa 28 ulisahihishwa na nchi wanachama 189 kufuatia mazungumzo nyeti mnamo siku ya mwisho wa mazungumzo ya mwezi mzima yaliyokusudia kuimarisha fungamano la mkataba unaotaka kupunguza matumizi ya nuclear, kama nguzo muhimu katika juhudi za kimataifa za kuondoa silaha.

Waraka huo unamtaka katibu mkuu wa Umoja wa mataifa kuandaa mkutano wa mataifa ya mashariki ya kati mnamo mwaka 2012 ili kuafikiana juu ya kuunda eneo lisilo kuwa na silaha za nuclear pamoja na silaha nyingine za maangamizi.

Rais wa mkutano huo, Libran Cabactulan kutoka Ufilipino amesema kuwa dunia yote inatuangalia sisi wakati waraka huo unaidhinishwa.

Mjumbe wa Misri, Maged Abedelaziz, akizungumza kwa niaba ya Vuguvugu la mataifa yasiyofungamana na siasa za upande wowote, alifurahia uwamuzi na kusema ni hatua muhimu katika kufikia malengo ya mkataba.

Wajumbe walijadili mapendekezo hadi usiku wa manane kabla ya kuyarejelea tena hapo jana asubuhi.

Mojapo ya hoja kuu ziliihusu Israel ambayo si mwanachama wa fungamano hili la mkataba unaodhamiria kupunguza silaha za nuclear, inaaminika kuwa na silaha za nuclear ingawaje haijawahi kukubali kuwa nazo.

Ilikuwa kazi ngumu kwa wajumbe wa nchi za Kiarabu na marafiki wa Israili ili kuweza kuafikiana juu ya maneno yanayostahili kutumika kuandika mkataba huu. Waandishi wa habari wanasema kuwa mataifa ya kiarabu yanataka kuishinikiza Israili isalimishe zana zake za nuclear.


Iran nayo ilitaka mataifa matano yanayomiliki silaha za nuclear yakubaliane juu ya mpango wa tareh ya kusalimisha silaha zake.

Katika waraka kamili ulioafikiwa hakuna mda uliowekwa lakini mataifa hayo lazima yaharakishe hatua za kufikia lengo hili la kupunguza silaha za nuclear na wakutane tena mnamo mwaka 2014.

Friday, May 28, 2010

Mama Afanya Mapenzi na Mwanae ili Kumpa Uzoefu wa Mapenzi


Baba na mama wa mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 9 wa nchini Australia wametupwa rumande kwa kufanya mapenzi na mtoto wao huyo wakidai wanampa elimu na uzoefu wa mapenzi.
Mwanaume mwenye umri wa miaka 57 na mkewe mwenye umri wa miaka 48 wa nchini Australia wametupwa rumande kwa kufanya mapenzi na mtoto wao wa kiume mwenye umri wa miaka 9.

Wazazi wa mtoto huyo ambao ni wafuasi wa kundi la watembea uchi "Nudist" walikuwa wakimpigisha punyeto na kufanya mapenzi na mtoto wao huyo ili kumpa uzoefu wa kimapenzi.

Mamlaka husika zilipewa taarifa juu ya suala hilo baada ya mtoto huyo kumtongoza msichana katika shule yake akimtaka wafanye mapenzi.

Polisi waliwatia mbaroni wazazi wa mtoto huyo novemba 16, 2009 na hawajapewa nafasi ya kumuona mtoto wao tena.

Akiongea mahakamani mjini Sydney jana, baba wa mtoto huyo alikiri makosa mawili ya kumuingilia mtoto wake na makosa mengine ya kumpigisha punyeto, kumshambulia na kuziweka picha na video za vitendo vyake kwenye internet.

Mama yake naye alikiri makosa ya kufanya mapenzi na mwanae na pia kumchua nyeti zake.

Taarifa ya polisi ilisema kuwa mtoto huyo aliwaambia kuwa wazazi wake hutembea uchi wanapokuwa ndani ya nyumba kunapokuwa na hali ya joto.

Baba yake hakuonyesha kujutia vitendo alivyokuwa akimfanyia mwanae na badala yake alidai kuwa anashangaa kwanini amekamatwa wakati alikuwa akimpa elimu ya mapenzi mwanae.

Wazazi wote wawili wa mtoto huyo wamenyimwa dhamana na wametakiwa kutowasiliana na mtoto wao kwa njia yoyote ile mpaka atakapofikisha umri wa utu uzima.

Watapandishwa tena mahakamani juni 4 kujua hatima zao.

Mwanamke Aliyewaingiza Mjini Wanajeshi 11 wa Marekani


Polisi nchi Marekani wanamtafuta mwanamke aliyewaingiza mjini wanajeshi 11 wa Marekani kwa kufunga nao ndoa na kisha kuwaibia mali zao zote waliposafiri na kumuachia nyumba zao.
Mwanamke huyo aliyetajwa kwa jina la Bobbi Ann Finley anaaminika kuwa ni tapeli sugu ambaye amekuwa akiwaingiza mjini wanajeshi wa Marekani kwa takribani miaka 20.

Msako umeanzishwa na polisi kwenye majimbo ya Washington, Nebraska na Texas wakati jeshi la Marekani limemkodisha mpelelezi maalumu kumsaka mwanamke huyo.

Njia yake ya kuwatapeli wanajeshi ni rahisi sana
Hujipeleka kwenye kambi za jeshi la Marekani kuwasaka wanaume waliojaa upweke wa mapenzi ambao wanaandaliwa kwaajili ya kusafirishwa kupelekwa kwenye kambi za Marekani nchini Afghanistan na kwingineko.

Anapofanikiwa kumnasa mwanaume humuongopea kuwa yeye ni binti afisa wa ngazi za juu wa jeshi la Marekani na kwamba ameachiwa urithi mkubwa ambao ataweza kuuchukua iwapo ataolewa.

Baada ya mwanajeshi wa Marekani kuingia mtegoni na kukubali kufunga naye ndoa, Finley huanza maisha ya ndoa na mumewe huyo huku akisubiria kwa hamu siku ambayo mumewe atasafirishwa kwenda nje ya Marekani.

Baada ya mumewe kusafiri, Finley huanza kazi ya kuiba vitu vyote kwenye nyumba na kuzitumia vibaya credit card anazoachiwa. Huhakikisha anawaingiza hasara kubwa kabla ya kutimkia mji mwingine kusaka mwanajeshi mwingine.

Katika miaka yake ya kuwatapeli wanajeshi wa Marekani kuanzia mwaka 1993, Finley amefanikiwa kuwatepeli jumla ya wanajeshi 11 na amezaa watoto tisa na wanajeshi 9 tofauti.

Watoto wake inasemekana wamezagaa katika miji mbalimbali ya Marekani na baadhi yao hawajawahi kuziona sura za baba zao.

Mmojawapo wa wanajeshi aliyelizwa na Finley alikuwa ni Shane Cheeseman, ambaye alikutana na Finley mwaka 1998 kwenye kambi ya jeshi ya Fort Hood mjini Texas.

"Nilifunga naye ndoa jumatatu, ilipofika mwisho wa wiki alikuwa ameishaondoka na ameniacha kwenye deni kubwa sana", alisema Cheeseman alipokuwa akiongea na waandishi wa habari.

Alipotoa taarifa polisi aliambiwa kuwa yeye ni mmojawapo ya wanajeshi wengi walioingizwa mjini na Finley.

Msako mkali unaendelea nchini Marekani kumsaka Finley na taarifa za awali zinasema kwamba jumla ya wanaume 40 wameishajitokeza kuripoti kutapeliwa kwao na Finley.

Wanawake Watakaovaa Vimini Kuvalishwa Sketi Ndefu


Serikali ya Indonesia imeandaa sketi ndefu 20,000 kwaajili ya kuwavalisha kinguvu wanawake watakaokamatwa barabarani wakiwa wamevaa vimini au nguo zinazobana.
Kuanzia leo polisi wa kiislamu wa Indonesia wanaingia mitaani kuwasaka wanawake wanaovaa nguo fupi au zinazobana zinazoonyesha maumbile yao, wanawake watakaokamatwa mitaani wakiwa wamevaa hivyo watalazimishwa wavae hapo hapo sketi ndefu zilizotolewa bure na serikali.

