KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Amazon MP3 Clips

Saturday, January 29, 2011

'Noti Mpya Hazina Ubovu ni Imara Sana' - Gavana


Noti mpya zilizotolewa na benki kuu ya Tanzania mwezi uliopita, hazina ubovu wowote na ni imara tofauti na uvumi uliozagaa mitaani, Gavana wa benki kuu ya Tanzania, Benno Ndulu amewatoa wasiwasi Watanzania.
Benki Kuu ya Tanzania Mwezi Januari 2011 ilitoa toleo jipya la noti za Shilingi 500, 1000, 2000, 5,000 na 10,000.

Baada ya kipindi cha takriban mwezi mmoja sasa, pamejitokeza dukuduku na maswali mbalimbali kutoka kwa wananchi.

Kwa kuwa ni maswali ambayo yakijibiwa yatasaidia kuelimisha jamii katika ufahamu wa noti hizi tumeona ni vyema tukayajibu kupitia kwenu alisema Gavana Benno kwa waandishi wa habari .

Maswali yaliyopokelewa au kuandikwa katika vyombo vya habari yameonekana kutaka kutoa uelewa zaidi katika maeneo yafuatayo:

2.1 Noti mpya zikisuguliwa kwenye karatasi nyeupe zinaacha rangi na kwamba zikilowa zinatoa rangi. Je hali hii haitokani na uduni wa noti hizi mpya?

Hali ya kuacha rangi noti zinaposuguliwa kwenye karatasi nyeupe ni ya kawaida kwa noti zote zilizochapishwa kwa teknolojia maalum inayojulikana kwa kitaalamu kama “Intaglio Printing”. Aina hii ya uchapishaji (Intaglio Printing) inazifanya noti kuwa na hali ya mparuzo zinapopapaswa. Teknolojia hiyo imetumika ili kuimarisha kingo za noti kwa lengo la kupunguza uwezekano wa kuchanika na kuchakaa haraka. Miparuzo hii huacha rangi noti inaposuguliwa kwa nguvu kwenye karatasi nyeupe kitendo ambacho kinathibitisha kuwa noti hiyo ni halali. Hali hii pia ni moja alama ya usalama (security feature) inayothibitisha kuwa noti siyo ya bandia.

Aidha, noti halali hazichuji zikilowekwa kwenye maji kama inavyodaiwa kwa kuwa wino uliotumika hauyeyuki katika maji.

Vilevile noti hizi zimetengenezwa kwa teknolojia ya kuwekewa kinga dhidi ya uchafu inayojulikana kitaalamu kama “Anti Soiling Treatment” ili kupunguza uwezekano wa kunasa uchafu inapokuwa katika mzunguko.
Teknolojia hizi mbili zinalenga kuongeza uhai wa noti katika mzunguko.

2.2 Je noti za zamani bado ni halali na zinaendelea kutumika?

Noti za zamani bado ni noti halali na zitaendelea kuwa katika mzunguko pamoja na zile mpya mpaka zitakapotoweka kwenye mzunguko kwa sababu za uchakavu wake. Kwa hiyo wananchi wanashauriwa kuendelea kutumia noti za toleo la zamani bila wasiwasi wowote.

2.3 Kwa kuwa noti mpya ni ndogo kuliko za zamani kwa umbo je thamani ya noti hizo siyo pungufu kulizo zile za toleo lililotangulia?

Thamani ya noti ni ile iliyoonyeshwa kwa tarakimu zilizoandikwa kwenye noti yenyewe bila kujali ukubwa wake. Kwa hiyo thamani ya noti za zamani na za sasa haitofautiani.

2.4 Kwa kuwa kumekuwa na matatizo ya upatikanaji wa noti mpya, je Benki Kuu ina mipango gani kuhakikisha noti mpya zinapatikana nchi nzima?

Benki Kuu huingiza noti mpya katika mzunguko kwa kupitia benki za biashara. Benki Kuu inaendelea kutoa noti hizo mpya kupitia benki hizo lakini kwa kuwa mtandao wa baadhi ya matawi ya benki hizo ni mpana imechukua muda mrefu kwa baadhi ya maeneo kufikiwa na noti hizo.

Hata hivyo kwa kuwa biashara nchini haina mipaka, noti hizo zitaendelea kusambaa nchini kote kupitia mzunguko wa kibiashara na kuongezeka siku baada ya siku.

2.5 Je noti halali zinatofauti gani na noti bandia?

Ili kuhakiki uhalali wa noti tunawashauri wananchi kuzichunguza kwa makini noti kwa kutumia alama za usalama kama zilivyoainishwa kwenye matangazo na vipeperushi vilivyotolewa na Benki Kuu ama kuwasiliana na ofisi zetu kwa ufafanuzi zaidi pale mtu anapokuwa na mashaka na noti hizi

No comments:

Post a Comment