KARIBU MAISHANI
KARIBU MAISHANI
Thursday, December 2, 2010
Uandikishaji wapiga kura Sudan kusini
KHARTOUM, Sudan
WAKAZI wa Sudan kusini leo wanaanza kujiandikisha kwa ajili ya kupiga kura ya maamuzi itakayofanyika Januari tisa mwaka ujao.
Habari zinasema kuwa takribani watu milioni tano wa kusini mwa Sudan watajiandikisha katika zoezi ambalo litaendelea hadi Desemba mosi mwaka huu.
Kura ya maamuzi kuhusu iwapo eneo la kusini mwa Sudan lijitenga na eneo la kaskazini mwa nchi hiyo au la itafanyika mapema mwakani.
Habari zinasema kuwa, serikali ya Sudan imeilaumu Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kuhimiza kujitenga eneo la kusini na hivyo kusambaratisha nchi hiyo kubwa zaidi barani Afrika.
Wakati huo huo jeshi la Sudan limelituhumu jeshi la Mamlaka ya Ndani ya Sudan Kusini kuwa linachochea mapiano huko Darfur.
Wakati huo huo, habari kutoka Sudan kusini zinasema kuwa jeshi la Kaskazini limefanya mashambulizi ya angani dhidi ya eneo la mpaka wa pande mbili hizo.
Haikubainika mara moja ni eneo gani haswa lililoshambuliwa ingawa msemaji wa jeshi la eneo la kusini Philip Aguer amesema kuwa makombora ya kaskazini yamelenga eneo lililoko katikati ya Bahr Gazal na kusini mwa Darfur.
Ofisa wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa katika eneo la Sudan Kusini David Gressly amesema kuwa mashambulizi kama hayo ni hatari kwa mustakabali wa makubaliano ya amani ya mwaka 2005 kati ya Juba na Khartoum.
Serikali kuu ya Khartoum haijasema lolote kuhusiana na tukio hilo.
Wiki iliyopita nchini humo, msaidizi wa Rais wa Sudan, Nafie Ali Nafie aliikosoa vikali Harakati ya Ukombozi ya Kusini mwa Sudan SPLM kwa kuwashawishi wakazi wa eneo la kusini waafiki kujitenga eneo hilo utakapowadia wakati wa kufanyika kura ya maoni mapema mwakani.
Habari zinasema kuwa, Msaidizi wa Rais Omar Hassan al Bashir ameeleza kuwa, Harakati ya SPLM inawashawishi wakazi wa kusini walioko katika maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo warejee katika eneo la kusini kwa shabaha ya kushiriki kwenye zoezi la kura ya maoni na hatimaye kupiga kura ya kujitenga eneo hilo.
Msaidizi wa Rais wa Sudan amesema kuwa, kitendo cha Harakati ya SPLM kinakiuka makubaliano ya amani yaliyotiwa saini Naivasha Kenya mwaka 2005.
Amesema kuwa, Harakati ya SPLM inadai kwamba wananchi wako huru katika kutoa maamuzi yao kwenye kura ya maoni, katika hali ambayo imethibiti kuwa madai hayo ni uwongo mtupu.
Nafie Ali Nafie pia ameitaka Harakati ya SPLM ifanye juhudi za kumaliza hitilafu zilizoko katika eneo linalozozaniwa na pande mbili la Abyei kwa njia za kiadilifu, kabla ya kuitishwa kura ya maoni
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment