KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Thursday, December 30, 2010

CHADEMA Yaipiga Mwereka CCM Kigoma



Chama cha Mapinduzi CCM mkoani Kigoma kimeshindwa kuwashawishi madiwani wa vyama vya upinzani kumchagua mgombea wake wa nafasi ya Umeya na Makamu Meya wa manispaa ya Kigoma Ujiji na hivyo nafasi hiyo kuchukuliwa na Chama cha CHADEMA.
Katika uchaguzi huo uliofanyika Disemba 31, 2010 mjini Kigoma, ambao uligubikwa na ushabiki mkubwa wa kisiasa kutoka kwa wanachama wa vyama vya CCM na CHADEMA, Diwani wa kata ya Rusimbi kwa tiketi ya Chama cha Demokrasi na Maendeleo (CHADEMA) Bw. Beji Bakari alichaguliwa kuwa Meya wa Manispaa hiyo.

Katika uchaguzi huo uliofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa manispaa, Beji alichaguliwa kwa kupata kura 15 dhidi ya kura 12 za mpinzani wake John Mutabirwa wa CCM ambapo kura moja iliharibika.

Nafasi ya Makamu Meya wa manispaa hiyo pia ilichukuliwa na Yunus Luhovya wa CHADEMA aliyepata kura 15 na kumshinda Salum Akilimali wa CCM aliyepata kura 13.

Katika uchaguzi huo ambao ulihudhuriwa pia na Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA, Zitto Kabwe madiwani wa CHADEMA ambao walikuwa 15 waliweka msimamo wa kuhakikisha hakuna diwani wao hata mmoja anayesaliti kambi ya upinzani na kumchagua mgombea wa CCM ambapo kambi hiyo ina wapiga kura 15 dhidi ya 13 wa CCM.

Akitoa hotuba baada ya kupewa nafasi ya kutoa shukrani kwa madiwani, Meya mpya wa manispaa ya Kigoma Ujiji, Beji Bakari aliwaambia madiwani hao kumaliza masuala yao ya kiitakadi na sasa kuungana kuwa kitu kimoja na kufanya kazi kama timu ya kuwaletea wananchi maendeleo.

Aidha Meya huyo alisema kuwa hatakubali visingizio vya watendaji kuhusu kuzembea kutekelezwa kwa maagizo ya baraza la madiwani sambamba na kutokuwa tayari kuvumilia kitendo cha wataalam kufanya kazi chini ya kiwango kutokana na utaalam mdogo au kuzembea makusudi kwa nia ya kurudisha nyuma maendeleo.

Beji alisema kuwa jambo la kwanza kwa sasa ambalo litafanyika ni kuanisha na kutekeleza ahadi zilizokuwa zikitolewa na madiwani wakati wa uchaguzi bila kujali itikadi zao za kisiasa na ameonya kuendelea kuwepo na mivutano ya kisiasa miongoni mwa madiwani.

No comments:

Post a Comment