Hosni Mubarak
Katika tangazo kupitia televisheni ya taifa, makamu wa rais Omar Suleiman amesema Bw Mubarak amekabidhi madaraka kwa jeshi.
Hatua hii imekuja baada ya maelfu ya watu kukusanyika mjini Cairo pamoja na miji mingine mikuu katika siku ya 18 ya maandamano ya kudai Bw Mubarak ajiuzulu.
Waandamanaji walipokea taarifa hizo kwa kushangilia, kupeperusha bendera, kukumbatiana na kupiga honi za magari. "Watu wameuangusha utawala," wamekuwa wakiimba.
Mubarak na Omar Suleiman
"Kwa jina na Mungu mwenye neema, mwenye rehema, raia, katika wakati huu mgumu, Misri inapopitia, Rais Hosni Mubarak ameamua kuachia madaraka kutoka ofisi ya rais ya jamhuri na ametoa jukumu la kuendesha nchi kwa baraza kuu la jeshi," amesema.
"Mungu awasaidie wote," amesema Omar Suleiman.
Bw Mubarak tayari ameondoka Cairo na yupo katika mji wa Sharm el-Sheikh, ambapo ana makazi mengine huko, maafisa wamesema.
Mjini Cairo, maelfu ya watu wamekusanyika nje ya Ikulu, katika eneo la wazi la Tahrir na katika kituo cha taifa cha televisheni.
Waandamanaji hao walikuwa na hasira kufuatia hotuba ya Bw Mubarak siku ya Alhamisi. Alikuwa akitarajiwa kutangaza kujizulu, lakini hakufanya hivyo na badala yake kupunguza madaraka yake kwa makamu wa rais.
Polisi amshitaki Winnie Mandela
Winnie Mandela
Afisa mmoja wa polisi nchini Afrika Kusini amefungua mashitaka dhidi ya mke wa zamani wa rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela.
Chama cha wafanyakazi cha polisi huyo kimesema hatua hiyo imefikiwa baada ya polisi kumtuhumu Winnie Madikizela-Mandela kwa kuendesha gari kwa kasi.
Chama hicho, Solidarity kimemtuhumu Winnie kwa kujaribu kumtisha polisi huyo Jannie Odendaal.
Anatuhumiwa kwa kuvunja sheria, kujeruhi na kuendesha gari kwa uzembe.
Bw Ondendaal pamoja na askari mwenzake walikuwa tayari wamehamishiwa katika nafasi nyingine.
Dereva wa Winnie na mlinzi wake binafsi wamewasilisha malalamiko yao ya kutishwa na kuelekeza bunduki dhidi ya wawili hao.
Uchunguzi umeanza kuhusu mwenendo wao.
Kasi
Solidarity imesema Bw Odendaal alikuwa akitekeleza wajibu wake.
"Madikizela-Mandela na walinzi wake ndio walitakiwa wachunguzwe kwa mienendo yao," amesema Dirk Hermann, katibu mkuu wa chama cha Solidarity, katika taarifa aliyotoa.
Bi Madikizela hajasema lolote kuhusiana na sakata hilo.
Bw Odendaal, ambaye alisimamisha gari la Madikizela-Mandela mwezi Disemba, amesema alikuwa akiendesha gari kwa kasi ya kilomita 150 kwa saa, ambayo ni kilomita 30 zaidi ya kasi inayoruhusiwa
Mapigano Sudan yasababisha 'vifo 100'
George Athol
Zaidi ya watu 100 wanasemakana sasa kufariki dunia katika mapigano Sudan kusini baada ya waasi kushambulia jeshi.
Ripoti za awali zilisema mapigano ya wiki hii yamesababisha vifo vya watu 16.
Msemaji wa jeshi la Sudan Kusini alisema, takriban watu 39 miongoni mwa waliouawa ni raia.
Mapigano baina ya wapiganaji wanaomtii George Athor na jeshi la Sudan kusini yameanza huku eneo hilo likijiandaa kwa uhuru kutoka kaskazini kufuatia kura ya maoni iliyofanyika mwezi uliopita.
Kulingana na matokeo rasmi yaliyotangazwa na maafisa wiki hii, takriban watu asilimia 99 wamepiga kura ya kujitenga kutoka kaskazini.
Bw Athor aliamua kuanzisha mapigano mwaka jana, akidai kuwepo na udanganyifu katika uchaguzi, lakini alitia saini mwezi uliopita ya kusitisha mapigano kabla ya kura hiyo ya kihistoria.
Changamoto za kiusalama
Msemaji wa jeshi la Sudan kusini Philip Aguer alisema, wanachama 20 wa majeshi ya usalama ya Sudan kusini waliuawa, pamoja na waasi 30, na kufanya jumla ya waliouawa kufikia 105.
Wakati wa mapigano hayo, magari mawili ya jeshi yalilipuliwa na mabomu ya kutegwa ardhini karibu na mji wa Fangak katika jimbo la Jonglei.
Alisema, wafuasi wa Bw Athor walifanya shambulio hilo siku ya Jumatano na mapigano yaliendelea mpaka Alhamis.
Jonglei ni mji maarufu sana upande wa kusini.
Wakati Bw Athor akiamua kuchukua silaha, upande wa kusini ulimtuhumu kwa kutumiwa na upande wa kaskazini ili kuchochea ghasia na kuharibu kura ya maoni, tuhuma ambazo maafisa wa upande wa kaskazini unazikana
Ushauri wa Jinsi ya Kulima Bangi
Mwanaume mmoja wa nchini Marekani amekuwa mkulima wa bangi mwenye mafanikio ziro baada ya kupiga simu polisi akiwafahamisha kuwa ameanza kulima bangi akitaka kujua adhabu zitolewazo kwa kulima angalau mmea mmoja wa bangi.
Robert Michelson, 21, alipiga simu polisi na kuwauliza adhabu ambayo anaweza kupewa iwapo atakamatwa akilima mmea mmoja wa bangi.
Polisi kwa kutumia namba ya simu aliyoitumia, waliweza kuigundua nyumba yake ambapo msako wa polisi ulifanikiwa kugundua mimea michache ya bangi.
Michelson alitiwa mbaroni kwa kumiliki mimea hiyo kinyume cha sheria na aliachiwa huru kwa dhamana ya dola 500
No comments:
Post a Comment