KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Wednesday, January 12, 2011

Historia ya Afrika


Kwa ujumla, historia au tarehe, ni kumbukumbu ya maisha ya mwanadamu duniani, hasa ile tarehe iliyosajiliwa na kuhifadhiwa katika vitabu, maandishi mbali mbali, na simulizi au hekaya za mapokeo. Ingawa historia iliyobebwa katika simulizi na hekaya huchukuliwa na baadhi kuwa haina nguvu kwa kukosa ithbati ya maandishi, bado hivi ni vyanzo muhimu vya historia. Mara nyingi historia iliyoko katika maandishi huwa imehifadhiwa katika simulizi na hekaya kwa muda mrefu kabla ya kuandikwa.

Tarehe ya AfrikaHapo kale, bara la Afrika lilishuhudia matukio mengi ya harakati za mwanadamu kuliko mabara mengine ya ulimwengu. Wataalamu wa athari wamegundua athari za binadamu zinazorudi nyuma kufikia hadi miaka milioni minne, na athari za ustaarabu wa Wamisri huko Misri na Wafiniki huko Tunis na sehemu nyenginezo za Afrika ya Kaskazini katika karne ya tisa (9) KK.

Harakati za madola makubwa ya Warumi na Waarabu ziliweza kuonekana kabla ya karne ya nne (4) BK, na Waarabu walianza kuingia Afrika huko Habasha (Ethiopia) tangu karne ya saba (7) BK na kutangaza dini yao na kuieneza katika maeneo mbali mbali ya Afrika pamoja na kuanzisha biashara na ustaarabu na utamaduni na kuimarisha mamlaka zao katika Sudan ya wakati huo tangu karne ya nane 8 ya Kikristo.

Himaya za Ghana, Mali, na Songhai zilikuwa zikijulikana kwa utajiri wao mkubwa na biashara stawi iliyokuwa ikifanyika wakati huo ya dhahabu na bidhaa nyinginezo. Mwisho wa karne ya 15 BK, himaya ya Songhai ilikuwa na nguvu kuweza kuitia chini ya utawala wake mamlaka ya Mali. Sehemu nyingine za kusini ya Afrika zilikuwa wakati huu hazijulikani sana, na historia yake ilikuwa bado haijasajiliwa.

Baina ya karne ya kwanza KK na karne ya kumi na sita (16) BK Watu waliokuwa wakizungumza lugha ya Kibantu watokao sehemu za Nigeria na Cameroon ya leo, ndio waliokuwa wameenea kwenye sehemu mbali mbali kusini mwa bara la Afrika, wakiwa wameanzisha vijiji, mashamba na mamlaka katika sehemu za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ya leo, za Luba na Mwememutapa, lakini makundi ya wachungaji wanyama walianza kuhamia kusini katika karne za 15 na 16 na kukutana na Wabantu. Ndipo walipoanzisha mamlaka zao za Bunyoro, Buganda, Rwanda na Ankole.

Ukoloni
Wazungu walianza kugundua bara la Afrika katika karne ya 15, wakati Wareno walipokuja kwenye fukwe za bara la Afrika kutafuta njia nyepesi na ya amani ya kufikia India, na kuweza kupata nafasi ya kushikilia biashara ya dhahabu na pembe na watumwa ambayo ilikuwa ikiendelea wakati huo katika bara la Afrika. Katika mwaka 1488 Bartolomew Diaz alizunguka rasi ya matumaini mema (cape of good hope), na katika mwaka 1498 Vasco da Gama alifika ufukwe wa Afrika Mashariki na kuendelea mpaka India.

Baada ya hapo, Ureno alianzisha vituo vya biashara Afrika kufuatiwa na Waholanzi, Waingereza, Wafaransa na Wazungu wengineo, na biashara ya Watumwa ikashika kani na kuwa na kasi na nguvu. Wakati huu huu Waturuki walishikilia sehemu za kaskazini ya Afrika na Waomani wakashikilia ufukwe wa Afrika Mashariki. Kati ya 1880 na 1912, Wazungu waliligawanya bara la Afrika baina yao, na nchi zote zikawa chini ya utawala wa Wazungu isipokuwa Liberia na Ethiopia.

Wafaransa wakachukuwa Afrika Magharibi na Kaskazini na kwa hivyo nchi za Afrika Magharibi (Dahomey - sasa [Benin]]), Guinea, Mali, Cote d'Ivoire, Mauritania, Niger, Senegal na Upper Volta (sasa Burkina Faso) zilikuwa chini ya utawala wake. Hali kadhalika, Algeria, Tunisia na Morocco zilitawaliwa na wao. Aidha, Wafaransa walitawala Togoland, Somaliland, Madagascar, Comoro, na Reunion.

Waingereza nao wakatawala Afrika Mashariki na Kusini, na kuwa sehemu ya Sudan na Somalia, Uganda, Kenya, Tanzania (chini ya jina la Tanganyika), Zanzibar, Nyasalanda, Rhodesia, Bechuanaland, Basutoland na Swaziland chini ya utawala wao na baada ya kushinda katika vita huko Afrika ya Kusini walitawala Transvaal, Orange Free State, Cape Colony, na Natal, na huko Afrika ya Magharibi walitawala Gambia, Sierra Leone, the Gold Coast, na Nigeria.

Wareno wakachukuwa sehemu ya Guinea, Angola, na Mozambique na sehemu na visiwa fulani fulani huko Afrika ya Magharibi. Wabelgiji wakachukuwa Kongo na Rwanda-Urundi, na Wahispania wakachukuwa sehemu ya Guinea, Spanish Sahara (sasa Sahara ya Magharibi),na Ifni na sehemu fulani za Morocco. Wajerumani nao wakachukuwa Togoland, Cameroon, na baadhi ya nchi katika Afrika ya Magharibi na Afrika ya Mashariki, lakini baada ya vita vya kwanza vya dunia wakanyanganywa. Wataliani wakachukuwa Libya, Eritrea na sehemu ya Somaliland


Uhuru
Nchi ya kwanza kujitawala wenyewe katika Afrika ni nchi za Afrika ya Kusini zilizojiunga na kujiendesha wao wenyewe katika mwaka 1910. Misri, katika mwaka wa 1922 walikuwa wanajiendesha wenyewe, na Tangier katika mwaka wa 1925. Madola mengi ya Afrika yalianza kupigania uhuru katika miaka ya baina 1950 na 1960, na Wazungu wakasalimu amri na kuanza kutoa uhuru. Libya wakajinyakulia uhuru katika mwaka wa 1951, Eritrea katika mwaka 1952 ikiwa imejiunga na Ethiopia, Morocco katika mwaka wa 1956, na wakarudishiwa Tangier. Katika mwaka huu wa 1956, Sudan na Tunisia vile vile walipata uhuru wao, na Ghana katika mwaka wa 1957, Guinea katika mwaka wa 1958, na vile vile Morocco wakarudishiwa Spanish Morocco.

Katika mwaka wa 1960 Ufaransa ukatoa uhuru kwa Cameroon, the Central African Republic, Chad, Congo (Brazzaville), Cote d'Ivoire, Dahomey (Benin), Gabon, Madagascar, Mali, Mauritania, Niger, Senegal na Upper Volta (Burkina Faso). Vile vile, katika mwaka huu huu wa 1960 Congo (Kinshasa), Nigeria, Somalia, na Togo zikapata uhuru wake, na katika mwaka wa 1961 Sierra Leone na Tanganyika zikapata uhuru, na Afrika ya Kusini ikawa Jamhuri. Katika mwaka wa 1962 Algeria, Burundi, Rwanda, na Uganda zikawa huru, na 1963 zikafuatia Zanzibar, Gambia na Kenya, na katika mwaka wa 1964 Malawi (Nyasaland), na Zambia (Rhodesia ya Kaskazini) zikapata uhuru. Baada ya miaka miwili, katika mwaka wa 1966 Botswana (Bechuanaland)na Lesotho (Basutoland) zikajinyakulia uhuru. Mauritius na Swaziland katika mwaka wa 1968 na vile vile Equitorial Guinea. Uhispania ukairudisha Ifni katika mwaka wa 1969 katika mamlaka ya Morocco.

Aidha, katika mwaka wa 1974 Portuguese Guinea (Guinea-Bissau) ikapata uhuru wake, na katika mwaka wa 1975 Angola, Cape Verde, Mozambique, Sao Tome na Principe zikapata uhuru. Uhispania vile vile ukaitoa Spanish Sahara (Western Sahara) na kuwapa Morocco na Mauritania katika mwaka wa 1976, lakini wananchi wa Sahara wakakataa kuwa chini ya nchi mbili hizi, na kukazuka vita. Mauritania ukaitoa sehemu yake na kuipa Morocco katika mwaka wa 1979, tatizo ambalo mpaka sasa linaendelea baina ya Morocco na Western Sahara, na Umoja wa Mataifa unajaribu kutatua tatizo hili. Waingereza wakawapa uhuru Seychelles katika mwaka wa 1976, na Ufaransa ukatoa uhuru kwa visiwa vya Ngazija (Comoro)

Katika mwaka wa 1977 Djibouti (Afars na Issas) iliyokuwa ikitawaliwa na Wafaransa ikarudi kwa wenyewe. Rhodesia (Zimbabwe) ikapata uhuru katika mwaka wa 1980, na South West Africa, iliyokuwa ikihukumiwa na Afrika ya Kusini ikapata uhuru katika mwaka 1990 na kuitwa Namibia. Ulaya Uingereza ukachukuwa visiwa vya St. Helena na Ascension, na Ufaransa ukaendelea kuhukumu Mayotte na Reunion. Uhispania vile vile ukaendelea kutawala visiwa vya Canary na visiwa viwili vya Ceuta and Melilla, vilivyoko karibu na Morocco vikabakia na Uhispania

No comments:

Post a Comment