KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Thursday, December 2, 2010

Wachinja nyama Vingunguti wagoma


Raymond Kaminyoge

WAFANYABIASHARA wa nyama katika machinjio ya Vingunguti, jijini Dar es Salaam, kwa siku nzima ya jana waligoma kuchinja ng’ombe wakishikinisha uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, kuwawekea jenereta la kufulia umeme, ili kuchukua nafasi ya ule wa Tanesco unaokatika mara kwa mara.

Mgomo huo ulioanza saa 8.00 usiku, ulisababisha bei ya nyama kupanda kutoka Sh 4,000 hadi kufikia Sh 6,000 kwa kilo moja, katika baadhi ya maeneo.

Baadhi ya wafanyabiashara hao, waliliambia Mwananchi, jana kwamba, mgomo huo umesababishwa uongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, kushindwa kuwawekea jenereta ambalo lingetoa mwanga katika kipindi ambacho umeme wa Tanesco unakuwa umekatika.

“ Sasa ni miaka mitano tunadai tuwekewe jenereta bila mafanikio, umeme wa Tanesco umekuwa ukikatika mara kwa mara, kazi ya kuchinja ng’ombe tunaifanya kuanzia saa 8.00 usiku, kukiwa na giza tutaifanyaje kazi hiyo,” alisema Kaguta Mazera, mmoja wa wafanyabiashara hao.

Aliongeza kuwa katika machinjio hayo, zaidi ya ng’ombe 400 huchinjwa kwa siku na kutozwa Sh 3,500 kwa kila ng’ombe na Halmashauri ya Manispaa ya Ilala kama ushuru wa uchinjaji na mhuri.

Alisema kilichowafanya wagome ni kuushinikiza uongozi wa halmashauri hiyo kuwapatia jenereta, baada ya baadhi ya wafanyabiashara kupoteza ng’ombe wao mara kwa mara kwenye machinjio hayo.

“ Kukiwa na giza mambo mengi mabaya yanatokea, kuna wengine wanapoteza hadi ng’ombe, wengine wanapoteza nyama, sasa hii ni kero ambayo tumeona haiwezi kuachwa hivi hivi ikizingatiwa kwamba tunachangia mamilioni ya fedha kama ushuru,” alisema.
Kwa mujibu wa wafanyabiashara hao, wakati wa mgomo huo, magari yalizuiwakupita kwenye eneo hilo na kusababisha polisi kuingilia kati kuzuia vurugu zilizotokea.

Mfanyabiashara mwingine wa eneo hilo, Ali Lubeya, alisema machinjia hayo pia yanakabiliwa na ukosefu wa vyoo na hivyo kuwafanya wafanyabiashara kujisaidia ovyo kwenye vichaka vilivyopo jirani na eneo hilo.

“ Choo kimoja kilichopo hutumiwa na madaktari wa mifugo na hukifunga kwa kufuri wanapomaliza shida zao, hivi kwanini tunanyanyapaliwa wakati tunatozwa ushuru mkubwa,” alisema.

Aliongeza kwamba pamoja na kutozwa ushuru, lakini huwa hawapewi risiti jambo ambalo wanahisi kuwa kiasi kikubwa cha fedha zinazopatikana, zinaweza kuwa zinaishia kwenye mikono ya watu wasiokuwa waminifu.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, hakupatikana kueleza sakata hilo baada ya kuelezwa na Katibu muhtasi wake kwamba alikuwa kwenye mkutano.

Hata hivyo baadaye, wafanyabiashara hao walipiga simu katika chumba cha habari cha Mwananchi, wakitoa taarifa kuwa tayari wameshapelekewa jenereta.

“Tunashukuru kilio chetu kimesikika, hii inaonyesha jinsi viongozi wetu wanavyofanya kazi kwa shinikizo la migomo,” alisema

No comments:

Post a Comment