Hatua hiyo imefuatia sheria ya kupiga marufuku nguo fupi za wanawake ambayo inaanza kufanya kazi leo katika mojawapo ya majimbo ya nchi hiyo yenye waislamu wengi kuliko nchi zote duniani.

Sheria hiyo imepitishwa katika jimbo la Aceh lililopo kaskazini mwa kisiwa cha Sumatra nchini Indonesia. Vimini, jeans na nguo za kubana ni miongoni mwa nguo za wanawake zilizopigwa marufuku.

Mkuu wa jimbo hilo Ramli Mansur alisema kwamba wanawake watakaosimamishwa na polisi wa sharia, hawatatiwa mbaroni lakini watalazimishwa wavae sketi ndefu zilizotolewa na serikali.

Mansur aliongeza kwamba ataisimamia vyema sheria hiyo kwa kuhofia siku moja ataulizwa na Mungu aliutumiaje uongozi wake katika kusimamia sharia za kiislamu.

Anyang'anywa Uraia Baada ya Kuoa Mke wa Pili


Mwanaume wa Uturuki ambaye alipata uraia wa Uswizi baada ya kuoa mwanamke wa Uswizi amenyang'anywa uraia baada ya kuoa mke wa pili kwa siri.
Mturuki huyo ambaye alipewa uraia wa Uswizi baada ya kumuoa mwanamke raia wa Uswizi, alinyang'anywa uraia na mahakama ya Uswizi jana baada ya kugundulika ana mke mwingine nyumbani kwao nchini Uturuki.

Mturuki huyo alikuwa akiishi maisha ya ndoa na mke wake wa Uswizi kwa miaka 26 lakini wakati huo huo alikuwa na mke mwingine nchini Uturuki ambaye amezaa naye watoto wawili, limeripoti shirika la habari la Uswizi, ATS.

Mwaka 2003 alipewa uraia wa Uswizi kutokana na ndoa yake na mwanamke huyo raia wa Uswizi.

Mke wake aligundua kuwa mumewe ameoa mke mwingine nchini Uturuki lakini alikaa kimya hadi hivi karibuni ikiwa imepita miaka mitano alipoamua kupeleka malalamiko wizara ya uhamiaji.

Wizara ya uhamiaji iliamua kumnyang'anya uraia Mturuki huyo ambaye aliamua kwenda mahakamani kukata rufaa.

Mahakama ya rufaa ya Uswizi imetoa uamuzi jana na kuamua Mturuki huyo anyang'anywe uraia na pasipoti ya Uswizi aliyopewa

Kila Anayemiliki Namba ya Simu Hii Hufariki


Shirika la simu la Mobitel la nchini Bulgaria limeamua kuifuta mojawapo ya namba zake za simu baada ya kugundulika kuwa kila mtu anayeimiliki namba hiyo hufariki baada ya muda mfupi.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Bulgaria, wamiliki wa namba ya simu hii 0888 888 888 hufariki ndani ya kipindi cha muda mfupi.

Shirika la simu la Mobitel la nchini Bulgaria ambalo linaimiliki namba hiyo limeamua kuifutilia mbali namba hiyo baada ya taarifa ya vifo vya wenye kuimiliki namba hiyo.

Mtu wa kwanza kufariki alikuwa ni bosi wa kampuni hiyo kubwa ya simu nchini Bulgaria, Vladimir Grashnov, ambaye alifariki mwaka 2001 kutokana na ugonjwa wa kansa.

Namba hiyo ya simu alipewa mtu mwingine aliyejulikana kwa jina la Konstantin Dimitrov ambaye naye alifariki miaka miwili baadae baada ya kupigwa risasi nchini Uholanzi.

Inasemekana kwamba mabosi wa kundi la Mafia wa Urusi ndio waliopanga mauaji yake baada ya kumuonea wivu kwa jinsi alivyokuwa akisafirisha kwa wingi madawa ya kulevya.

Mfanyabiashara Konstantin Dishliev alipewa namba hiyo baada ya Konstantin kufariki lakini naye alifariki miaka miwili baadae baada ya kupigwa risasi nje ya mgahawa wa vyakula vya kihindi mjini Sofia nchini humo.

Mfanyabiashara huyo inasemekana alikuwa akisafirisha madawa ya kulevya toka nchi za kusini mwa America kuziingiza Bulgaria. Aliuliwa baada ya polisi kuugundua mzigo wake wa madawa ya kulevya ukiwa njiani kuingizwa Bulgaria.

Mobitel wameamua kuifuta namba hiyo baada ya polisi kukumbana nayo mara kadhaa katika upelelezi wao wa baadhi ya vifo vya watu vilivyohusishwa na madawa ya kulevya.

Namba hiyo hivi sasa haipatikani tena na mtu anapojaribu kuipiga hupewa ujumbe "Namba unayopiga haipo kwenye mtandao wetu".

Ampa Mimba Binti Yake, Amuua Akijaribu Kuitoa


Mwanaume mmoja nchini Jordan anashikiliwa na polisi baada ya kumuua binti yake wakati alipojaribu kuitoa mwenyewe mimba aliyompachika.
Mwanaume mmoja nchini Jordan anashikiliwa na polisi kwa makosa ya kumbaka binti yake na kusababisha kifo chake alipoamua kuitoa mimba aliyompachika.

Taarifa ya polisi ilisema kwamba mwanamke mwenye umri wa miaka 19 alifariki dunia siku ya jumapili baada ya kupoteza damu nyingi sana wakati baba yake alipoamua kuitoa mwenyewe mimba aliyompachika.

Taarifa ya polisi haikusema baba huyo alitumia njia gani kuitoa mimba hiyo ya binti yake ambayo ilikuwa na umri wa miezi mitano.

Msemaji wa polisi alisema kwamba tukio hilo lilitokea kwenye mji wa Zarqa kaskazini mashariki mwa Jordan.

Baba huyo ambaye ana umri wa miaka 46 amekiri kuwa alikuwa akifanya mapenzi na binti yake kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita na pia alisema kuwa mama wa binti huyo alikuwa akijua kinachoendelea.

Amefunguliwa mashtaka mashtaka matatu ya mauaji, ubakaji na utoaji mimba.

Baba huyo huenda akahukumiwa adhabu ya kifo iwapo mahakama itamuona ana hatia.

Haijajulikana kama mama wa binti huyo naye atapandishwa kizimbani kwa kuifumbia mambo tabia mbaya ya mume wake.

Liyumba kuwasilisha rufaa l


ALIYEKUWA Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Amatus Liyumba, leo anatarajiwa kukata rufaa na kuiwasilisha mahakama kuu, kupinga hukumu ya miaka miwili jela.
Wakili aliyekuwa akimtetea Liyumba, Majura Magafu amesema kuwa, watawasilisha rufaa hiyo leo kutokana na kutoridhishwa na maamuzi wa mahakama ya Kisutu dhidi ya hukumu hiyo.


Liyumba alihukumiwa Mei 24 mwaka huu, baada ya kukutwa na hatia ya matumizi mabaya ya ofisi akiwa mkurugenzi katika mradi wa majengo pacha ya benki hiyo hali aliyoisababishia serikali kupata hasara ya shilingi bilioni 221.

Unyumba Kila Siku Wasababisha Aione Ndoa Chungu


MWANAMKE mmoja [jina kapuni] amelazimika kuchukua maamuzi ya kuchelewa kurudi nyumbani kwake kutoka kazini ili kukwepa kumpa unyumba mumewe ambaye anadaiwa kutumia dawa za kimasai za kuongeza nguvu za kiume.
Mwanamake huyo ambaye ni mfanyakazi wa kampuni ya utengenezaji wa vinywaji vya cocacola,amekutwa na kadhia hiyo ambayo hajui itamuisha lini ambayo amesema inamkosesha raha ya maisha ya ndoa.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii, mwanamke huyo alisema kuwa mume wake amebadilika kitabia na amezidisha unywaji wa pombe.

Mwanamke aliendelea kusema kuwa mumewe anapolewa huwa mkorofi kupita kiasi.

Kubwa ya yote amesema kuwa anafanya maamuzi ya kuchelewa kurudi nyumbani kwake sasa hivi kwa kuwa mume wake huyo amekuwa akionekana kupenda zaidi unyumba tofauti na miaka ya nyuma hali inayofanya achoshwe na zoezi hilo.

