KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Amazon MP3 Clips

Thursday, December 2, 2010

Wassira aipa somo Tume ya Mipango


Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Mahusiano ya Jamii na Uratibu, Stephen Wassira amesema mipango ya muda wa kati na muda mrefu inayopangwa na Tume ya Mipango ni lazima itoe majibu ya matatizo halisi ya Watanzania.

Wassira alisema tatizo kubwa la Watanzania ni umaskini ulio vijijini na mijini hivyo mipango inayopangwa ni lazima iweke bayana ni kwa vipi tatizo hilo linaweza kutatuliwa.
“Ushauri wangu kwenu ni kwamba vipaumbele vitakavyowekwa katika mpango wa muda wa kati na muda mrefu ni lazima viweze kutoa majibu ya tatizo kubwa la umaskini linalowakabili wananchi walioko mijini na vijijini,” alisema Wassira.

Wassira alisema hayo jana jijini Dar es salaam alipotembelea Ofisi za Tume ya Mipango na kuongea na watendaji wake katika ziara yake ya kujitambulisha baada ya kuteuliwa kuwa waziri hivi karibuni.
Alisema kuwa tume hiyo, amnbayo imerejeshwa na serikali ya awamu ya nne, ni chombo ambacho kinajaribu kurejesha utaratibu uliokuwepo zamani wa kupanga mipango inayobainisha nchi inataka kufika wapi na mipango hiyo kuratibiwa ili kuleta matokeo chanya kwa maendeleo ya nchi.

Wassira alisema umaskini hauwezi kupungua kama kilimo hakitaangaliwa kwa umakini kwa sababu Watanzania wengi wanaishi vijijini, hivyo ni lazima mipango yetu iweke bayana ni kwa vipi kilimo kinaweza kuwa tija kwa mkulima.
“Tunapozungumzia kukuza uchumi, tunazungumzia kukuza soko la ndani ambalo haliwezi kupanuka kama miundombinu ni mibovu,” alisema Wasira ambaye katika baraza lililopita alikuwa Waziri wa Kilimo na Maendeleo ya Mifugo.

Alisema ili kilimo kiweze kuwa na tija na kuwa na faida kwa mkulima, ni lazima kuwepo na miundombinu ya kufikisha mazao sokoni tofauti na hali ilivyo sasa ambayo ni vigumu kusafirisha mahindi kutoka Rukwa kwenda Shinyanga.

"Mipango ya nchi pia lazima iangalie aina ya elimu tunayotoa kwa watoto wetu sasa na jinsi itakavyowasaidia katika maisha yao ya baadaye," alisema Wasira na kufafanua kuwa kama elimu haiwezi kutoa majibu ya ajira la baadaye, basi tatizo hilo litakuwa kubwa zaidi.
Waziri Wassira alisema kazi yake haingilii utendaji wa kila siku wa Tume ya Mipango, bali ni kuhakikisha kuwa mipango inafika serikalini kwa utaratibu uliowekwa.

Awali katibu mtendaji wa tume hiyo, Dk Philip Mpango alieleza kuwa kazi zinazoendelea kufanyika katika mwaka wa fedha 2010/11 ni pamoja na kufanya mapitio ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 ili kuhuisha panapostahili na kuandaa Mpango Elekezi wa Miaka Kumi na Tano (2011-2025) wa kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025.

Alisema kazi nyingine ni kuandaa Mpango wa Kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano utakaoanzia mwaka 2011 hadi 2015 na kubainisha mfumo utakaowianisha utayarishaji wa mipango yote ya kitaifa nchini.
Dk Mpango alisema kazi nyingine ni kujenga uwezo wa Tume ya Mipango kitaaluma ili iweze kutekeleza majumu yake ipasavyo

No comments:

Post a Comment