KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Saturday, May 29, 2010

Wanaume wapendanao waachiwa Malawi


Wanaume wawili wanaofanya mapenzi ya jinsia moja nchini Malawi waliofungwa baada ya kufanya sherehe ya uchumba wamesamehewa na Rais Bingu Wa Mutharika.

Bw Mutharika, akizungumza wakati katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa alipotembelea nchi yake, amesema ameamuru waachiliwe huru haraka iwezekanavyo.

Steven Monjeza na Tiwonge Chimbalanga walihukumiwa kifungo cha miaka 14 jela mapema mwezi huu kwa kufanya vitendo kinyume cha maumbile na vitendo vya aibu.

Kesi hiyo iliibua malalamiko kutoka nchi za kimataifa napia mjadala juu ya mapenzi ya jinsia moja ndani ya Malawi.

Bw Ban ameusifu uamuzi wa Rais kuwa ni wa "kijasiri."

Amesema, "Sheria hii iliyopitwa na wakati irekebishwe popote ilipo."

'Utamaduni wa chuki'
Waandishi wanasema Malawi ni jamii yenye msimamo mkali sana ambapo viongozi wa dini huhusisha mapenzi ya jinsia moja na ushetani.

Bw Mutharika amewaachia huru kwa misingi ya haki za binadamu.

Baada ya kukutana na Bw Ban alisema, "Wanaume hawa wawili wametenda uhalifu dhidi ya mila zetu, dini zetu na sheria zetu."

"Hata hivyo, kama mkuu wa nchi nawasamehe na hivyo waachiwe haraka iwezekanavyo bila masharti yeyote."


Steven Monjeza, 26, na Tiwonge Chimbalanga, 20, walikuwa gerezani tangu walipokamatwa Desemba 2009 baada ya kufanya sherehe ya uchumba, kabla ya mipango ya kufunga ndoa mwaka 2010.

Gift Trapence, kutoka kituo cha kutetea maendeleo ya watu, amefurahiswa na uamuzi huo.

Amesema, "Tumefurahi sana na tunamsifu Rais kwa ukomavu wake, lakini bado tuna safari ndefu kumaliza mila hizi za chuki."

Sheria za kikoloni
Mashirika ya kutoa misaada na haki za binadamu yamekuwa yakishinikiza serikali yake kuheshimu haki ya wachache.

Wanaume hawa wawili wametenda uhalifu dhidi ya mila zetu, dini zetu na sheria zetu.
Bingu Wa Mutharika, Rais wa Malawi
Serikali ya Uingereza, mfadhili mkuu wa Malawi, ilisema ilishtushwa na hukumu hiyo, na Marekani iliuelezea kama hatua moja nyuma katika harakati za kupigania haki za binadamu.

Siku ya Jumamosi, mwanamuziki wa miondoko ya Pop Sir Elton John aliandika barua ya wazi kwa Bw Mutharika kupitia gazeti la Uingereza la The Guardian akiomba waachiwe huru.

Wanaume hao wawili wamehukumiwa kwa sheria ya zamani ya kikoloni wakati Malawi ilipokuwa ikitawaliwa na Uingereza.

Makoloni mengi yaliyokuwa ya Uingereza yana sheria sawa na hiyo inayopinga mapenzi ya jinsia moja: India ilibadilisha sheria hiyo ya kuwapinga mwaka jana.

No comments:

Post a Comment