“Sikia yaani nilivyochoka hapa ngoja nikaekae hapa hadi masaa yaende kwanza, nikirudi nitamkuta ameshalala hataulizia tena mana nisikufiche nimechoka kila siku nakandamizwa inachosha”

Amedai kuwa akiwahi kurudi tu na kumkuta mumewe amesharudi basi ni kazi moja tu hadi uchwao.

Hata hivyo alidai kuwa huenda anahisi mume wake anatumia vilevi ama hizo dawa za kimasai zinazofanya awe na nguvu kupita kiasi hali ambayo inampa shida na kutamani kuchelewa kurudi nyumbani kwake.

Amesema ameishaishi na mume wake huyo kwa miaka sita sasa na wamebahatika kupata watoto wawili mapacha wa kike na kiume ambao kwa sasa wana umri wa miaka miwili na nusu.

AIBU kubwa jana ilimpata mwnaume mmoja


AIBU kubwa jana ilimpata mwnaume mmoja kwa kuchapwa vibao na mwanamke ambaye hakumfahamu kutokana na shida ya usafiri iliyowakumba wawili hao.
MWanaume huyo alipigwa vibao na mwanamke ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake ndani ya daladala baada ya mwanamke huyo kukerwa kwa kukanyagwa na baba huyo.

Kabla ya kuchapwa vibao hivyo na mwanamke huyo ambaye hakumfahamu kabisa, mwanamke huyo katika pilikapilika ya kugombania daladala na kufanikiwa kuingia ndani alijikuta amekosa siti na kuchukua ndoo yake aliyokuwa akitoka nayo katika pilikapilika zake na kuikalia sehemu ambayo abiria wanatakiwa wasimame.

Wakati watu wengine wanaingia ndani ya basi hilo mwanamke huyo alijikuta akikanyagwa miguu na kuwapa tahadhari kuwa watu wasimkanyage.

Basi hilo lilivyoanza safari zake na abiria kuzidi kuongezeka kila liliposimama kwenye kituo, kasheshe ilimkumba mwanaume ambaye aliamrishwa na konda asogee nyuma kuwapa nafasi abiria wengine. Mwanaume huyo katika kurudi nyuma alimkanyaga mwanamke huyo.

Ghafla mama huyo aliinuka na kuchukua uamuzi wa kumnasa kibao mwanaume aliyemkanyaga na kumshambulia kwa maneno kuwa amemuumiza hadi anasikia maumivu.

Inaonekana mwanaume huyo alikuwa mstarabu na hakupewa kipaji cha kuongea alimwambia mama huyo maneno mawili tu ‘kwanini unanipiga? Wakati anamaliza mama huyo aliinua mkono na kumuwasha kibao kingine cha pili

Bila kuamini mwanaume huyo ambaye muonekano wake ulikuwa ni bonge la mwanaume aliyejaaliwa umbile kubwa hakubishana na mama huyo na kubaki kimya huku abiria wengine wakionekana kumshambulia mama huyo kwa maneno kwa kitendo chake ambacho si cha kistaarabu alichomfanyia mwanaume huyo.

Mkasa huo wa aina yake ulitokea jana majira ya saa 12:49, ndani ya basi linalofanya safari zake kati ya Mbagala na Kivukoni.

Familia Iliyoteketezwa Kwa Moto Yazikwa, Aliyeanzisha Moto Akamatwa


MTUHUMIWA Shemsa Mpelela [22] anayesadikiwa kuwa kuichoma moto nyumba na kupelekea vifo vya watu watano wa familia moja amekamatwa.
Mtuhumiwa huyo ni mlinzi wa Shule ya Sekondari Aboud Jumbe iliyopo Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Ilidaiwa kuwa kabla ya kukamatwa kwake juzi, Shemsa alikwenda kwa kaka yake eneo la Kigamboni, Kisiwani, kuomba nauli ili aondoke Dar es Salaam ndipo watu walipomwona na kutoa taarifa Polisi.

Pia marafiki wawili wa mtuhumiwa huyo walikamatwa akiwamo mwanaume anayedaiwa kushirikiana naye kuichoma moto nyumba hiyo na kusababisha vifo vya watu watano wa familia moja.

Rafiki wa mtuhumiwa aliyeenda nae eneo la tukio alisikika kijiweni akisema kuwa alimuona rafiki yake huyo akinunua lita moja moja za petroli na zilipofika lita 10 alimwomba amsindikize bila kujua adha ya rafiki yake huyo.

Aliendelea kueleza kuwa, alishangazwa kuona wamefika katika nyumba hiyo na kuona mwenzake akichoma nyumba na wakaondoka eneo la tukio haraka na kukaa mbali huku wakishuhudia nyumba hiyo inavyoteketea, ndipo wasamaria walipotoa tarifa polisi.

Jana marehemu wote walizikwa kwa pamoja katika mazishi yaliyofanyika Tungi, Kigamboni, Dar es Salaam.

Miili ya marehemu iliwasili nyumbani kwa Onesmo saa 9 alasiri na sala ya kuwaombea iliongozwa na Mchungaji wa Kanisa la Anglikana wa Tungi, Obed Ntigogozwa na baadaye majeneza yote matano yalipelekwa kuzikwa eneo la makaburi la Vijibweni.

Hata hivyo miili ya marehemu hao haikuoneshwa, kutokana na kuharibika kwa miili hiyo iliyoteketea kwa moto.

Marehemu hao walioteketea kwa moto wakiwa katika nyumba yao yenye chumba kimoja ni baba mwenye nyumba John Onesmo (32), Catherine Jackson (25), watoto wao wawili Oliver (2) na Joyce John (5) na Esther Mugulu (20) ambaye ni mdogo wa Catherine.

Marekani yaonya ugaidi Kombe la Dunia


Serikali ya Marekani imetoa onyo kwa raia wake kuwa Afrika Kusini inakabiliwa na tishio la ugaidi wakati wa Kombe la Dunia.

Imesema matukio yanayoshughulisha umati mkubwa wa watu huwavutia magaidi kufanya mashambulio.

Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema, " Kuna hatari kubwa kuwa makundi ya wapiganaji yanaweza kufanya ugaidi ndani ya Afrika Kusini siku za usoni."

Onyo hilo limetolewa wakati Rais Barack Obama akiitakia kheri timu ya soka ya Marekani.

Bw Obama, aliyeambatana na aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Bill Clinton aliwaaga wachezaji hao kwenye ikulu ya White House, " Nataka tu kusema jinsi gani tunavyosikia fahari juu ya timu hiyo."

Amesema, " Kila mmoja atakuwa anawashangilia."

"Na japokuwa mara nyingi hatukumbuki hilo hapa Marekani, hili litakuwa shindano kubwa zaidi la soka duniani."

Katika taarifa iliyotolewa, wizara ya mambo ya nje imesema haina taarifa kamili ya vitisho wakati wa mashindano hayo, lakini vitisho vimeripotiwa na vyombo vya habari.

Afrika Kusini imeandaa maelfu ya polisi waliopitia mafunzo maalum kushughulika na usalama wa mashabiki.

Takriban watu 350, 000 wanatarajiwa kutembelea Afrika Kusini kwa ajili ya Kombe la Dunia, linalofanyika kwa mara ya kwanza barani Afrika na kuanza Juni 11.

Waasi wajinufaisha na madini DRC


Ripoti iliyotolewa na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa imesema makundi ya waasi mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yanaendelea kukusanya ushuru kinyume cha sheria kutoka kwa watu wanaohudumu katika kiwanda cha kuchimba madini ya dhahabu.

Ripoti hiyo pia imewasilisha ushahidi kuthibitisha kuwa waasi hao wanatumia stakabadhi gushi za Umoja huo ili kuyauza madini hayo katika mataifa jirani.

Waasi wa CNDP vile vile wametuhumiwa kuweka vituo vya ukaguzi na kuwatoza wenye magari na raia kodi kinyume cha sheria.

Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo ina mali asili za madini nyingi lakini makundi ya waasi wenye silaha wanadhibiti biashara hii.

Makundi haya yanaarifiwa kupata faida kutokana na biashara hii ya mamilioni ya dola kutokana na madini na kudhibiti migodi kwa nguvu na kuomba hongo au kodi.

