KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Amazon MP3 Clips

Wednesday, January 12, 2011

Kura za Sudan kusini zafikia 60%


Wapiga kura ya maoni Sudan kusini Januari 9, 2011


Chama tawala cha kusini na kundi lililokuwa la waasi limesema Sudan kusini imefikia asilimia 60 ya wapiga kura waliotakiwa ili kupitisha kura ya maoni ya kuweza kujitenga na kaskazini.

Anne Itto wa SPLM alisema, " Kiwango cha asilimia 60 kimefikiwa lakini tunaomba idadi ya wapiga kura ifikie asilimia 100."

Hakutoa idadi kamili, lakini alisema kiwango hicho kimetokana na ripoti kutoka vituo vya kupigia kura katika siku ya tatu ya kura itakayochukua wiki nzima na iliyoanza siku ya Jumapili.

Kura hiyo iliafikiwa kama sehemu ya makubaliano ya mwaka 2005 ya kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miongo miwili.

Chama cha Sudan People's Liberation Movement kimekuwa kikiongoza eneo hilo tangu makubaliano hayo ya amani kuafikiwa.

Takwimu rasmi za watu waliojitokeza kupiga kura hiyo, pamoja na matokeo ya awali yanatarajiwa kutolewa mwanzoni mwa mwezi Februari, na tume ya kura ya maoni ya Sudan kusini.

Takriban watu milioni nne wamejiandikisha kupiga kura hiyo.

Shirika la habari la AP limeripoti kuwa Bi Itto alisema watu wameacha kuulizana "vipi hali yako?" kama salaam na badala yake wanaulizana "umepiga kura?".

Kura hiyo, ambapo upande wa kusini tu ndio unashiriki, unatarajiwa sana kukubaliana na kujitenga.

Wakati huo huo wizara ya mambo ya nje ya Marekani imeashiria kwamba inaweza kuiondosha Sudan katika orodha yake ya mataifa yanayofadhili ugaidi iwapo kaskazini itatambua matokeo ya kura hizo.

Iwapo kura hiyo ya maoni itapitishwa Sudan kusini itakuwa taifa la 54 la Afrika tarehe 9 Julai 2011.

Kaskazini na kusini wamekuwa katika mapigano kwa miongo kadhaa kutokana na tofauti za kidini na kikabila, huku kukikadiriwa takriban watu milioni 1.5 wameuawa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.

No comments:

Post a Comment