KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Thursday, December 2, 2010

Mawakili wampinga Dk Shein kuteua majaji

Rais wa Zanzibar,Dk.Mohamed Ali Shein

CHAMA Cha Mawakili Zanzibar (ZLS) kimepinga uteuzi wa majaji wa Mahakama Kuu uliofanywa na Rais wa Zanzibar (SMZ), Dk Ali Mohammed Shein Novemba 29 mwaka huu wa 2010 na kuhoji uhalali wa uwepo wa Jaji Mkuu wa Zanzibar aliyestaafu.

Tayari ZLS kimemwandikia barua Dk Shein Novemba 30, ambayo Mwananchi ilifanikiwa kuiona nakala yake kikieleleza kuwa hakijaridhishwa na uteuzi huo kwa kuwa haukuzingatia vigezo na kwamba, umekiuka sheria kwa kuwa hakijashirikishwa.

Barua hiyo ya ZLS ya Novemba 30, mwaka huu yenye kumbukumbu namba ZLS/IKULU/001 tayari imepelekewa Dk Shein ikiwa na saini ya Rais wa chama hicho, Yahya Khamis Hamad na mawakili 15 kwa niaba na wenzao zaidi ya 50, kupinga uteuzi huo wa majaji uliofanywa na Rais Dk Shein.

Novemba 29, mwaka huu Rais wa Zanzibar kwa mamlaka aliyopewa na katiba ya SMZ aliteua majaji wanne wa Mahakama Kuu pamoja na Mwenyekiti wa Mahakama ya Ardhi, Haroub Sheikh Pandu.

Majaji wanne walioteuliwani Abdul-hakim Ameir Issa, Fatma Hamid Mahmoud, Mkusa Isaac Sepetu na Rabia Hussein Mohammed.

"Rais, katika uteuzi wako huo, ambao umetumia mamlaka uliyopewa na Katiba ya Zanzibar ya 1984 kifungu cha 94(2) na (3), Chama cha Mawakili hakina mashaka na uteuzi wa Abdul-hakim Ameir Issa, wala uteuzi wa Mwenyekiti wa Mahakama ya Ardhi, Haroub Shehe Pandu. Mashaka yetu yapo katika uteuzi wa waheshimiwa kuanzia nambari 2 mpaka 4,” Sehemu yabarua yao kwa Dk Shein ZLS inasomeka:

Hata hivyo, ZLS ilisema Rais hawezi kuwaelewa majaji wala hakuna sababu ya kumjua yeyote kati ya majaji wanne aliowateua, lakini wanachoamini uteuzi wake unatokana na ushauri uliopewa na Tume ya Utumishi ya Mahakama iliyoanzishwa chini ya Sheria Namba 13 ya mwaka 2003 ambayo Mwenyekiti wake ni Jaji Mkuu wa Zanzibar, Hamid Mahmoud Hamid pamoja na wasaidizi wa rais wengine katika sekta ya sheria.

“Rais, sisi mawakili ambao tumetia saini barua hii tukiwa ni wadau wakubwa katika sekta hii, tuna imani kubwa nawe ..., lakini tunaamini washauri wako hawakukutendea haki walipokushauri uwateue Fatma, Mkusa na Rabia kuwa majaji wa Mahakama Kuu,” ilieleza barua ya ZLS na kuongeza:

"Rais, haitoshi tu kusema kwamba Jaji Mteule ametimiza masharti ya Katiba na hivyo anafaa kuwa Jaji wa Mahkama Kuu.

Vipo vigezo vyengine ambavyo ni lazima viangaliwe kabla ya uteuzi wa jaji wa Mahakama Kuu kufanyika. Nafasi ya ujaji ni nafasi ya juu kabisa katika ngazi ya mahakama zetu na pia ni nyeti. Utaalamu uliobobea, rekodi iliyothibitika, umakini wa hali ya juu, kujiamini, uadilifu na umahiri wa hali ya juu - vyote kwa pamoja vinahitajika.”

Mawakilili hao walisema kuwa kifungu cha 94(2) cha Katiba kinasema kuwa Majaji wa Mahakama Kuu watateuliwa na Rais kutokana na mapendekezo ya Tume ya Utumishi ya Mahakama wakati.

“Rais, Chama cha Mawakili kina mjumbe katika Tume ya Utumishi ya mahakama. Pia wajumbe wengine wa tume ni watu walio karibu na Chama cha Mawakili. Tunapenda kukuthibitishia kwamba, hakuna kikao chochote cha Tume hiyo ambacho kimemjadili Rabia Hussein. Hivyo uteuzi wake umefanywa kinyume kabisa na Katiba ya Zanzibar na hauwezi kusimama katika macho ya sheria,” walisema mawakili hao na kuongeza:


“Wateule wa ujaji tuliowataja hapo juu, hawatokuwa majaji rasmi, kikatiba na kuanza kazi ya ujaji wa Mahakama Kuu, mpaka baada ya kula kiapo. Hilo likishafanyika, itakuwa dhiki sana kutenugua uteuzi huo. Hivyo, tunakuomba Mheshimiwa Rais, utafakari upya juu ya uteuzi huo na uridhike kuusitisha,” walisema mawakili hao.

