KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Amazon MP3 Clips

Wednesday, January 12, 2011

Dawa Mseto za Kutibu Malaria Ruksa Kuuzwa Vituo Vya Afya Binafsi


SERIKALI kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imendelea kusisitiza matumizi ya Dawa Mseto kuwa ndiyo tiba sahihi iliyopendekezwa kutibu ugonjwa wa Malaria hivyo imetoa idhini kwa dawa hizo kuuzwa hata na vituo na hospitali binafsi.
Katika waraka ulitolewa hivi karibuni na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na kusainiwa na Katibu Mkuu wa Blandina Nyoni umeangiza Dawa Mseto za kutibu ugonjwa wa Malaria (Artemether and Lumefantrine (ALu)) kuanza kuuzwa katika vituo vya afya na hospitali binafsi.

Awali kabla ya taarifa hii, Dawa Mseto zilikuwa zikipatikana katika vituo vya afya na hospitali za serikali pekee kwa gharama za shilingi 500 kwa dozi moja, huku katika vituo vya afya vya watu binafsi zilikuwa zikiuzwa kwa kati ya shilingi 10,000/= hadi 15,000/= kwa dozi.

Katika waraka huo, wizara imeendelea kusisitiza matumizi ya dawa hiyo kama tiba sahihi na hatua ya kuzitaka zipatikane kwa bei nafuu katika maduka ya dawa binafsi ni hatua ya kurahisisha upatikanaji wake.

Imeelezwa katika waraka huo kuwa, uamuzi wa kutoa idhini kwa vituo vya afya na maduka ya dawa binafsi unatokana na ukweli kuwa karibu asilimia 40 ya wagonjwa wa malaria hupata matibabu katika vituo binafsi.

Waraka huo umeendelea kueleza usahihi wa matumizi ya Dawa Mseto kote nchini kwa kile kilichoelezwa kuwa zimeonyesha ufanisi wa juu kutibu malaria kuliko dawa zingine kwa vile zina mchanganyiko wa kiambata cha 'Artemesinin'.

Katika hatua ya kuendelea kuitambulisha Dawa Mseto kuwa kinga sahihi ya kutibu malaria nchini, Wizara ya Afya imepanga kuendelea na kampeni ya matumizi ya dawa hiyo kupitia vyombo vya habari, vipeperushi na mabango, lengo ni kuwafikishia ujumbe wananchi wa kuwataka waitambue tiba hii sahihi.

No comments:

Post a Comment