KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Amazon MP3 Clips

Saturday, May 29, 2010

Walinda amani 2000 kuondolewa Congo


Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepiga kura ya kuruhusu kuondolewa kwa kiasi cha wanajeshi wake 2000 wanaolinda amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Hata hivyo, baraza hilo limeahirisha uamuzi kuhusu kuondolewa kikamilifu kwa kikosi chake chenye wanajeshi 20, 500, hadi mwaka ujao,kama alivyoagiza Rais wa Congo, Joseph Kabila.

Wajumbe wote 15 wa baraza kwa kauli moja walipitisha azimio la kuwaondoa wanajeshi hao "haswa katika maeneo ambayo hali ya usalama inaruhusu".

Umoja wa Mataifa pia uliamua operesheni zake za kawaida kuendelea nchini Congo hadi mwezi June mwaka wa 2011.

Kikosi cha Umoja wa Mataifa nchini Congo ambacho hujulikana kama MONUC, kuanzia mwezi July kitafahamika kama (UN Organisation Stabilisation Mission in DR Congo) MONUSCO.

Azimio hilo linaruhusu MONUSCO kuwa na wanajeshi 19,815, waangalizi wa kijeshi wapatao 760, na polisi mchanganyiko wapatao 1400.

Unyanyasaji wa kimapenzi

Wanajeshi wa Umoja wa Mataifa wamekuwa na rekodi yenye utata katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, pamoja na madai ya kuhusika na dhulma za kimapenzi, usafirishaji wa dhahabu kimagendo na kuwatoroka waasi wakati wa mapigano.

Askari wa kulinda amani waliwasili katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo mwaka wa 1999, wakati huo wakianza kushughulikia mapigano ya wenyewe kwa wenyewe nchini kote.


Tangu kumalizika kwa mapigano mwaka wa 2003, wamekuwa wakipambana na wanamgambo wa makundi mbali mbali, ambao wamekuwa wakiiba madini yenye thamani kubwa mashariki mwa nchi.

Wengi wa wanamgambo hao sasa aidha wamenyanganywa silaha, au kujumuishwa katika jeshi la Congo, huku wengine wakibakia kama majangili wenye silaha.

Rais Kabila anaamini kuwa jeshi lake la taifa lina uwezo wa kushughulikia matatizo yaliyobaki na amesema anataka wanajeshi wa Umoja wa Mataifa wawe wameondoka nchini humo mwishoni mwa mwaka wa 2011.

Hata hivyo, baadhi ya wadadisi wanaamini kuwa eneo hilo baado halina usalama, na halitoweza kuhimili athari za kuondoka kwa wanajeshi hao wa kulinda amani.

Unyanyasaji wa kimapenzi ni shida ya kipekee, ambapo zaidi ya wanawake 8,000 walibakwa wakati wa mapigano, mwaka wa 2009, kulingana na repoti ya Umoja wa Mataifa.

Hali hiyo ilisababisha kikosi cha MONUC kuwasindikiza wanawake wanapokwenda sokoni.

Umoja wa Mataifa umeamua kuwa mustakbala wa wanajeshi wake utaamuliwa kutokana na mafanikio yatakayopatikana mashariki mwa nchi na uwezo wa serikali ya Congo wa kuwalinda raia wake, pamoja kudhibiti nchi nzima.

"Hatua ya kuwalinda raia lazima ipewe umuhimu" Umoja wa Mataifa ilisema katika azimio lake, na kuongeza kuwa iliwaruhusu walinda amani wake kutumia "nguvu zao zote" kutekeleza azimio hilo.

No comments:

Post a Comment