KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Friday, May 28, 2010

Familia Iliyoteketezwa Kwa Moto Yazikwa, Aliyeanzisha Moto Akamatwa


MTUHUMIWA Shemsa Mpelela [22] anayesadikiwa kuwa kuichoma moto nyumba na kupelekea vifo vya watu watano wa familia moja amekamatwa.
Mtuhumiwa huyo ni mlinzi wa Shule ya Sekondari Aboud Jumbe iliyopo Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Ilidaiwa kuwa kabla ya kukamatwa kwake juzi, Shemsa alikwenda kwa kaka yake eneo la Kigamboni, Kisiwani, kuomba nauli ili aondoke Dar es Salaam ndipo watu walipomwona na kutoa taarifa Polisi.

Pia marafiki wawili wa mtuhumiwa huyo walikamatwa akiwamo mwanaume anayedaiwa kushirikiana naye kuichoma moto nyumba hiyo na kusababisha vifo vya watu watano wa familia moja.

Rafiki wa mtuhumiwa aliyeenda nae eneo la tukio alisikika kijiweni akisema kuwa alimuona rafiki yake huyo akinunua lita moja moja za petroli na zilipofika lita 10 alimwomba amsindikize bila kujua adha ya rafiki yake huyo.

Aliendelea kueleza kuwa, alishangazwa kuona wamefika katika nyumba hiyo na kuona mwenzake akichoma nyumba na wakaondoka eneo la tukio haraka na kukaa mbali huku wakishuhudia nyumba hiyo inavyoteketea, ndipo wasamaria walipotoa tarifa polisi.

Jana marehemu wote walizikwa kwa pamoja katika mazishi yaliyofanyika Tungi, Kigamboni, Dar es Salaam.

Miili ya marehemu iliwasili nyumbani kwa Onesmo saa 9 alasiri na sala ya kuwaombea iliongozwa na Mchungaji wa Kanisa la Anglikana wa Tungi, Obed Ntigogozwa na baadaye majeneza yote matano yalipelekwa kuzikwa eneo la makaburi la Vijibweni.

Hata hivyo miili ya marehemu hao haikuoneshwa, kutokana na kuharibika kwa miili hiyo iliyoteketea kwa moto.

Marehemu hao walioteketea kwa moto wakiwa katika nyumba yao yenye chumba kimoja ni baba mwenye nyumba John Onesmo (32), Catherine Jackson (25), watoto wao wawili Oliver (2) na Joyce John (5) na Esther Mugulu (20) ambaye ni mdogo wa Catherine.

No comments:

Post a Comment