KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Thursday, December 2, 2010

'Muhimbili kuna mgomo baridi'


Nora Damian
BAADHI ya wafanyakazi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, jijini Dar es Salaam, wamesema wamekuwa wakifanya kazi lakini wakiwa wanaendesha mgomo baridi unaotokana na matatizo mbalimbali yanayowakabili, ikiwemo mishahara midogo.

Wafanyakazi hao walisema hayo jana, walipozungumza na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hadji Mponda, aliyetembelea hospitali hiyo ili kujitambulisha kwa wafanyakazi.

Mmoja wa wafanyakazi hao, Premis Saidia, alisema wamekuwa wakifanya kazi nyingi na kwa muda wa ya saa 24, lakini wanalipwa mishahara midogo.

"Watu wanafanya kazi kwa mgomo baridi wapo kama hawapo kutokana na matatizo hayo,"alisema Saidia.
Alisema wafanyakazi wengi wa sekta ya afya ni wazuri na wawajibikaji lakini hawalipwi mishahara na marupurupu makubwa.

Alisema tatizo hilo ndilo linalosababisha baadhi ya watumishi wa sekta hiyo, kukimbia kwenye hospitali za watu binafsi na kwenda nje ya nchi.


Wafanyakazi hao pia walilalamikia kutokuwepo kwa Mkurugenzi Mtendaji katika hospitali hiyo na kwamba nafasi hiyo imekuwa wazi tangu Novemba mwaka jana, alipostaafu mkurugenzi wa zamani.


"Nachelea kuamini kwamba hospitali hii inaendeshwa kisiasa. Tangu mkurugenzi amestaafu ni mwaka mmoja sasa anakaimu mtu mwingine hata maamuzi yake yatakuwa ya kukaimu,"alisema Saidia.

Mfanyakazi mwingine, Theresia Yomo, aliiomba serikali kuwaangalia wafanyakazi wanaosihi na virusi vya Ukimwi ambao bado wana nguvu za kufanya kazi ili waweze kupata posho na chakula.

Rehema Mwaipaja alilalamikia ubaguzi katika kuwasomesha madaktari na wauguzi na kuacha watumishi wa kada nyingine.


"Wataalamu wa kada zote tunahitaji kwenda na wakati lakini wanasomeshwa ni madaktari na wauguzi tu, je mgonjwa anahudumiwa na watu hao wawili,"alihoji Mwaipaja

No comments:

Post a Comment