KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Wednesday, January 12, 2011

Pinda aenda UDOM kuokoa jahazi


LICHA ya kuwepo kwa taarifa kwamba Waziri Mkuu, Mizengo Pinda atakutana na wadhahiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma, wahadhiri hao wameendelea kuchachamaa wakisisitiza kwamba subira yao imefikia ukingoni sasa wanajiandaa kwenda mahakamani kutafuta haki yao.


Wahadhiri wa chuo hicho wamekuwa katika mgomo kuingia madarasani kufundisha kwa kile wanachodai kuwa wanadhulumiwa viwango vya mishahara wanavyolipwa na serikali.

Akizungumza na Mwananchi, Naibu Katibu mkuu wa chama cha wahadhiri hao (Udomosa),
Peter Kokeli alisema juhudi zao kubwa wamezielekeza katika kuhakikisha wanapata haki zao.Kokeli alisema wamekuwa na mategemea kuwa Rais Jakaya Kikwete atalitatua suala hilo lakini tayari wameanza hatua za kwenda mahakamamani.

Licha ya kuahidi kwamba wako tayari kuzungumza na Pinda, alisema suala hilo ni kosa la jinai kwa sababu wamegunduia kwamba kumekuwa na tabia ya kughushi slipu zao za mishahara.“Wahadhiri wamesikitishwa sana na taarifa hizi za uongo.

Tunapenda kuweka wazi kuwa mishahara mipya iliyoletwa chuoni ni sawa na ngazi ya mishahara iliyolipwa pia kwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Kwa mfano Tutorial Assistant (PUTS 12), kwenye vyuo vyote viwili imekuwa Tsh 1,248,070/=, lakini menejimenti ya UDOM imekata mishahara hiyo.

"Wahadhiri wamebaini nyaraka za ndani ya chuo Kikuu cha Dodoma zikionyesha kuwa mishahara mipya imeletwa na kimsingi hazina makosa yoyote kwa wanataaluma,” alisema Kokeli.

Alieleza pia kusikitishwa na kauli ya Makamu mkuu wa chuo hicho Profesa Idrisa Kikula, aliposema kuwa wahadhiri wamekosa uelewa na madai yao si ya msingi, akisema kuwa kauli hiyo imelenga kuwadhalilisha, hivyo wamemtaka aiombe radhi jumuiya hii ya wanataaluma wa UDOM.

“Tunapenda kuweka wazi kuwa madai yetu ni ya msingi sana na pia ni stahiki za msingi na za kisheria. Makamu Mkuu wa Chuo ajibu hoja na si kueneza propaganda zisizo na msingi wowote” alisema KokeliLakini kwa upande wake, Profesa Kikula alisisitiza kuwa taarifa zake ni za kweli na kwamba Waziri Mkuu, Mizengo Pinda atakwenda chuoni hapo leo ili kutoa maelezo kamili ya madai hayo. “Kesho (leo) Waziri mkuu atakuja hapa chuoni kueleza mambo yote wanayolalamikia.

Lakini pia kuna mkaguzi wa serikali anayefanya ‘special auditing’ (ukaguzi maalum) kuanzia wizarani, atakuja hapa Jumatatu kutoa maelezo yake. Ukweli wote utajulikana,” alisema Profesa Kikula. Akizungumzia hatua ya wahadhiri hao kufungua kesi mahakamani, Profesa Kikula alionyesha kutokutishwa na hatua hiyo.

“Mahakama zipo waache waende tu. Jana nimetoa matangazo ya ujio wa Waziri Mkuu. Nimetoa pia tangazo la mkaguzi wa hesabu za serikali. Sasa kama wao wanakwenda mahakamani, mimi siwezi kuwazuia.