Mchango wa biashara ya madini umetambulika kuwa moja ya sababu zinazochochea vita na kuchangia ukiukwaji wa haki za binadamu mashariki mwa nchi hii tangu kuanza kwa vita.

Juhudi za kufukua miili Uganda zaendelea


Maafisa wa shughuli ya uokoaji nchini Uganda wanasema wanajitahidi kufukua mamia ya miili ya watu waliozikwa hai kufuatia maporomoko ya ardhi katika wilaya ya Bududa miezi mitatu iliyopita.

Kwa mujibu wa ripoti ya serikali zaidi ya watu mia mbili hawajulikani waliko, huku miili mia moja ikiwa imefukuliwa.

Kiongozi wa shughuli hiyo Luteni Kanali Wilson Kabera, amedokeza shughuli hiyo imetatizika kutokana na mvua kubwa na pia matatizo ya kuharibika kwa mitambo na mashini zinazotumika kufukua miili hiyo.

Zaidi ya watu elfu nane walihama makwao kutokana na maporomoka hayo ya ardhi.

Omar al-Bashir aapishwa nchini Sudan


Rais wa Sudan, Omar al-Bashir, leo ameapishwa kuendelea na mamlaka ya rais, licha ya utata uliozuka katika uchaguzi wa mwezi uliopita.


Kumekuwa na malalamiko dhidi ya Bashir kutokana na uchaguzi mwezi uliopita
Mahakama ya kimataifa ya uhalifu ya ICC inamtaka kiongozi huyo kufikishwa mbele yake, kutokana na visa vya uhalifu katika eneo la Darfur.

Wageni wa nchi nyingi walioalikwa hawakuhudhuria sherehe hizo za kuapishwa, lakini viongozi kutoka nchi tano za Afrika walishiriki.

Umoja wa Mataifa ulikuwa umetangaza hapo awali kwamba wajumbe wake wa amani katika nchi hiyo watahudhuria sherehe hizo.

Akiapishwa, rais Bashir alilihutubia bunge mjini Khartoum kwa kipindi cha nusu saa.

Marais wa Ethiopia, Chad, Malawi, Mauritania na Djibouti walikuwa ni miongoni mwa walioalikwa.

Shirika la kutetea haki za kibinadamu la Human Rights Watch (HRW), limeelezea kwamba ni wazi serikali zinazotaka kuhakikisha haki inatendeka katika kuutatua mzozo wa Darfur kamwe hazikutaka kushiriki katika sherehe za kuapishwa rais Bashir.

Daktari wa Rwanda akamatwa Ufaransa.

Maafisa wa polisi nchini Ufaransa hatimaye wamemkamata daktari kutoka Rwanda, Eugene Rwamucyo, kwa kutuhumiwa kuhusishwa na mauaji ya watu wengi mwaka 1994.


Daktari Rwamucyo alikamatwa kutokana na hati iliyotolewa na serikali ya Rwanda
Eugene amekuwa akitafutwa na polisi ya kimataifa, Interpol, tangu mwaka 2006.

Aliachishwa kazi katika hospitali moja ya kaskazini mwa Ufaransa, mwezi uliopita.

Maafisa wa serikali ya Rwanda, wanaodai kwamba daktari Rwamucyo alihusishwa na uhalifu katika mazingira ya vita wakati wa mauaji hayo ya watu wengi, wameelezea kufurahia hatua hiyo.

Daktari Rwamucyo amekanusha madai hayo, akisema ni kampeni na njama ya serikali ya Rwanda kumharibia sifa.

Alikamatwa mjini Sannois, kaskazini mwa Ufaransa, mara tu baada ya kuhudhuria mazishi ya afisa mmoja wa zamani wa serikali ya Rwanda, na ambaye pia alikuwa ameshitakiwa kwa mauaji ya watu wengi.

Habari hizo ni kwa mujibu wa maafisa wa serikali wa Ufaransa.

Hatua ya kukamatwa kwake inafuatia juhudi za Ufaransa kuwakamata washukiwa wa mauaji ya watu wengi nchini Rwanda, huku uhusiano wa kidiplomasia ukiendelea kuimarika kati ya nchi hizo mbili.

Magazeti binafsi rukhsa Zimbabwe

Magazeti manne ya binafsi yanayochapishwa kila siku Zimbabwe yamepewa kibali na tume iliyoundwa na serikali ya muungano ili kufanya marekebisho ya vyombo vya habari.


Magazeti manne yapewa kibali Zimbabwe
Vyombo vya habari vya Zimbabwe kwa sasa vimeshamiri magazeti ya serikali.

Kibali kimoja kimetolewa kwa Daily News, gazeti lililokuwa likimkosoa Rais Robert Mugabe, lililofungwa mwaka 2003.

Bw Mugabe na Waziri mkuu Morgan Tsvangirai wamekuwa katika serikali ya kugawana madaraka tangu mwaka 2008.

Tume ya habari ya Zimbabwe (ZMC) iliundwa Desemba 2009 chini ya makubaliano ya kufanya mabadiliko kwa vyombo vya habari, ikiwemo kutoa vibali kwa magazeti mapya, redio na televisheni.

Kwa sasa, vyombo vya habari vya binafsi nchini humo vinapewa vipingamizi vizito.

Shirika la habari la Reuters limemnukuu mwenyekiti wa ZMC Godfrey Majonga akisema, " Tuko hapa kuwapa Wazimbabwe fursa ya kupata habari."

Mwaka 2002, Bw Mugabe alianzisha sheria kali kwa vyombo vya habari ikiwataka waandishi wa habari na magazeti kujisajili kwa serikali na iwapo mtu akashindwa kutekeleza hilo hufungwa gerezani.

Waandishi wa habari pia huweza kufungwa gerezani kwa "kuchapisha taarifa za uongo."

Waandishi wa habari wa gazeti binafsi la Daily News walikamatwa, na kiwanda cha kuchapisha magazeti kililipuliwa kabla ya gazeti hilo kufungwa rasmi mwaka 2003.

MSF yahofia kupunguzwa misaada

Shirika la kutoa misaada ya afya, Medecins Sans Frontieres, limeonya kwamba ikiwa jamii ya kimataifa itapunguza misaada, basi kuna hatari ya mamilioni ya watu kuambukizwa ukimwi na HIV, na kuhatarisha kampeni dhidi ya ugonjwa huo.

Shirika hilo limefanya utafiti katika mataifa manane ya Afrika, na kuelezea kwamba kupunguzwa kwa misaada hiyo ni jambo ambalo limeanza kuziathiri nchi hizo.

MSF imeelezea kwamba hazina ya dunia ya Global Fund tayari imepunguza misaada kwa asilimia nane hadi kumi na mbili.

Shirika hilo limefafanua kwamba hata serikali ya Marekani, kupitia mpango wake wa kutoa misaada ya dharura unaosimamiwa na rais, President's Emergency Plan for AIDS (PEPFAR), pia umepunguza msaada wake kwa nchi wahitaji.

Benki ya dunia, Umoja wa Ulaya na mpango wa rais wa zamani wa Marekani, Clinton Health Initiative, ni baadhi ya mashirika zaidi yaliyopunguza misaada.

Amnesty: Mataifa makubwa yakiuka haki

Shirika la kutetea haki za kibinadam la Amnesty International limeshutumu baadhi ya mataifa yenye ushawishi mkubwa duniani kwa kukiuka haki za kibinadam na kuvuruga juhudi za kimataifa za kuwatendea haki waliodhulumiwa.

Katika ripoti yake ya kila mwaka shirika hilo la amnesty limeyataka mataifa 20 tajiri duniani maarufu kama G-20 kujisajili kama wanachama wa mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita ICC.

Mataifa ya Marekani, Uchina, Urusi, India na Indonesia yamekataa kutambua mahakama hiyo.

Kwa mjibu wa ripoti hii, mataifa mia moja kumi na moja yameripotiwa kuendeleza mateso dhidi ya raia wake, mataifa mengine hamsini na tano yamearifiwa kuwafungulia watuhumiwa wasio na hatia kesi zisizo kuwa za haki, huku mataifa tisini na sita yakiwazuia wanachi wake kujieleza wazi.

Pamoja na hayo shirika hilo linadai kwamba serikali zenye ushawishi mkubwa duniani zinaendelea kuvuruga juhudi za kimataifa za kuwatendea haki waliodhulumiwa.

