KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Thursday, December 30, 2010

Serikali yatahadharisha kuhusu njaa


WANANCHI wametakiwa kujiwekea akiba ya chakula cha kutosha, ili kujihami juu ya uwezekano wa nchi kukumbwa na uhaba wa mvua.
Wito huo ulitolewa jana Katibu Mkuu katika Ofisi ya Waziri Mkuu Paniel Lyimo, kufuatia utabiri uliotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini, juu ya uwezekano wa kukumbwa na uhaba wa mvua.

Alisema uhaba wa mvua unaojulikana kama La-Nina, unatarajia kuikumba nchi kwa kipindi cha kuanzia Disemba mwaka huu hadi Januari mwakani na huenda ukaendelea zaidi.

"Kwa kuwa mvua zinahofiwa kuwa kidogo na zisizo na mtawanyiko, ni vema wakulima wakazingatia ushauri wa maofisa ugani, kilimo kuhusu mazao ya kupanda," alisema Lyimo.

Katibu mkuu huyo aliitaka mikoa, wilaya na halmashauri kutekeleza mipango mbadala katika maeneo yatakayobainika kuwa na uwezekano wa kukumbwa na mafuriko na kuathiriwa na mmomonyoko wa ardhi.
Kwa mujibu wa Lyimo mipango hiyo ni pamoja na kuwahamisha wananchi kuondoka katika maeneo hayo na kwenda sehemu salama.

Hali kadhalika, kurejesha mawasiliano kama yataharibika.
Pia aliitaka mikoa, wilaya na halmashauri kuhakikisha kuwa kuna kuwa na dawa muhimu za magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu na dawa za kusafishia maji ya kunywa.

Hatua nyingine ni kuchimba na kukamilisha uchimbaji wa mabwawa ya kuvunia maji ya mvua na kuainisha mitaro inayoweza kuingiza maji katika migodi ya wachimbaji wadogo wadogo.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa, maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka yanatarajiwa kuwa makavu ifikapo Januari mwakani na vipindi vya mvua kubwa zenye kuleta madhara kama mafuriko vinaweza kutokea.
Mamlaka hiyo pia ilisema hali hiyo inaweza kutokea katika maeneo mengine yasiyopata mvua mara mbili kwa mwaka hapa nchini

No comments:

Post a Comment