Shirika la kutoa misaada ya afya, Medecins Sans Frontieres, limeonya kwamba ikiwa jamii ya kimataifa itapunguza misaada, basi kuna hatari ya mamilioni ya watu kuambukizwa ukimwi na HIV, na kuhatarisha kampeni dhidi ya ugonjwa huo.
Shirika hilo limefanya utafiti katika mataifa manane ya Afrika, na kuelezea kwamba kupunguzwa kwa misaada hiyo ni jambo ambalo limeanza kuziathiri nchi hizo.
MSF imeelezea kwamba hazina ya dunia ya Global Fund tayari imepunguza misaada kwa asilimia nane hadi kumi na mbili.
Shirika hilo limefafanua kwamba hata serikali ya Marekani, kupitia mpango wake wa kutoa misaada ya dharura unaosimamiwa na rais, President's Emergency Plan for AIDS (PEPFAR), pia umepunguza msaada wake kwa nchi wahitaji.
Benki ya dunia, Umoja wa Ulaya na mpango wa rais wa zamani wa Marekani, Clinton Health Initiative, ni baadhi ya mashirika zaidi yaliyopunguza misaada.
No comments:
Post a Comment