Shirika hilo pia limesema ulegevu wa kutochukua maamuzi makali katika baraza la haki za kibinadam la Umoja wa Mataifa ni ishara kuwa jamii ya kimataifa imeshindwa kuwajibika wakati inapohitajika.

Limekashifu muungano wa Afrika kwa kutoshirikiana na mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa kivita katika kutekelezwa kwa kibali cha kukamatwa kwa rais wa Sudan Omar al Bashir, kuhusiana na uhalifu wa kivita katika eneo la darfur.

Lakini limetaja kibali hicho cha kwanza cha kukamatwa kwa rais anayehudumu kama hatua muhimu ya kuafikiwa haki na inatoa ujumbe kwamba hakuna aliyejuu ya sheria.

Mourinho sasa ni meneja wa Real Madrid

Klabu ya Real Madrid ya Uhispania imetangaza kwamba itamjulisha Jose Mourinho rasmi kwa mashabiki wao, Jumatatu ijayo.
Klabu kilitoa taarifa kuthibitisha hayo.

Marais wa vilabu vya Inter Milan ya Italia, na Real Madrid, walikutana Ijumaa mjini Milan, Italia, kutatua masuala yote, hasa ya kifedha, kuhusiana na Jose Mourinho kuhama kutoka Inter, na kuelekea Uhispania.

Real Madrid wameshawahi kunyakua ubingwa wa Ulaya mara tisa.

Jose Mourinho anaondoka Inter baada ya msimu uliokuwa wa fanaka mno, kupata ushindi katika mashindano matatu muhimu Italia, ikiwa ni pamoja na kuwa klabu bingwa barani Ulaya.

Hata hivyo klabu ya Inter haikutoa maelezo kamili katika taarifa hiyo, kuhusu mapatano hayo kati ya rais wa klabu Massimo Moratti na mwenzake wa Real, Florentino Perez.

Lakini vyombo vya habari nchini Uhispania vimekuwa vikielezea kwamba Inter watapata euro milioni nane, ambazo ni sawa na dola milioni 9.80.

Mourinho aliiongoza Inter kupata vikombe vitatu muhimu, na alimalizia kwa ushindi katika fainali ya klabu bingwa Ulaya, dhidi ya Bayern Munich ya Ujerumani katika uwanja wa Bernabeu, mjini Madrid.

UEFA kuzindua sheria mpya


Shirikisho la mchezo wa Soka barani Ulaya UEFA, hii leo linatarajiwa kuidhinisha sheria mpya ambazo zitazuia vilabu kutumia fedha zaidi wanavyopata.

UEFA ambayo husimamia mhezo huo barani ulaya imetumia muda wa miaka mitatu kubuni sheria hizo ambazo zinatarajiwa kuidhinishwa wa kamati kuu ya shirikisho hilo.

Sheria hizo zitazuia vilabu kupata hasara kila mwaka na pia kuzuia wamiliki tajiri kuwekeza fedha nyingi kwa kununua wachezaji wapya. Hata hivyo sheria hiyo itaruhusu vilabu kutumia kiasi chochote cha pesa kununua wachezaji mradi tu wana fedha za kutosha.


Ikiwa sheria hizo zingelikuwa zinatumika kwa sasa, mabingwa wa ligi kuu ya Uingereza Chelsea hawangeruhusiwa kushiriki kwenye ligi ya klabu bingwa barani Ulaya msimu ujao.

Wayne Rooney akanusha hali yake si nzuri


Mshambuliaji wa England Wayne Rooney amepuuza taarifa kwamba bado anaendelea kusumbuliwa na maumivu wakati zimesalia siku chache kabla kuanza fainali za Kombe la Dunia.
Rooney, mwenye umri wa miaka 24, msimu uliopita alikuwa akisumbuliwa na matatizo ya kiwiko cha mguu na nyonga na siku ya Jumatatu alipatwa na maumivu ya kukakamaa shingo wakati England ilipoilaza Mexico mabao 3-1 katika mchezo wa Kimataifa wa kirafiki.

Lakini amesema: "Hali yangu ni nzuri na nipo imara. Tangu tulipokusanyika pamoja wachezaji wa England nimekuwa nikifanya mazoezi kila siku.

"Sijapata matatizo ya kiwiko cha mguu, taarifa iliyoandikwa ni upuuzi mtupu. Nilipata matatizo kidogo ya kukakamaa shingo lakini yamekwisha."

Rooney ndiye mchezaji muhimu zaidi kwa England katika mashindano ya Kombe la Dunia yatakayofanyika Afrika Kusini, baada ya kuonesha kiwango kikubwa cha kupachika mabao ambapo aliifungia Manchester United mabao 34 msimu uliomalizika.

Mshambuliaji huyo wa England alicheza dakika zote 90 dhidi ya Mexico katika uwanja wa Wembley, laikini alishindwa kuongeza bao katika jumla ya mabao 25 aliyokwishafunga akiichezea England katika mechi yake ya 59 ya kimataifa.

Amefunga mara moja tu katika mechi saba zilizopita akiichezea England, lakini anaamini kuihakikishia timu yake anauwezo wa kucheza ni muhimu zaidi ya kufunga mabao.

Fran Merida ahama Arsenal aenda Atletico

Kiungo wa Arsenal Fran Merida anarejea Hispania ambako atajiunga na klabu ya Atletico Madrid akiwa mchezaji huru.
Merida mwenye umri wa miaka 20, amejiunga na Atletico Madrid kwa mkataba wa miaka minne, alijiunga na Arsenal tangu mwaka 2006 akitokea Barcelona.

Lakini ameshindwa kujitutuma katika timu ya kwanza na msimu uliopita alitumiwa akiwa mchezaji wa akiba katika michezo minne ya ligi.

Alifunga bao dhidi ya Bolton katika mchezo wa ligi na alianza tangu mwanzo katika michezo minne ya kuwania kombe la Carling na FA Cups na pia Ligi ya Ulaya.

Merida pia alifunga bao muhimu wakati Arsenal walipoifunga Liverpool mabao 2-1 mwezi wa Oktoba katika mechi ya mchakato wa Kombe la Carling.

Mchezaji huyo raia wa Hispania, ambaye mkataba wake na Arsenal unamalizika tarehe 30 mwezi wa Juni, anatazamiwa kutambulishwa kwa mabingwa hao wa Ligi ya Europa siku ya Ijumaa katika uwanja wa Vicente Calderon.

Atletico pia imethibitisha kwamba Quique Sanchez Flores amesaini mkataba mpya wa kuifundisha klabu hiyo kwa msimu mmoja zaidi.

Flores, ambaye awali alizifundisha Valencia na Getafe pamoja na Benfica ya Ureno, alichukua nafasi ya Abel Resino mwezi wa Oktoba mwaka 2009.

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 45 aliiwezesha Atletico kushinda Ligi ya Europa katika mchezo wa fainali walipoilaza Fulham mabao 2-1, ikiwa ni mara yao ya kwanza kushinda taji kubwa tangu mwaka 1996 ingawa katika fainali ya Kombe la Hispania walipoteza kwa kufungwa mabao 2-0 na Sevilla.

Muimbaji ufunguzi Kombe la Dunia afariki

Muimbaji wa mtindo wa opera aliyeteuliwa na Nelson Mandela kuimba wakati wa sherehe za ufunguzi wa Kombe la Dunia amefariki dunia baada ya kuuguwa homa ya uti wa mgongo.

Siphiwo Ntshebe, mwenye umri wa miaka 34, alilazwa hospitali mjini Port Elizabeth wiki iliyopita na alifariki dunia siku ya Jumaanne kwa mujibu wa kampuni inayouza nyimbo zake, Epic Records.

Alitazamiwa kuimba wimbo wake mpya "hope" katika sherehe za ufunguzi tarehe 11 mwezi wa Juni mjini Johannesburg. Wimbo huo una ujumbe maalum wa matumaini na imani uliotungwa na kutolewa na Bwana Mandela.

