KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Wednesday, January 12, 2011

Madai ya Ubaguzi na Uzawa ndani ya TAZARA


HALI ya mambo ndani ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) imeenekana bado haijatengemaa baada ya kuzuka kwa madai mengine ya kufanyika kwa ubaguzi na uzawa baina ya wafanyakazi wa mamlaka hiyo.
Mambo si shwari TAZARA kufuatia hatua ya wafanyakazi wazalendo kutaka mmoja wa Mkurugenzi raia wa Zambia, Devison Mulenga kuachia ngazi kwa kile walichodai kuwa anafanya kazi kwa njia ya ubaguzi na uzawa.

Taarifa zilizotufikia zilieleza kuwa, kutokana na madai hayo, wafanyakazi wazalendo wameupinga uongozi wa Mkurugenzi huyo raia wa Zambia na kulazimika kufikisha malalamiko yao kwa uongozi wa bodi ya TAZARA huku wakiwa na mabango ya maandishi yakimtaka ajiuzulu.

Katika moja ya madai yao, wafanyakazi hao walimwelezea Devison Mulenga kuwa ni mkurugenzi anayefanya kazi kwa njia ya ubaguzi, hususan katika suala la ajira mpya ambapo kipaumbele chake huwa ni uraia wa mwombaji.

Mmoja wa wafanyakazi hao aliyejitambulisha kwa jina la Telesia Mahagatila aliliambia CHANGAMOTO kuwa, wamelazimika kufikisha malalamiko yao katika uongozi wa bodi mara baada ya kuchoshwa na mwendendo mzima wa mkurugenzi huyo na kwamba wataendelea kumpiga kutokana na ubaguzi huo.

Alisema Mahangatila kuwa, pamoja na ubaguzi unaofanya na kiongozi huyo katika upande wa nafasi za ajira mpya, pia amekuwa akitoa maamuzi yanayoonekana wazi kuwa ni ya kibaguzi.

"Tumechoka na utaifa unaofanywa na Mkurugenzi Mzambia, akija Mzambia mwenzake hapa anapata ajira haraka na muda mfupi tu anapewa cheo wewe uliyekuwa na cheo unashushwa na hata kufukuzwa kazi bila sababu, hatumtaki aondoke kabisa," alisema Mahagatila.

Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa TAZARA, Sylvester Rwegasira alizungumzia msimamo wa wafayakazi kwa mkurugenzi huyo na kusema, hatua yao ya kufikisha ujumbe kwa bodi unatokana na ukweli kuwa wamechoshwa na uongozi wa aina hiyo ya ubaguzi na wameomba malalamiko yao hayo yafanyiwe kazi mara moja.

Rwegasira alisema kuwa, pamoja na kulalamikia ubaguzi, pia wafanyakazi wanalalamikia suala la nyongeza za mishahara ambayo hufanywa kwa kuangalia uzawa na kutozingatia uwajibikaji wa mtu binafsi, na viwango vya mishahara yao na hali hiyo inachangiwa na ubinafsi wa Mzambia huyo.

"Tumeleta ujumbe wetu hapa ili viongozi wa bodi waone na waweze kuyafanyia kazi malalamiko yetu ya muda mrefu,tunasubiri kuona kama watayafanyia kazi, endapo kutaonekana kuendelea kufumbia macho malalamiko haya basi sisi kama wafanyakazi wazalendo tutachukua hatua nyingine nadhani haitakuwa ya kistaarabu kama hii tuliyoichukua hapa," alimalizia kusema katibu huyo wa wafanyakazi wa TAZARA

No comments:

Post a Comment