KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Thursday, December 30, 2010

Nahodha achambua vikwanzo kwa Zimamoto



WAZIRI wa Mambo ya Ndani, Shamsi vuai Nahodha, amesema miundombinu mibovu ya Jiji la Dar es Salaam pamoja na uhaba wa vitendea kazi, ni moja ya vikwanzo vcya mafanikio ya kikosi cha zimamoto nchini.

Nahodha aliyasema hayo jana, alipotembelea kikosi cha zimamoto kilichopo Upanga jijini hapa.
“Kitendo cha kuwa na vituo vichache, kinasababisha askari wachelewe katika matukio, unakuta moto umetokea Gongolamboto ,gari linatoka hapa kwenda katika eneo la tukio (Kituo cha Upanga), mpaka wafike inakuwa wamechelewa,” alieleza Nahodha.

Alisema pia kuwa, kutokuwa na vituo maalumu vya kuchota maji ya kuzima moto katika mitaa mbalimbali ya jijini na pia kwenye makazi ya watu, kunasababisha shughuli hiyo kufanyika katika mazingira magumu, kutokana na waokoaji kulazimika kwenda kutafuta maji maeneo ya mbali na lilipo tukio.

“Ipo haja kwa mamlaka za miji na mitaa kuhakikisha kila eneo linakuwa na vituo maalumu vya kuchota maji mengi ya kuzima moto wakati wa matukio hayo”, alisema.

Kutokana na hali hiyo, Nahodha alibainisha kuwa atafanya mazungumzo na viongozi wa sekta zinazohusika ili changamoto hizo ziweze kutatuliwa.

Katika hatua nyingine, gazeti hili liliweza kushuhudia baadhi ya wananchi wakitumia vibaya huduma ya kupiga simu ili kutoa taarifa za moto na majanga, ambazo hutolewa bure na jeshi hilo.
Wananchi wengi, waliokuwa wakipiga simu katika kituo hicho, walikuwa wakitoa kauli za matusi na kejeli badala ya kutoa taarifa za moto kama inavyo takiwa.

Muhudumu wa zamu katika chumba hicho ambaye hakutaja jina lake kutokana na kuwa yeye siye mzungumzaji, alisema anapokea maelfu ya simu kwa siku, lakini kati yake, simu zinazoeleza matukio hazizidi kumi.

“Hapa bora wangetuletea kompyuta ili simu zitakazopigwa tuone namba, kwasababu watu wanaotumia hii namba kupiga ni walewale, mtu unaweza kuepuka kupokea namba ambayo unajua mtu anakutukana,” alisema muhudumu huyo.
Alieleza pia kuwa, wakati mwingine baadhi ya watu hutoa maelezo ya uongo, hali ambayo husababisha usumbufu mkubwa kwa waokozi hao pamoja na kutumia bure raslimali za jeshi hilo

No comments:

Post a Comment