Mwaandishi wa BBC mjini Johannesburg, Pumza Fihlani anasema Ntshebe hakuwa maarufu sana nchini Afrika Kusini. Hata hivyo kwa yeye kutumbuiza katika sherehe za Kombe la Dunia kungempa fursa ya kujulikana zaidi nchini mwake

Thursday, May 27, 2010

Aliyejaribu Kuulipua Ubalozi wa Marekani Afikishwa Mahakamani

MTOTO Nassib Mpamka (15) mwanafunzi wa kidato cha pili, katika shule ya Sekondari Biafra Dar es Salaam, anayekabiliwa na tuhuma za kufanya jaribio la kuulipua Ubalozi wa Marekani Dar es Salaam, amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Nassib alifikishwa mahakamani hapo jana, chini ya ulinzi wa maofisa wa Polisi.

Hata hivyo mahakama hiyo haikuwa tayari kusoma mashtaka hayo kwa kudai kuwa jalada lake lilihamishiwa mahakama ya watoto na mashauri juu ya kesi hiyo hayaruhusiwi kuripotiwa na vyombo vya habari kwa mujibu wa sheria za nchi.

Mwanafunzi huyo alionekana akihamishwa kutoka mahakama ya kawaida kupelekwa mahakama ya watoto lakini baadae alirudishwa tena mahakama ya kawaida baada ya kutopatikana kwa hakimu wa kusikiliza shauri lake kwenye mahakama ya watoto.

Juhudi za wanahabari za kutaka kujua hatma ya mtoto huyo kama alisomewa mashitaka ama la hazikuzaa matunda kwa kuwa ilidaiwa kesi za watoto zinakuwa zinaendeshwa kwa usiri

Pia mujibu wa tarifa kutoka ndani ya jeshi la polisi ilidaiwa kuwa mtoto huyo alipelekwa katika mahabusu ya watoto iliyoko Upanga jijini Dar es Salaam.

Awali, Mei 16 mwaka huu, majira ya saa 2:30 usiku, Nassib Mpamka alidaiwa kufika katika maeneo ya jengo la ubalozi wa Marekani na alirusha chupa iliyokuwa imejaa mafuta ya taa iliyowekwa utambi na chupa hiyo iliangukia katika eneo ambalo lilikuwa karibu na maegesho ya malori ya kubebea maji.

Nia ya Nasibu ilikuwa ni kuyalipua malori hayo na kusababisha moto mkubwa ambao ungeuteketeza ubalozi lakini walinzi waliwahi kumkamata kabla hajarusha bomu lake la pili mafuta ya taa.

Familia Iliyoteketezwa Kwa Moto Yazikwa, Aliyeanzisha Moto Akamatwa

MTUHUMIWA Shemsa Mpelela [22] anayesadikiwa kuwa kuichoma moto nyumba na kupelekea vifo vya watu watano wa familia moja amekamatwa.
Mtuhumiwa huyo ni mlinzi wa Shule ya Sekondari Aboud Jumbe iliyopo Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Ilidaiwa kuwa kabla ya kukamatwa kwake juzi, Shemsa alikwenda kwa kaka yake eneo la Kigamboni, Kisiwani, kuomba nauli ili aondoke Dar es Salaam ndipo watu walipomwona na kutoa taarifa Polisi.

Pia marafiki wawili wa mtuhumiwa huyo walikamatwa akiwamo mwanaume anayedaiwa kushirikiana naye kuichoma moto nyumba hiyo na kusababisha vifo vya watu watano wa familia moja.

Rafiki wa mtuhumiwa aliyeenda nae eneo la tukio alisikika kijiweni akisema kuwa alimuona rafiki yake huyo akinunua lita moja moja za petroli na zilipofika lita 10 alimwomba amsindikize bila kujua adha ya rafiki yake huyo.

Aliendelea kueleza kuwa, alishangazwa kuona wamefika katika nyumba hiyo na kuona mwenzake akichoma nyumba na wakaondoka eneo la tukio haraka na kukaa mbali huku wakishuhudia nyumba hiyo inavyoteketea, ndipo wasamaria walipotoa tarifa polisi.

Jana marehemu wote walizikwa kwa pamoja katika mazishi yaliyofanyika Tungi, Kigamboni, Dar es Salaam.

Miili ya marehemu iliwasili nyumbani kwa Onesmo saa 9 alasiri na sala ya kuwaombea iliongozwa na Mchungaji wa Kanisa la Anglikana wa Tungi, Obed Ntigogozwa na baadaye majeneza yote matano yalipelekwa kuzikwa eneo la makaburi la Vijibweni.

Hata hivyo miili ya marehemu hao haikuoneshwa, kutokana na kuharibika kwa miili hiyo iliyoteketea kwa moto.

Marehemu hao walioteketea kwa moto wakiwa katika nyumba yao yenye chumba kimoja ni baba mwenye nyumba John Onesmo (32), Catherine Jackson (25), watoto wao wawili Oliver (2) na Joyce John (5) na Esther Mugulu (20) ambaye ni mdogo wa Catherine.

Chama cha CCJ Champa Tendwa Wiki Moja

Chama cha Jamii CCJ kimempa wiki moja msajili wa vyama vya siasa nchini John Tendwa ahakikishe ametoa usajili wa kudumu kwa chama hicho.
Msemaji mkuu wa chama cha CCJ Fred Mpendazoe alitoa tamko hilo wakati akiongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.

Mpendazoe alisema kuwa mnamo tarehe 17 mei mwaka huu msajili wa vyama vya siasa nchini John Tendwa akizungumza na waandishi wa habari alieleza kuwa Ofisi yake kwa wakati huu haina fedha za uhakiki wa wanachama wa chama cha jamii cha CCJ ili hatimaye chama hicho kiweze kupata usajili wa kudumu na kushiriki uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Mpendazoe aliwambia wandishi wa habari kuwa uongozi wa chama hicho cha CCJ umesikitishwa na kauli hiyo ya msajili wa vyama hapa nchini kwani imetolewa ikionyesha nia ya wazi ya kutotaka kufanya uhakiki na hatimaye kutotoa usajili wa kudumu kwa chama hicho.

Alisema kuwa ni muhimu sana kauli hiyo iliyotolewa na msajili wa vyama isiachwe bila kutolewa majibu.

Mpendazoe alitabainisha kuwa lengo la usajili wa muda kama inavyojulikana lilikuwa ni kuwapa nafasi ya kujiandaa na usajili wa kudumu lakini hali haikuwa hivyo kwani msajili wa vyama vya siasa John Tendwa ameonesha nia yake ya kutotaka kutoa usajili wa kudumu kwa chama hicho jambao ambalo ni kinyume na sheria ya usajili wa vyama.

Mpendazoe alisema kuwa ni heri wananchi wakafa wamesimama kuliko kuishi wamepiga magoti.

Mpendazoe alisema kuwa uongozi wa CCJ unampa Tendwa wiki moja ahahakishe anakipatia usajili wa kudumu chama hicho.

Kila Nyumba Tanzania Kuwa na Maji ya Uhakika Ifikapo Mwaka 2013

RAIS Jakaya Kikwete amesema kuwa kero ya maji nchini inatarajiwa kuisha kabisa ifikapo mwaka 2013.
Hayo aliyasema jana katika ukumbi wa Karimjee katika majumuisho ya ziara yake ya siku moja jijini Dar es Salaam.

Alisema upo mradi mkubwa unaotarajiwa kuanza mapema mwaka huu wa kuvuna maji yaliyoko ardhini katika eneo la Kimbiji ambao ukikamilika mwaka 2013 vyanzo vyote vitakuwa na uwezo wa kutoa maji lita milioni 710 kwa siku ikiwa ni pamoja na kukamilika kwa upanuzi wa vyanzo vya maji vya Ruvu Chini na Ruvu Juu.

Alisema kwa sasa mahitaji ya maji katika Jiji la Dar es Salaam ni lita milioni 450 lakini zinazopatikana ni lita milioni 300 kutoka vyanzo mbalimbali ikiwemo Ruvu chini na Juu, Mtoni na visima.

Rais Kikwete aliwaagiza watendaji wa halmashauri zote wakishirikiana na Mamlaka ya Majisafi na Majitaka (DAWASA) na Shirika la Majisafi na Majitaka (DAWASCO) na Wizara ya Maji na Umwagiliaji kuondoa kero ya maji katika kipindi cha mpito kwa kuchimba visima vingi virefu na kumaliza kero hiyo ya maji inayowasumbua wananchi.

