KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Saturday, January 29, 2011

Mzozo Misri huenda mazungumzo yakaamua


Baada ya siku kumi na moja za maandamano makubwa ya kumtaka Rais Mohamed Hosni Mubarak kuondoka madarakani, kuna dalili serikali ya Misri na upinzani huenda wakaanzisha mazungumzo ya hatua za kukabidhi madaraka.


Hali nchini Misri


Waziri wa fedha, Samir Radwan, ameiambia BBC kuwa Makamu wa Rais, Omar Suleiman, alitarajiwa kufanya majadiliano na viongozi wa upinzani.

Kikundi kikubwa cha upinzani nchini Misri, Muslim Brotherhood, kilisema kiko tayari kushiriki katika mazungumzo hayo na serikali iwapo kwa kufanya hivyo matakwa ya watu yatajibiwa katika kipindi maalum kinachofahamika.

Kikundi hicho hakijatoa maelezo zaidi.

Makundi mengine madogo madogo tayari yameshakubali kufanya mazungumzo na Bw Suleiman.

Wakati hayo yakiendelea maelfu ya watu bado wamekusanyika katika viwanja vya Tahrir katikati ya mji mkuu wa Misri, Cairo, baada ya maandamano makubwa ya kupinga serikali, lakini mwandishi wa BBC anasema idadi ya waandamanaji inapungua.

Amesema serikali inaonekana kutokuwa na nia ya kukubali matakwa ya waandamanaji na wasiwasi unazidi kuongezeka miongoni mwa harakati za waandamanaji kuhusu malengo wanayoweza kufukia.

Mwandishi wa BBC ameongeza kueleza, watu wengi wana wasiwasi kuhusu kupata hasara ya mapato yao.

Benki nchini Misri zinatarajiwa kufunguliwa tena siku ya Jumapili na masoko ya hisa ya mjini Cairo yataanza kazi Jumatatu.

Pia kumeelezwa mlipuko umetokea kwenye bomba la kusafarisha gesi la Misri kaskazini mwa Sinai karibu na mpaka wa Israel.

Mlipuko huo ulisababisha moto mkubwa karibu na mji wa El Arish nchini Misri.

Chanzo cha mlipuko huo hakijulikani. Lakini Gavana wa jimbo hilo Abdel Wahab Mabruk, alisema anashuku bomba hilo limehujumiwa, lakini hakutoa ufafanuzi.

Bomba hilo linapeleka gesi kwa nchi za Israel na Jordan na taarifa za hivi karibuni zinasema usambaji wa gesi umesitishwa.

No comments:

Post a Comment