KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Wednesday, December 22, 2010

Wanane mbaroni kwa mauaji faru wa JKWATU wanane wamekamatwa, wakituhumiwa kumuua, faru mweusi mmoja kati ya watano waliopokewa na Rais Jakaya Kikwete, kutoka nchini Afrika Kusini.

Faru huyo dume aliyekuwa akijulikana kwa jina la George (12), aliyeletwa nchini na kampuni ya uwekezaji ya Grumeti Reserve, aliuawa na majangiri Desemba 12 mwaka huu na kutoweka na pembe zake katika mbuga ya wanyama ya Serengeti, eneo la Nyabeho.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk Ladislaus Komba, alisema pamoja na mambo mengine, watuhumiwa hao pia wanasaidia la polisi kufanikisha jitihada za kupata mtandao wa majangiri na pembe iliyochukuliwa.

“Katika kutafuta ushahidi wa silaha iliyotumika, mzoga ulikaguliwa kwa kutumia chombo maalumu kilichotolewa na Franfurt Zoological Society na kufanikiwa kupata kipande kimoja cha risasi, ambacho kitasaidia katika uchunguzi,’’ alisema Dk Komba

Kuhusu ulinzi wa faru wanne waliobaki, Dk Komba alisema wamewekewa mitambo ya kisasa zaidi itakayosaidia kuratibu mwenendo wao, ikiwamo ujengaji wa vituo vipya na askari kupewa mbinu mpya.

Alisema ongezeko la ujangiri linatokana na baadhi ya jamii, hasa Mashariki ya Kati na ya Mbali, kuamini kuwa unga unaotokana na pembe za faru, ambao ni kati ya wanyama walio hatarini kutoweka, una chembechembe ambazo zina dawa yenye nguvu sana .


Akizungumzia mazingira ya kifo alisema kabla ya hapo kifaa cha mawasiliano ambacho faru huyo na wenzake wanne waliwekewa, kilipoteza mawasiliano na walinzi na katika kufuatilia walibaini kuwa aliuawa na majangili.

Kuhusu ahadi ya Rais Kikwete ya kuwawekea faru hao ulinzi mkali unaozidi wa kwake, Dk Komba alisema tukio hilo limewashtua kwa kuwa wanafanya jitihada kubwa za kuwalinda faru, ambao ni aina moja kati ya tano za wanyama wakubwa barani Afrika ambao ni kivutio kikubwa cha utalii.


Alisema wanajitahidi kuongeza nguvu kwenye ulinzi ili kukabiliana na matukio hayo. Kuanzia mwishoni mwa mwaka 2009 hadi sasa, zaidi ya tembo 15 wameuawa na meno kuchukuliwa.

Hata hivyo alisema hawajajua soko kuu la meno ya tembo liko wapi ,hata hivyo alikiri kuwa kuna taarifa za kuwepo kwa soko zuri la meno ya tembo na kuwa wanashirikiana na polisi kwa upelelezi

No comments:

Post a Comment