Mwanafunzi anyofolewa sehemu zake za siri -Manyara


MTOTO wa kike aliyekuwa akisoma darasa la pili mkoani Manyara amenyofolewa sehemu zake za siri na kisha maiti yake kuwekwa kwenye kiroba kabla ya kutupwa kwenye kichaka mkoani humo.
Tukio hilo la kusikitisha liligundulika jana, huko eneo la Mbuyu wa Wajerumani mkoani Manyara baada ya wananchi kugundua maiti ya mtoto huyo wa kike aliyekuwa akisoma darasa la pili ikiwa imefichwa kwenye kiroba.

Wiki moja nyuma walezi wa mtoto huyo waliripoti katika vituo vya polisi kuwa mtoto huyo alipotea katika mazingira ya kutatanisha.

Katika juhudi za kumsaka mtoto huyo jana wananchi waliona kiroba kilichotelekezwa porini na kukichunguza ndipo ndani yake waligundua mwili wa mtoto huyo ukiwa humo.

Kutokana na tukio hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Manyara linawashikilia waliokuwa walezi wa mtoto huyo ambao ni Fatma Juma na Hamad Athuman ambao ilidaiwa walimuomba mtoto huyo kwa mzazi wao waje kumlea.

Imedaiwa kuwa watuhumiwa hao ambao kwa sasa wako chini ya ulinzi wa polisi ni wafanyabiashara wa madini wa muda mrefu

Wanashikiliwa na uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio hilo unafanywa na polisi ili kubaini kama tukio hilo limeendana na mambo ya ushirikina kama watu wanavyodai na kuhisi ama la.

WATU 22 wamejeruhiwa katika ajali -Dar


WATU 22 wamejeruhiwa vibaya na kupelekea kufikishwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kutibiwa baada ya kupata majeraha yaliyotokana na daladala waliyokuwa wakisafirira kupinduka katika Barabara ya Nyerere Dar es Salaam jana asubuhi.
Watu hao walikuwa ndani ya basi la abiria lililokuwa likifanya safari zake kati ya Gongolamboto na Kivukoni na walipata ajali eneo la Tanangozi kwenye brabara hiyo ya Nyerere .

Basi hilo lilipinduka na abiria hao kulaliana na basi hilo lilijaza abiria kupita kiasi kutokana na shida ya usafiri majfira ya asubuhi.

Majeruhi hao waliweza kupata majeraha katika sehemu mbalimbali za mwilini zikiwemo usoni, mikononi, kishwani na sehemu mbalimbali za mwili.

Masikini mtoto huyu!


MTOTO Mohamed Ridhiwani mwenye umri wa miezi mitano amefariki dunia baada ya kutumbukia kwenye ndoo iliyojaa maji huko maeneo ya Sabasaba, Mtoni Mtongani jijini Dar es Salaam.
Akitoa taarifa juu ya tukio hilo kwa waandishi wa habari, Kamanda wa Polisi Mkoa Temeke, Bw. Elias Kalinga alisema kuwa tukio hilo lilitokea jana majira ya saa 12:00 jioni.

Amesema kuwa mtoto huyo alikuwa amelazwa kitandani ndani chumbani na mama yake.

Amesema mtoto huyo wakati yuko katika usingizi alianguka kutoka kitandani alikokuwa amelala na kutumbukia kwenye ndoo ya maji iliyokuwa karibu na kitanda hicho bila ya mama yake kuwa na taarifa.

Hivyo kutokana na mtoto huyo kuwa na umri huo alishindwa kujitetea na kufariki dunia baada ya kunywa maji mengi.

Wazazi wake waligundua tukio hilo mtoto huyo akiwa tayari ameishafariki. Taarifa zilipelekwa kituo cha polisi kwa uthibitisho na polisi mkoani Temeke walithibitisha tukio hilo.

Maiti ya mtoto huyo ilichukuliwa na kwenda kuhifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Temeke.

Msafara wa Kikwete Mmmh! chupuchupu


MAGARI aliyokuwa amepanda Rais Jakaya Kikwete, katika ziara yake ya siku moja jijini Dar es Salaam, yalileta hitilafu baada ya magari hayo kuchomoka matairi yake katika maeneo tofauti yakiwa safarini.
Tukio la kwanza lilitokea jana maneneo ya Kimara Mwisho wakati Rais alipokuwa akitoka Kimara Bonyokwa katika ziara yake ya siku moja kutembelea maeneo yaliyokuwa na matatizo ya ukosaji maji kwa muda mrefu.

Msafara huo ulilazimika kusimama ghafla kutokana na gari alilokuwa amepanda kuchomoka tairi lake la mbele na baadaye Rais alilazimika kuhamishwa kutoka gari hilo kwenda jingine na bendera kuhamishwa kutoka gari hilo na kuwekwa gari alilopanda kwa mara ya pili.

Zoezi hilo ambalo lilishuhudiwa na wananchi na wakazi wa maeneo kufurika eneo la tukio kumshuhudia Rais wao akitoka gari moja kuingia jingine na walinzi wake pia kulazika kuhama ndani ya gari hilo.

Katika tukio la pili ya hitilafu msafara huo wakati unatoka eneo la Keko Toroli, ghafla ulisimama katika eneo la bandarini karibu na ofisi za BP baada ya gari alilokuwemo rais kuwa na hitilafu katika tairi lake la nyuma upande wa kulia lililochomoka.

Hivyo Rais alilazimika kuhamishwa tena kutoka kwenye gari hilo kwenda jingine.

Hivyo ndivyo ilivyokuwa katika msafara huo wa Rais na kuingia dosari na Rais kunusurika na ajali ambayo labda ingeweza kumpotezea maisha au kupoteza viungo kutokana na magari hayo kuleta hitilafu katikati ya msafara.

Liyumba jela miaka miwili


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imemuhukumu kifungo cha kwenda miaka jela aliyekuwa Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa Benki Kuu (BOT) Amatus Liyumba (62) baada ya kupatikana na hatia ya matumizi mabaya ya ofisi ya Umma.

Hukumu hiyo ilitolewa jana mahakamani hapo na Hakimu Lameck Mlacha wa Mahakama hiyo kwa kushirikiana na jopo la mahakimu watatu waliokuwa wakiongozwa na Hakimu Mkazi Edson Mkasimongwa wakati upande wa mashitaka ulikuwa ukiongozwa wakili Hilaly Mkate.

Katika hukumu hiyo mahakimu walionekana kutofautiana kwa maamuzi juu ya hakumu hiyo ambapo mmoja katika mahakimu waliokuwa wakisikiliza kesi hiyo kutofautiana na wenzake kwa kusema mshitakwia hakuwa na hatioa ya kosa hilo.

Hata hivyoo hukumu iliyotumika kumfunga mshitakiwa huyo ni ile iliyoonekana maoni yanayofanana na kukubalika na mahakimu wawili na kutumia hiyo kwa kuwa mahakimu wote waliona mshitakwia alikuwa ana hatia na kuacha ya mmoja ambapo alikuwa na maamuzi ya peke yake na kutumia usemi wa wengi wape.

Hivyo Liyumba alisomewa hukumu mbili mahakamani hapo na ya kwanza iliyosomwa na Hakimu Lameck Mlacha ilisema amemfunga mshitakwia huyo kwa kuridhika na ushahidi uliotolewa na mashahidi watano upande wa mashtaka kati ya mashahidi wanane waliosikilizwa katika shauri hilo.

Alisema watano kati yao walitoa ushahidi na kuidhihirishia na waliisisitizia mahakama kuwa gharama katika Mradi wa Ten Milambo ulisababishwa na matumizi mabaya ya madaraka na kuharibu mali ya umma.

Mashahidi hao walisema kuwa mshtakiwa alikuwa akisaini na kutoa maelekezo katika mradi huo uliokuwa chini ya uongozi wa idara aliyokuwa akiiongoza mshitakiwa.

Hakimu Mlacha alisema kuwa mahakama imebaini kuwa mshtakiwa alikuwa akitoa maelekezo kinyume na utaratibu wa BOT kiasi cha kuwa na nguvu ya kubadili uhalisia wa mradi..

Baada ya hukumu hiyo wakili aliyekuwa akimtetea mshtakiwa Bw. Majura Magafu aliiomba mahakama hiyo kuwa na huruma na mshitakiwa japo ameonekana kupatikana na hatia kwa kuwa mshitakiwa alikuwa ni mtumishi wa serikali na ameitumikia BoT kwa uadilifu na kwa muda mrefu kwa miaka 35.