Taarifa zote tunazo, mimi sizungumzi tu, natumia takwimu” alisisitiza Profesa Kikula. Taarifa zilizolifikia gazeti hili jana zilieleza kwamba Pinda akiwasili leo anatarajia kukutana na wahadhiri hao na kutoa msimamo wa serikali.Akizungumza kwa niaba ya Wahadhri hao, Peter Kokeli ambaye ni kaimu katibu wa umoja huo alisema kuwa moja ya mambo ambayo wangependa Waziri Mkuu afahamu maelezo ya ufasaha kuhusu madai yao.

Alisema kuwa wako tayari kupokea maelekezo yoyote kuhusiana na kazi yao kutoka kwa Pinda kwa kuwa wanamtambua kuwa ni kiongozi wao tena mwenye heshima lakini si katika suala la kudanganywa kuhusu malipo.
Ujio wa Waziri MKuu unaweza kuwa neema kwa wanafunzi ambao wamekuwa wakimhitaji kwa muda mrefu lakini kwa upande wa wahadhiri itakuwa bado ni kilio kwani wao wanamhitaji rais mwenyewe.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Profesa Kikula, Pinda pamoja na mambo mengine anatarajia kuzungumza na wanafunzi wa UDOM pia pamoja na kukagua miradi ya chuoni hapo ikiwemo majengo pamoja na mifumo ya maji.

Kokeli alisema kuwa Wahadhiri wana mashaka kuwa suala lao ni kama moja ya vitu ambavyo Waziri Mkuu atakuwa akivijadili lakini halitiliwi uzito mkubwa kutokana na ukweli kuwa hata katika mlolongo wa mambo ya kufanya liko katika ajenda ya nne.

“Unaweza kuona ni namna gani kuwa Waziri Mkuu hakupanga kuzungumza na sisi kwani hata katika ajenda sisi tumewekwa nafasi ya nne ni kama yaliyomo, lakini tumekubaliana kwa pamoja kuwa lazima tutakutana na kiongozi wetu huenda akawa na maagizo kutoka ngazi ya juu yake lakini tutapenda atuambie lini tunalipwa pesa zetu na si vinginevyo” alisema Kokeli.

Kiongozi huyo alisema katika maombi na malengo yao wanatarajia kumuona Rais Jakaya Kikwete akiingia katika viwanja hivyo na kukaa meza moja na wahadhiri hao ili kilio chao kiweze kufika mahali panapotakiwa na kwamba uwepo wa Pinda inawezekana ukawa ni kwa ajili ya wanafunzi.

Katibu huyo alisema wamekubaliana kuiburuza menejimenti ya Chuo mahakamani kama wataona haki yao haiipatikani na wanaiomba serikali ikubali kumtuma mkaguzi na mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali CAG Ili afanye ukaguzi wa mali za Udom ikiwemo masuala ya fedha.

Katika kipindi kisichozidi mwezi mmoja kumekuwa na mfululizo wa migomo na maandamano ya wanachuo wa Chuo hicho wakishinikiza kuonana na Waziri Mkuu huku wahadhiri wao walioanza mgomo mwanzoni mwa wiki wakitaka kuonana na Mkuu wa nchi.

Dai kubwa la walimu hao ni kupunjwa kwa mishahara yao kunakofanywa na uongozi wa Udom kwa kile walichokiita kuwa ni uchakachuaji mkubwa ndani ya menejimenti ya utawala na fedha chuoni hapo.

Wahadhiri hao walisema kuwa hawana shida na Hazina kwani mishahara yao inaonyesha kuwa imekuwa ikitumwa vizuri lakini tatizo lipo ndani ya uongozi wa chuo wenyewe ambao wanashindwa kulipa mishahara kama ilivyotumwa na Hazina.

Tatizo lingine ni pamoja na kutolipwa kwa fedha za kujikimu tangu walipoajiliwa ambao wengine wanazaidi ya miaka mitatu lakini hawajui ni lini watalipwa fedha za kujikimu kama wahadhiri wa vyuo vingine.Mwisho

No comments:

Post a Comment