KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Thursday, December 2, 2010

Mawakili wa Ghailani wajaribu kumnasua


NEW YORK, Marekani

MAWAKILI wanaomtetea Mtanzania Ahmed Khalfan Ghailani anayetuhumiwa kwa makosa ya ugaidi wamepambana vikali mahakamani nchini Marekani, iwapo mtuhumiwa huyo hahusiki na ulipuaji wa balozi za Marekani nchini Tanzania na Kenya mwaka 1998.

Katika siku ya pili ya kusikilizwa kwa hoja za mwisho kwenye kesi dhidi yake juu ya kushiriki katika mashambulio dhidi ya balozi hizo za Marekani, wakili Peter Quijano aliihakikishia mahakama kwamba mteja wake, yaani Ghailani hakuwa akijua chochote na kwamba alidanganywa.

Kesi hiyo ya kwanza kusikilizwa katika mahakama za kiraia kwa mtuhumiwa huyo aliyekuwa akishikiliwa katika gereza la Guantanamo iliyoanza kusikilizwa October 12 mwaka huu imekuwa kivutio hasa ikitarajiwa kutoa uamuzi wa wazi tofauti na kesi nyingine za aina hiyo ambazo zimekuwa zikisikilizwa katika mahakama maalum za kijeshi.

Quijano alisema waendesha mashtaka wa Marekani walikuwa hawana udhibitisho kuwa mtanzania huyo alifahamu kwamba alikuwa akisaidia kupanga njama za mashambulio hayo yaliyosababisha vifo vya watu 224.

Wakili huyo alikosoa pia ushahidi uliotolewa na serikali akisema ni dhaifu na wa kutiliwa shaka, hukua akikanusha pia hoja kwamba Ghailani alikwenda Pakistan kabla ya mashambulio hayo kutokea.

"Ingekuwa Ahmed alikuwa ndani ya ndege iliyokuwa ikielekea Pakistan, mngemsikia japo shahidi mmoja. Hakujakuwa na hata mmoja. Ahmed hajakuwemo ndani ya ndege hiyo na nyaraka zilizotolewa ni za bandia," alisisitiza wakili Peter Quijano.

Naye mwendesha mashtaka wa serikali, Michael Farbiarz, alisema kuwa Ghailan (36) ni mwongo na kwamba alikuwa mwanachama wa mtandao wa al-Qaida aliyekuwa akilipwa na kuhusika na mashambulio hayo.

Farbiarz alisema hoja hizo hazina msingi kwa kuwa siku ya mashambulio, Ghailani aliacha kila kitu alichokuwa nacho maishani mwake, marafiki zake, familia yake, kazi yake na jina lake, akisisitiza hakuna ukweli katika madai kwamba alidanganywa.

Ghailan alikamatwa nchini Pakistan mwaka 2004, na kupelekwa katika jela ya siri ya shirika la ujajusi la Marekani CIA kabla ya kuhamishiwa katika jela la Guantanamo Bay.

Wakati wakili wake akisimamia vifungu anavyoona vitasaidia kumnusuru, Ghailani anayetuhumiwa kuhusika na visa 286 vya uhalifu, ikiwa ni pamoja na njama ya kutaka kuwauwa Wamarekani alikuwepo katika ukumbi wa mahakama akiwa amevalia shati ya rangi ya buluu na tai ya rangi hiyo hiyo.

Baada ya kusikilizwa hoja za pande zote mbili, jopo la majaji linaloongozwa na Jaji Lewis Kaplan jopo la majaji limeanza kushauriana kuhusu mwenendo wa kesi hiyo

No comments:

Post a Comment