KARIBU MAISHANI
KARIBU MAISHANI
Thursday, December 2, 2010
Mafuta ya kuzuia wanawake kupata Ukimwi yagundulika
Neville Meena, Vienna-Austria
DUNIA itakuwa inazidi kushangilia ushindi dhidi katika tafiti dhidi ya Ukimwi baada ya wanasayansi wanasayansi kueleza kuwa wamegundua mafuta yenye dawa ambayo wanawake wanapaka kabla na baada ya tendo la ndoa na hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa uwekezekano wa kuambukizwa ugonjwa huo hatari unaodhoofisha kinga ya mwili.
Wanasasansi pia wameeleza kuwa mafuta hayo yanapunguza kwa asilimia 50 uwezekano wa kupata vijidudu aina ya HSV-2, ambavyo husababisha malengelenge kwenye sehemu za siri za mwanaume.
Habari za matokeo hayo ya utafiti zimetolewa katika kipindi ambacho dunia inashangilia ugunduzi wa dawa ambayo imebainika kuwa inapambaa na Ukimwi kwa asilimia 90 uliotangazwa wiki iliyopita na Taasisi ya Marekani ya Magonjwa ya Kuambukiza na Athari Zake (NIAID).
Matokeo hayo ya utafiti wa kisayansi yanayobainisha usalama na uwezo wa mafuta ambayo kitaalamu yanaitwa tenofovir, kuzuia maambukizi ya Ukimwi yalitangazwa jana na mjini Vienna, Austria na Kituo cha Utafiti wa Magonjwa ya Ukimwi cha Afrika ya Kusini (Caprisa).
Mmoja wa wataalamu walioongoza utafiti huo, Dk Quarraisha Abdool Karim, ambaye ni mkurugenzi mshiriki katika kituo cha Caprisa, alisema mafuta hayo yana uwezo wa kupunguza zaidi ya nusu ya maambukizi ya Ukimwi nchini Afrika ya Kusini katika kipindi cha miaka kumi ijayo.
Katika mkutano wa kimataifa wa Ukimwi unaofanyika mjini hapa watafiti hao kutoka Afrika ya Kusini walisema kuwa mafuta hayo ambayo yana kiwango cha asilimia moja ya dawa za kawaida za kupunguza makali ya Ukimwi, yana uwezo wa kumkinga mwanamke kwa asilimia kati ya 39 na 55 asiambukizwe Ukimwi iwapo atajamiiana na mwathirika wa ugonjwa huo.
Dk Quarraisha ambaye pia ni profesa wa epidemiolojia kwenye Chuo Kiku cha Columbia, Marekani aliwaambia mamia ya wanasayansi na watafiti walioshiriki katika hadhara ya kutangazwa kwa dawa hiyo kuwa matokeo ya utafiti pia yalithibitisha dawa ya Tenofovir kuwa na uwezo wa kukabiliana kwa asilimia 51 na malengelenge katika sehemu za siri.
Katika nchi nyingi za bara la Afrika hasa zile zilizo kusini mwa Jangwa la Sahara baadhi ya wanawake wamekuwa wakiambukizwa ugonjwa wa Ukimwi kutokana na kutokuwa na uwezo wa kukataa kufanya ngono na waathirika wa ugonjwa huo au kuwepo katika mazingira ambayo hawawezi kutumia kinga wakati wa tendo la ngono.
“Mafuta ya Tenofovir yanaweza kuziba pengo katika mchakato wa kuzuia maambukizi ya ukimwi hasa kwa mwanamke ambaye hana uwezo wa kimaamuzi kuhusu usalama wake au kutumia kondom wakati wa tendo la ndoa dhidi ya mwenzi wake ambaye ni mwanamume,” alisema Dk Quarraisha katika hafla ambayo pia ilihudhuriwa na Waziri wa Afya wa Afrika Kusini, Dk Aaron Motsoaledi.
Kwa mujibu wa Dk Quarraisha teknolojia hiyo mpya ni muhimu sana kuwa chachu ya mabadiliko katika vita dhidi ya Ukimwi hasa katika nchi za kusini mwa Afrika ambako wanawake wamekuwa wavumilivu sana dhidi ugonjwa huo hatari.
Naye Waziri Motsoaledi aliiambia Mwananchi baada ya uzinduzi huo kuwa “mafanikio yaliyopatikana ni ya kujivunia barani Afrika” na kwamba huo ni uthibitisho kwamba majibu ya matatizo mengi yanayolikabili bara hilo yanapatikana kutoka kwa Waafrika wenyewe.
Ikiwa katika mfumo wa vidonge, Tenofovir ni moja ya kati ya dawa tatu ambazo zimekuwa zikitumika kwa pamoja katika kukabiliana na maambukizi ya Ukimwi na kazi yake kubwa ni kuzuia ukuaji wa VVU ndani ya chembechembe (seli) za mwili wa binadamu.
Hata hivyo, matokeo ya tafiti za kisayansi yanaonyesha kuwa tenofovir ina uwezo mkubwa wa kumkinga mwanamke asiambukizwe virusi vya Ukimwi pia vijidudu vya malengelenge vinavyojulikana kitaalamu kwa jina la HSV-2 kwa mafuta hayo kupakwa katika njia ya uzazi kabla ya tendo la kujamiiana.
Mkurugenzi wa Caprisa, Dk Salim Abdool Karim alisema kuwa "matokeo ya utafiti huu ni hatua muhimu ya kwanza kuelekea katika mafanikio makubwa zaidi ya kuukabili ugonjwa wa Ukimwi”.
"Tenofovir Gel ina uwezo wa kuzuia maambukizi ya VVU pia kuvikabili vijidudu vinavyosababisha malengelenge sehemu za siri ambavyo pia ni kichocheo cha maambukizi hayo,” alisema Dk. Karim ambaye pia ni muhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kwazulu – Natal nchini Afrika ya Kusini.
Kwa mujibu wa wataalamu hao, mwanamke anaweza kutumia si zaidi ya dozi mbili katika muda wa saa 24 na anaweza kuweka dawa hiyo katika sehemu saa 12 kabla ya tendo la kujamiiana.
Utafiti huo uliwahusisha wanawake 889 ambapo kati yao 98 walipatwa na maambukizi ya Ukimwi katika kipindi cha majaribio ijapokuwa Dk. Karibu alisema hawakutafiti sababu za maambukizo hayo kwani ni idadi ndogo sana ikilinganishwa na wale wasioambukizwa.
Utafiti huo uliogharimu dola 17.6 za Kimarekani, ulifadhiliwa kwa pamoja na serikali za Afrika Kusini na Marekani kwa kumtumia Wakala wa Ubunifu wa Teknolojia na Shirika la msaada la Marekani (USAID) sawia.
Mashirika ya kimataifa yanayojishughulisha na utafiti wa tiba ya Ukimwi yameshangilia mafanikio hayo ya Caprisa. Dk. Seth Berkley, ambaye ni rais wa Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Dawa ya Ukimwi (IAVI), alisema ugunduzi huo ‘zama mpya’ katika mapambano dhidi ya Ukimwi hasa barani Afrika ambako wanawake ni zaidi ya asilimia 60 ya watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi.
Mkurugenzi wa NIAID, Dk. Anthony Fauci alisema hatua iliyofikiwa na Caprisa inaweka matumaini mapya si kwa watafiti pekee katika jitihada za kutafuta tiba, bali pia uwezo kwa wanawake ambao ni waathirika wakubwa wa Ukimwi duniani
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment