KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Friday, May 28, 2010

Fran Merida ahama Arsenal aenda Atletico

Kiungo wa Arsenal Fran Merida anarejea Hispania ambako atajiunga na klabu ya Atletico Madrid akiwa mchezaji huru.
Merida mwenye umri wa miaka 20, amejiunga na Atletico Madrid kwa mkataba wa miaka minne, alijiunga na Arsenal tangu mwaka 2006 akitokea Barcelona.

Lakini ameshindwa kujitutuma katika timu ya kwanza na msimu uliopita alitumiwa akiwa mchezaji wa akiba katika michezo minne ya ligi.

Alifunga bao dhidi ya Bolton katika mchezo wa ligi na alianza tangu mwanzo katika michezo minne ya kuwania kombe la Carling na FA Cups na pia Ligi ya Ulaya.

Merida pia alifunga bao muhimu wakati Arsenal walipoifunga Liverpool mabao 2-1 mwezi wa Oktoba katika mechi ya mchakato wa Kombe la Carling.

Mchezaji huyo raia wa Hispania, ambaye mkataba wake na Arsenal unamalizika tarehe 30 mwezi wa Juni, anatazamiwa kutambulishwa kwa mabingwa hao wa Ligi ya Europa siku ya Ijumaa katika uwanja wa Vicente Calderon.

Atletico pia imethibitisha kwamba Quique Sanchez Flores amesaini mkataba mpya wa kuifundisha klabu hiyo kwa msimu mmoja zaidi.

Flores, ambaye awali alizifundisha Valencia na Getafe pamoja na Benfica ya Ureno, alichukua nafasi ya Abel Resino mwezi wa Oktoba mwaka 2009.

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 45 aliiwezesha Atletico kushinda Ligi ya Europa katika mchezo wa fainali walipoilaza Fulham mabao 2-1, ikiwa ni mara yao ya kwanza kushinda taji kubwa tangu mwaka 1996 ingawa katika fainali ya Kombe la Hispania walipoteza kwa kufungwa mabao 2-0 na Sevilla.

No comments:

Post a Comment