KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Thursday, December 2, 2010

Dk Kawambwa aja na mpango wa ‘K’ tatu kuboresha elimu


WAZIRI wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi (MOEVT), Dk Shukuru Kawambwa, ameibuka na mkakati wake wa ‘K’ kwa ajili ya kuboresha elimu ya msingi nchini, katika kipindi chake cha uongozi wa wizara hiyo nyeti nchini.

Utafiti uliofanywa na Shirika lisilo la Kiserikali la Twaweza hivi, karibuni ulionyesha kwamba asilimia kubwa ya wanafunzi wanaohitimu elimu ya msingi, hawawezi kusoma sentensi za kiengereza na hesabu wanazofundishwa wanafunzi wa darasa la pili.

Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Mo Ibrahim kuhusu ubora wa elimu katika nchi mbalimbali za Afrika uliipa Tanzania nafasi ya 47 kati ya nchi 50 zilizofanyiwa utafiti huo.

Jana Dk Kawambwa alisema elimu ya msingi ya Tanzania hairidhishi na kwamba katika uongozi wake katika wizara hiyo, atasimamia mkakati wa ‘K’ tatu ili kuhakikisha wanafunzi wa shule za msingi wanapata elimu bora itakayowasaidia baada ya kuhitimu.

"Tutatilia mkazo mpango wa K tatu, ili kuwawezesha wahitimu wetu wa elimu ya msingi, kupata elimu bora itakayowasaidia hata baada ya wao kuhitimu na siyo ya kufanyia mtihani tu.," alisema waziri huyo.

Akifafanua mpango huo wa ‘K’ tatu, Dk Kawambwa alisema ‘K’ ya kwanza ni kumwezesha mwanafunzi kujua na kuweza kuhesabu vizuri.

"Hesabu ndio maisha yako, kila sehemu na wakati unafanya hesabu hata katika familia yako ukiwa mtu mzima unafanya hesabu. Mfano una midomo mitatu ndani ya familia na kipato chako kinaruhusu kulisha midomo hiyo, kwa kutumia hesabu utaweza kujua iwapo uongeze mdomo mwengine au la," alisema Dk Kawambwa.

Alisema ‘K’ ya pili ni kwa mwanafunzi kuweza kusoma kwa ufasaha na kuelewa kile anachokisoma katika lugha za Kiswahili, Kiiengereza na hata lugha nyingine za kimataifa.

"Hivyo tutajitahidi kuhakikisha tunapata walimu wazuri wa lugha kwa ajili ya shule za msingi ili wanafunzi hawa waweze kusoma na kuelewa vizuri. Ni aibu na haipendezi mwanafunzi anahitimu elimu ya msingi halafu hajui kusoma," alisema.

Alisema katika ulimwengu wa sasa habari ina thamani kubwa katika maisha ya mwanadamu hivyo kama wahitimu hao hawataweza kusoma na kuelewa ni wazi kuwa watashindwa kupata habari muhimu za kiuchumi, kisiasa na hata kijamii na kusababisha maisha yao kuwa magumu.

Dk Kawambwa alisema ‘K’ ya tatu ni kwa muhitimu wa elimu ya msingi kuweza kuandika na maandishi yake kuweza kueleweka na mtu mwengine yeyote atakayeyasoma bila ya kupata tabu.


"Ulimwengu wa sasa ni ulimwengu wa maandishi kila utakachofanya unahitaji kuandika, ukiomba mkopo unatakiwa kuandika, kazi unatakiwa kuandika, biashara unatakiwa kuandika hata ukijiwekea malengo ya maisha unatakiwa kuandika. Hatutafanikiwa kama mhitimu wa darasa la saba hawezi kuandika,” alisema Dk Kawambwa.Mwisho

No comments:

Post a Comment