Katika maombi hayo pia aliiomba mahakama hiyo kuangalia umri wa mshitakiwa apunguziwe adhabu kwa kuwa anategemewa na familia yake na atayari alishakuwa mstaafu.

Awali Mwendesha Mashtaka Wakili wa Serikali, Bw. Prosper Mwangamila alidai mbele ya mahakama hiyo kuwa Amatus Liyumba, alitenda makosa hayo kati ya mwaka 2001 na 2006 akiwa mtumishi wa Benki Kuu ya Tanzania [BoT] alitumia vibaya madaraka ya ofisi yake katika ujenzi wa majengo pacha ya benki hiyo na kuisababishia hasara serikali y a shilingi bilioni 221.

Ndugu, jamaa na marafiki walianza kuangaua kilio mahakamani hapo bada ya kutolewa hukumu hiyo na ndugu yao kulalamika kuwa hukumu hiyo haikua sahihi na kudai ushahdi uliotolewa haukuchambuliwa ipasavyo.

Liyumba aliweza kusotatu rumande kwa zaidi ya mwaka mmoja na miezi mitatu baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana yaliyomtaka kutoa Sh bilioni 110.

Hivyo Liyumba alipandishwa kwenye gari la washitakiwa lililokuwa na namba STK 4373, majira ya saa 7.43 mchana kwenda kuanza maisha yake mapya gerezani kwa muda wa miaka miwili.

Watano wa familia moja wateketea kwa moto


WATU watano wa familia moja wamefariki dunia baada ya nyumba yao kuteketezwa kwa moto uliodaiwa kuwashwa kimakusudi kuteketeza familia hiyo huko Vijibweni Wilayani Temeke.
Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia jana majira ya usiku, huko maeneo ya Vijibweni Temeke ambapo ajali hiyo imetokana na ugomvi wa kimapenzi kutoka kwa mmoja wa wanafamilia hiyo.

Watu hao wote kwa pamoja waliweza kupoteza maisha usiku huo baada ya nyumba hiyo kuteketea kwa moto wakiwa ndani kwao katika chumba kimoja kwa pamoja.

Wanafamilia hao walioteketea kwa moto ni baba wa familia, John Onesmo (32) ambaye ni mfanyabiashara wa samaki eneo la Feri, mke Catherine John (25), watoto wao wawili ambao ni Joyce John (5) na Oliver John na Esther Amos (20) ambaye ni mdogo wa Catherine.

Moto huo uliolipuliwa majira ya saa 6 usiku, ulidaiwa kulipuliwa na mchumba wake Ester aliyetambulika kwa jina la Shemsa Mpelela (22), kutuhumiwa kuchoma moto nyumba hiyo kwa kutumia mafuta aina ya petroli

Kwa mujibu ya maelezo ya majirani usiku huo walisikia mlipuko mkali na walidhani kuwa pikipiki imepasuka tairi ama mlio wa risasi na kuamka na kuona nyumba hiyo inawaka moto.

Majirani waliweza kuamka kwa kushirikiana kutaka kuwaokoa watu hao lakini ilishindikana kwa kuwa moto ulishapamba kuzingira nyumba hiyo na juhudi zilishindikana na watu hao kumaliza maisha ndani humo

Hata hivyo zimamoto lilichelewa kufika eneo hilo kutokana na ubovu wa barabara na gari lilikwama njiani.

Askari walipofika eneo la tukio na baada ya moto huo kuzimwa walipoingia ndani tayari watu hao walishapoteza maisha na John alikutwa amekumbatia watoto wake kitandani.

Tukio hilo ambalo moja kwa moja linahusishwa na ugomvi kati ya Ester na Shemsi majirani walidai kuwa mwaka jana Esther alipomaliza darasa la saba Manyoni, Singida, alikuja kwa dada yake huyo kuishi nae.

Ilidaiwa na majirani hao kuwa Ester alianza tabia ya kuwa na mahusiano ya kimapenzi na wanaume mahali hapo hali ambayo dada yake alikuwa akigombana nae hadi ilifikia hatua dada yake huyo kumrudisha kijijni kwao kutokana na tabia zake hizo.

Ilidaiwa kuwa Ester alirudi tena jijini kwa kurudishwa na nauli aliyotumiwa na Shemsi na kwenda kuishi nae Kigamboni nyumbani kwa Shemsi na alirudi na kuja tena kwa dada yake baada ya kutokea ugomvi wa kimapenzi ambao haujafahamika chanzo chake hali iliyopelekea Shemsi kumchoma kisu Ester shingoni na tumboni.

Na dada yake kwa kushirikiana na mume wake walijaribu kumtafuta Shemsi na hawakuweza kumpata na hawakujua yuko wapi.

Na usiku wa kuamkia jana baada ya tukio hilo kutokea dumu ambalo lilikuwa na mafuta hayo lilionekana pembezoni mwa nyumba hiyo ambayo ilikuwa haijaisha na kumalizika chumba hicho na kuhamia.

Polisi Mkoani Temeke limethitisha kutokea kwa tukio hilo na tayari linafanyia kazi tukio hilo la kusikitisha.

Wednesday, May 26, 2010

Elton John asababisha utata Morocco


Mwanamuziki wa Uingereza Elton John anatarajiwa kuwepo katika tamasha nchini Morocco licha ya kuwepo wito wa kuzuiwa.

Wapiganaji wa kiislamu wamejaribu kuzuia mwaliko wake huo, wakidai kuwa mwanamuziki huyo aliyeweka wazi kuwa anafanya mapenzi ya jinsia moja anaenda kinyume na maadili ya umma.

Lakini waratibu wa tamasha la Mawazine huko Rabat wametetea uamuzi wa kumwalika John, kwa madai ya "kustahamiliana kimaadili".
Wiki iliyopita, tamasha lililopangwa kufanywa huko Misri liliahirishwa baada ya John kusema katika mahojiano ya jarida moja kuwa Yesu alikuwa anafuata mapenzi ya jinsia moja.

Mkurugenzi wa sanaa wa tamasaha la Mawazine Azizi Daki ameiambia BBC kuwa wanatarajia umati mkubwa kujitokeza kwenye oneysho lake.

Amesema, " Kawaida umati mkubwa ni takriban watu 40,000."

" Usiku wa leo tunatarajia takriban watu 60,000 kuja kumwona Elton John."

Bw Daki amesema hii ni mara ya kwanza kwa John kufanya onyesho Morocco na ana umaarufu sana nchini humo.

Amesema, " Kipaji chake kimekuwa cha kuridhisha sana, anawafanya raia wa Morocco wawe na matumaini na kila mmoja anajua nyimbo zake."

Wasanii maarufu
Lakini mapema mwezi huu, chama cha Islamist Justice and Development (PJD) lilipinga onyesho hilo la John.

Mwanachama wa PJD Mustapha Ramid amesema: " Tuliiomba serikali kutomhusisha mtu huyo katika orodha ya wasanii walioalikwa kwenye tamasaha hilo."

"Mwanamme huyu-samahani, bora niseme mtu huyu, na si mwanamme huyu- anajulikana kwa kujisifu kwa kufuata mapenzi ya jinsia moja."

Bw Ramid amesema, "Morocco ni taifa la kiislamu ambapo jukwaa halitakiwi kumruhusu mtu mwenye kiwango hicho cha ufisadi kufanya onyesho kwasababu inabidi tuwanusuru watoto na mambo kama hayo."

Tamasha la Mawazine la siku tisa huhusisha wasanii kutoka duniani kote, wakiwemo Sting, Carlos Santana, Julio Iglesias, Toumani Diabate na Alpha Blondy.

Makundi ya kiislamu yamekuwa yakikosoa tamasha hizo kwa kushinikiza ufisadi na kuharibu maadili ya kiislamu.

Mwezi Februari, John aliliambia jarida la America's Parade: " Nafikiri Yesu alikuwa mtu mwenye imani, mtu hodari sana mwenye kufuata mapenzi ya jinsia moja aliyeelewa matatizo ya mwanadamu."

Kauli hii ndio ilisababisha tamasha lake lililokuwa lifanyike Mei 18 kuzuiwa.