KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Tuesday, December 14, 2010

Maelfu wakimbia Ivory Coast

Umoja wa Mataifa (UN) umesema takriban watu 14,000 wamekimbia kutoka Ivory Coast na kukimbilia nchi jirani ya Liberia, kufuatia mtafaruku unaotokana na uchaguzi wa urais wa mwezi uliopita.

Ouattara anayetambulika kimataifa kuwa mshindi


Msemaji wa umoja huo ameiambia BBC kuwa UN inajiandaa kupokea wakimbizi 30,000 katika eneo hilo.

Wengi wanaokimbia ni wafuasi wa Alassane Ouattara, ambaye anatambulika kimataifa kama mshindi halali wa urais.

Ghasia

Rais anayetetea kiti chake, Laurent Gbagbo, ametupilia mbali wito wa kuondoka madarakani, akidai ulifanyika wizi wa kura upande wa kaskazini wa nchi.

Wanajeshi wa UN Abidjan

Msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR), Fatoumata Lejeune-Kaba, amesema wengi wa walioondoka Ivory Coast tangu baada ya uchaguzi wa Novemba 28, wametokea katika vijiji upande wa magharibi mwa nchi.

Amesema watu hao wamekuwa wakitembea kwa siku kadhaa kukimbia mvutano uliopo, huku wakihofia huenda ghasia zikazuka. Amesema watu wanazidi kuongezeka.




Alassane Ouattara

Bw Gbagbo ametaka majeshi ya Umoja wa Mataifa na ya Ufaransa kuondoka nchini humo. Mshirika wa karibu wa Bw Gbagbo alidiriki hata kuonya kuwa, wanajeshi hao watachukuliwa kama waasi iwapo hawatotekeleza amri ya kuondoka.

Umoja wa Mataifa ambao una wanajeshi 10,000 wa kulinda amani, umetupilia mbali wito huo.

Kuimarisha kikosi

Maafisa wa UN wanasema watu wasiopungua 170 wameuawa katika ghasia za hivi karibuni zinazohusishwa na majeshi ya Ivory Coast, ambayo yanamtii Bw Gbagbo waziwazi.

Kumekuwa na mapendekezo kuwa nchi wanachama zipeleke wanajeshi zaidi kuimarisha kikosi cha kulinda usalama cha Umoja wa Mataifa.

Uchaguzi wa Ivory Coast ulikuwa na lengo la kuiunganisha nchi hiyo baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, ambavyo viliigawanya nchi hiyo inayozalisha kakao kwa wingi duniani, huku Waisilam upande wa kaskazini wakimuunga mkono Bw Ouattara, na Wakristo upande wa kusini wakimuunga mkono Bw Gbagbo.

No comments:

Post a Comment