KARIBU MAISHANI
KARIBU MAISHANI
Wednesday, January 12, 2011
Wanaharakati waapa kuzuia Serikali kuilipa Dowans
KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kwa kushirikiana na wanaharakati wa haki za kijinsia nchini wamewasilisha pingamizi Mahakama Kuu kupinga Serikali isiilipe kampuni ya Dowans Sh 97 bilioni zilizotokana na hukumu ya Mahakama ya Usuluhishi ya Biashara ya Kimataifa (ICC).
Mahakama hiyo ilikuwa imesikiliza malalamiko ya Dowans dhidi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na kuamua iilipe fidia hiyo baada ya kubaini kuwa ilivunja mkataba kinyume cha taratibu.
Kwa kawaida kabla ya malipo hayo kufanyika, hukumu hiyo ya ICC inapaswa kusajiliwa na Mahakama Kuu ya Tanzania, lakini wanaharakati hao wamekusudia kuweka pingamizi kuzuia mchakato huo usifanyike hivyo Dowans isilipwe.
LHRC jana walitoa tamko hilo wakisisitiza kuwa wanaungwa mkono na vyama mbalimbali visivyo vya kiserikali yakiwemo mashirika yanayotetea haki za binadamu, usawa wa jinsia na ukombozi wa wanawake (FemAct).
Akisoma tamko kuhusu uamuzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Francis Kiwanga alisema wameamua kuwake pingamizi kutokana na mikataba ya awali ya kampuni ya Dowans kupatikana kwa rushwa na kukiuka maslahi ya umma.
“Kituo kinafungua shauri Mahakama Kuu kupinga uhalali wa tuzo iliyotolewa kwa Dowans isisajiliwe na kuwa tuzo ya kimataifa kwasababu mikataba ya awali ilipatikana kwa rushwa na kukiuka maslahi ya umma,” alisema Kiwanga.
Kiwanga alimtataja Wakili wa Kujitegemea na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Bagamoyo, Dk Sengondo Mvungi kuwa ndiye wakili aliyeteuliwa kulisimia shauri hilo.
Katika mkutano huo na waandishi wa habari, Kiwanga alisema katika suala la Dowans kuna maswali mengi ya kujiuliza.
“Ikiwa Bunge la Jamuhuri ya Muungano kupitia Kamati Teule ya Bunge iliyoundwa Novemba 13 mwaka 2007 ilishathibitisha kuwa Richmond ni kampuni hewa, inawezekanaje kuwa na mkataba wa kurithisha Dowans?” alihoji Kiwanga.
Kiwanga alisema Wizara ya Nishati na Madini inatia shaka kuhusu mwenendo wa suala zima la Dowans na kuitaka Tanesco kukataa kulipa deni hilo.
“Uhalali wa kisheria wa miliki ya Dowans kwa mali za Richmond haupo. Ni kwanini Serikali haikutaifisha mali za Richmond tangu awali? Pili ikiwa Dowans haikurithi kwa halali mali ya Richmond, inawezekanaje Dowans kuwa na madai halali dhidi ya Serikali ya Tanzania?” alihoji Kiwanga.
Kiwanga alielezea shaka kwa Serikali kuwa na uharaka wa kulilipa deni hilo bila hata ya kuchukua hatua zozote za kisheria.
Alihoji, "Nini hasa maslahi ya Wizara ya Nishati na Madini hasa ikizingatiwa ndio iliyoishinikiza Tanesco kukubali kuhusishwa na kuhamishwa kwa mkataba wa Richmond kwenda Dowans?"
Alisema suala la usiri wa mikataba ya Serikali na uwekezaji hasa katika sekta ya nishati na madini linaibua maswali mengi na kuhoji dhana nzima ya uwajibikaji na uhifadhi wa rasilimali ya umma.
Alisema kutokana na hali hiyo, LHRC imependekeza mambo makuu sita likiwamo la kuitaka Serikali, watawala na maofisa wa umma na wote wanaohusika na suala hilo kuheshimu uamuzi ya Bunge wa kwamba Richmond ni kampuni hewa.
Alisema katika mazingira hayo kuilipa Dowans fedha hizo ni ukiukwaji wa utawala wa sheria na misingi ya demokrasia na ni kinyume na maslahi ya Taifa.
Aliitaka Wizara ya Nishati na Madini kuacha mara moja kuwabebesha mzigo Watanzania wa kulipa kiwango hicho kikubwa cha fedha wakati huo ni uzembe, ubadhilifu na ufisadi unaotokana na watendaji wa Serikali.
“Serikali na watawala pamoja na maofisa wa umma wote wanaohusika na suala hilo wazingatie maelekezo ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 9(c), (d), (h) na (i) ambavyo vinasisitiza mali ya umma iwanufaishe wananchi wote,” alisema Kiwanga.
Kiwanga alisema kituo kinapinga malipo hiyo kwakuwa hata Serikali iliweka siri katika kuendesha kesi hiyo jambo linalotia shaka hata utetezi wake kama ulizingatia masilahi ya umma.
Naye Dk Mvungi ambaye ndiye wakili aliyeteuliwa kusimamia shauri hilo, alisema kitendo cha Serikali kukubali kulipa deni la Dowans ni ufisadi mwingine na kuwataka Watanzania kuamka kupinga hilo.
Naye Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Ananilea Nkya alisema suala la Dowans ni ufisadi na usanii wanaofanyiwa Watanzania na kutaka waamke ili kupinga suala hilo kwa nguvu.
Aliomba vyombo vya habari kulichukulia suala hilo kwa uzito unaostahili kwa kuwa jamii ikishirikiana katika kuweka nguvu kuzuia fedha za umma kwenda kwa wachache kifisadi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Usu Mallya alisema kitendo cha watu kuwaingiza Watanzania kwenye mikataba feki bila ya kuchukuliwa hatua, kinatia shaka hata katika mkataba huo.
“Waliotushauri kujitoa kwenye mikataba hiyo mibovu leo ndio wanatushinikiza kulipa deni hilo. Hii inatia mashaka, ni vema kundi la watu waliotuingiza kwenye hasara hiyo toka mwanzo, tukawafahamu na wachukuliwe hatua za kisheria,” alisema Mallya
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment