KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Thursday, December 30, 2010

Waziri: Sijui lolote kuhusu Dowans



From MWANACHI GAZETI.

WAKATI Sakata la Dowans likiendelea kuumiza vichwa vya wadau mbalimbali nchini ikiwamo Serikali, Naibu Waziri wa Nishati na Madini Adam Malima, amesema hajui lolote kuhusu suala hilo.


Malima alisema hayo jana alipokuwa akizungumza na gazeti hili kwa simu kutoka jimboni kwake Mkuranga, mkoani Pwani.

Alisema hajui lolote kuhusu Dowans wala taarifa kwamba Serikali inatakiwa kuilipa fidia kampuni hiyo ya kufua umeme kwa kuwa yeye sio mtendaji wa wizara.

“Kwani lazima unipigie mimi hujui wengine huko wizarani? Sasa hivi nipo jimboni kwangu naendeleza jimbo bwana. Tafuta wengine kwanza. Nimesema sijui lolote kuhusu hayo malipo ya Dowans,’’alisema

Malima alitoa kauli hiyo baada ya kutakiwa na gazeti hili kueleza nani mmiliki wa Dowans na kwamba lini serikali itaanza kuilipa kampuni hiyo.

Sakata la Dowans lilikuwa likiumiza vichwa vya wadau mbalimbali nchini lilivuta kasi baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Frederick Werema kueleza kuwa mjadala huo umefungwa kwa serikali kukubali kulipa Sh185 bilioni.

“Mimi kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali nimeisoma hukumu hiyo kwa makini na nimeridhika nayo kuwa iko sawa,” alisema Jaji Werema Desemba 27 alipokuwa akizungumza na waandishi kwenye hafla ya kuapishwa Jaji Mkuu mpya Ikulu Dar esSalaam.

Ulipaji wa fidia hiyo unafuatia uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Biashara (ICC Court), Novemba 15, mwaka huu chini ya Mwenyekiti Gerald Aksen na wasuluhishi Swithin Munyantwali, Jonathan Parker ukiamuru Tanesco iilipe Dowans kiasi hicho cha fedha.

Awali baada ya uamuzi huo kufikiwa, Tanesco ilionyesha nia kwamba ingechukua hatua za kukata rufaa, lakini Jaji Werema aliliambia Mwananchi jana katika viwanja vya Ikulu jijini Dar es Salaam kuwa hakuna haja ya suala hilo kukatiwa rufaa, hivyo kuyeyusha ndoto hizo za Tanesco.

Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, William Mhando katika mkutano wake na wahariri wa vyombo vya habari wiki mbili zilizopita alisema shirika lake lingeweza kutoa tamko kuhusu hatua za kuchukua kuhusu uamuzi wa ICC, lakini akaweka wazi kuwa walikuwa wakisubiri uamuzi huo kusajiliwa rasmi katika Mahakama Kuu nchini.

Hata hivyo, kutokana na kauli ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, sasa ni rasmi kwamba hakutakuwa na hatua zozote za kisheria dhidi ya uamuzi wa ICC na badala yake Tanesco watatakiwa kujipanga kuwalipa Dowans mabilioni hayo ya shilingi kama walivyoamriwa.


Akizungumza na Mwananchi baada ya hafla ya kuapishwa kwa Jaji Mkuu mpya, Mohamed Chande Othman jana, Jaji Werema alisema ameshamaliza kuisoma hukumu hiyo na kufanya uamuzi ambao tayari ameukabidhi kwa Waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja kwa ajili ya hatua nyingine baada ya kuridhika nayo.

Tanesco inabeba mzigo wa kulipa gharama hizo wakati ambao nchi imekumbwa na mgawo wa umme untokana na kasoro mbalimbali katika mitambo ya kuzalishia nishati hiyo, sambamba na uamuzi wa kupandishwa kwa gharama za umeme ambao umelalamikiwa na wananchi.

Tayari wasomi, wanaharakati na wanasiasa wamemtaka Jaji Werema kujiuzulu kutokana na matamshi yake kuhusu kwamba serikali itailipa fidia kampuni ya Dowans Tanzania Ltd, wito ambao hata hivyo mwanasheria huyo mkuu ameupuuza.

Katibu Mkuu wa Chadema Dk Willbroad Slaa alisema kitendo cha serikali kukubali kuilipa Kampuni ya Dowans kina maana kwamba fedha zitakazolipwa kwa Kampuni hiyo ni za Watanzania na kufafanua kwamba serikali inalipa deni lisilowahusu.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Abdallah Safari alisema umefikiwa wakati serikali ikaweka wazi nani mmiliki wa Dowans na kuacha kuwaadaa Watanzania.

Mpaka sasa Serikali imeshindwa kusema mmiliki wa Dowans ni nani, jambo ambalo bado linaendelea kuwakosesha usingizi wadau wa umeme nchini

No comments:

Post a Comment