KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Tuesday, December 14, 2010

Raia wa kigeni kortini kwa cocaine za Sh 930milioni


Hadija Jumanne na Shakila Nyerere
RAIA sita kutoka Uganda, Guinea na Liberia wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala kujibu shitaka la kukutwa na dawa za kulevya aina ya cocaine zenye thamani ya Sh 930 milioni.

Watuhumiwa hao wanadaiwa kukamatwa na hati za kusafiria zikionyeshwa kuwa ni mabalozi wa kutoka nchini ya Guinea ambao wanafanya kazi hapa nchini katika Ubalozi wa Guinea wakati wakijua kuwa sio kweli.
Washtakiwa hao ni Diaka Koba(52) kutoka Guinea, Ndjano Abubakar(50) kutoka Liberia na raia wanne kutoka Uganda ambao ni Sylivia Namombe(34), Faridi Kisulile(26), Rehirson Teise (32) na Ismael Mugali.

Mwendesha mashtaka Daniel Buma alidai mahakamani kuwa watuhumiwa kwa pamoja walikamatwa Juni 23, mwaka huu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere wakiwa na kilo 31 za dawa ya kulenya aina ya cocaine.
Alidai kuwa siku ya tukio, majira ya saa 1:00 usiku katika uwanja huo walikutwa na dawa hizo zikiwa katika mabegi.

Aliendelea kudai mahakamani hapo kuwa watuhumiwa hao walikamatwa wakati wakisafirisha dawa hizo kutoka nchini Brazil kuzileta nchini.
Alidai kuwa wakati wakiwa katika uwanja huo maofisa wa polisi wa uwanja huo waliwashtukia watuhumiwa hao na walipowakagua ndio wakagundulika kuwa na dawa hizo za kulevya.

Buma aliendelea kudai kuwa watuhumiwa walipopekuliwa katika mabegi yao walikutwa pia na vitambulisho vya Ubalozi wa Guinea, hati ya kusafiria zikionyeshwa kuwa watuhumiwa hao ni mabalozi wa Guinea wakifanya kazi hapa nchini katika ubalozi wa Guinea wakati sio kweli.

Hata hivyo kwa upande wa wakili wa washtakiwa Steven Urasa na Msetu walidai kuwa kesi inayowakabili wateja wao ni kesi ya kusingiziwa kwani washtakiwa wa kwanza na wa pili walikamatiwa Uwanja wa Ndege wa Kilimanjaro na sio Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere kama hati ya mashtaka ilivyoeleza.

Hata hivyo iliendelea kudaiwa mahakamani hapo kuwa kesi hiyo ni ya muda mrefu na pia hati za mashtaka za washtakiwa zimekosewa hivyo waliiomba mahakama ifute kesi hiyo kwa kuwa hati za mashtaka zimekosewa.

Hata hivyo watuhumiwa hao hawakutakiwa kusema chochote mahakamani hapo kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza kesi hiyo na Hakimu Ester Mwakalinga aliahirisha hadi Januari 5, mwakani itakapotajwa tena.

Washtakiwa walirudishwa rumande kutokana na shtaka linalowakabili kutokuwa na dhamana na upelelezi bado haujakamilika

No comments:

Post a Comment