Mmoja wa majaji hao wanne waliolalamikiwa (Fatma Hamid Mahmoud) ametajwa kuwa ni mtoto wa Jaji Mkuu wa Zanzibar Hamid Mahmoud huku mawakili hao wakieleza pia kwamba uwepo wake katika wadhifa wa jaji mkuu una mashaka kikatiba na ukiukwaji wa taratibu za kisheria.

“Mheshimiwa Rais, sisi kama chama cha mawakili, tunaamini hata uwepo wa Hamid Mahmoud kama Jaji Mkuu wa Zanzibar una mashaka tele ya kikatiba. Inaeleweka kwamba Hamid Mahmoud alistaafu kwa hiari alipotimiza miaka 60," imeeleza barua ya ZLS na kuongeza:

"Kama alitakiwa kuendelea kushika wadhifa huo, alipaswa kwanza kupewa mkataba wa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu. Mkataba wa aina hiyo ulilazimu kujadiliwa na Tume ya Utumishi ya Mahakama kwa mujibu wa kifungu cha 95 (1) cha Katiba ambacho kinasema: "Bila ya kuathiri masharti ya kifungu hiki, Jaji wa Mahakama Kuu ataendelea kushika wadhifa wake hadi kufikia umri wa miaka 60 ambapo anaweza kustaafu kwa hiari ama kuendelea hadi kufikia umri wa miaka 65 ambapo atastaafu kwa lazima.


Aidha (2) Bila ya kuathiri masharti ya kijifungu cha (1) cha kifungu hiki, Rais kwa kushauriana na Tume ya Utumishi ya Mahkama anaweza kumteua tena Jaji aliekwisha staafu kushika madaraka ya Jaji wa Mahkama Kuu kwa muda au kwa ajili ya kesi maalum.


Kutokana na maelezo hayo ZLS walisema kuwa hakukuwa na sababu yoyote kuendelea jaji mkuu huyo kuendelea kufanya kazi katika mkataba kwa kuwa Katiba ilikuwa inamruhusu kuendelea na ajira hadi kufikia miaka 65".

Barua ianeleza kuwa kama Jaji Mkuu alitakiwa kuendelea na nafasi yake baada ya kumaliza utumishi wake, ililazimu mambo mbalimbali kufuatwa kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar (kifungu cha 94(1), 94(2), 94(6)(a) na (b).

Waliyataja mambo hayo kuwa ni pamoja na kuwa ateuliwe kuwa Jaji wa Mahkama Kuu, Mapendekezo ya uteuzi wake yatokane na Tume ya Utumishi ya Mahkama; Endapo ni Jaji wa Mkataba, “masharti ya kazi, marupurupu na kiinua mgongo cha jaji wa mkataba wa kipindi maalum yataamuliwa na Tume ya Utumishi ya Mahkama.
Wameleeza katika barua hiyo kuwa kifinga cha 94(6)(b) kinasema iwapo atateuliwa kuwa jaji basi atakula kiapo cha Jaji wa Mahkama Kuu.

“Kuendelea kwake kuwa Jaji Mkuu kunakuwa na mashaka ya kikatiba na sisi tusingependa nchi yetu iwe na Jaji Mkuu ambaye uteuzi wake umegubikwa na kasoro kadhaa za kikatiba,” ilieleza ZLS.

Kwa mujibu wa ZLS, suala la kuwa jaji au Jaji Mkuu wa mkataba linalopigwa vita katika Mahakama za Jumuiya ya Madola kwa sababu mikataba inaondoa kinga ya kikatiba aliyonayo Jaji wa Mahkama Kuu, hivyo kudumaza uhuru wa Mahakama na kwamba, jaji wa mkataba hawezi kufanya kazi yake bila ya hofu wala woga kwa mamlaka ya uteuzi.

Hata hivyo ZLS ilisema kuwa haihoji mamlaka ya rais kikatiba bali wanatoa tahadhari kwake kama mchango wao katika kujenga mahakama iliyotukuka, hasa kutokana na wananchi kupoteza imani kwa mahakama ziliopo sasa hivyo ni vyema kuepuka mambo yanayoonekana dhahiri kulenga katika kudumaza ufanisi wa mahakama katika suala la utoaji haki.

Nakala ya barua hiyo imepelekwa kwa Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Jaji Mkuu waTanzania; Jaji Mkuu wa Zanzibar; Waziri wa Katiba na Sheria wa Zanzibar; Waziri wa Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Zanzibar; Mwanasheria Mkuu waTanzania; Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar; Mkurugenzi wa Mashtaka ya Jinai

No comments:

Post a Comment