KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Amazon MP3 Clips

Wednesday, December 15, 2010

Nahodha ataka wakazi haramu kukaa chonjo


Exuper Kachenje SERIKALI imesema itawafuatilia mahotelini wageni ambao vibali vyao vimeisha ili kuwakumbusha kurejea makwao, zoezi ambalo litaenda sambamba na kuwasaka wakazi haramu na wanaofanya kazi bila ya vibali. Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha alisema hayo wakati alipokutana na watendaji wa Idara ya Uhamiaji kwenye ofisi za makao makuu ya wizara hiyo jana.

“Idara ya Uhamiaji itahakikisha kuwa wageni wote wanaoingia nchini wanakuwa na vibali halali. Wale ambao muda wa vibali vyao umekwisha wanaondoka muda unaotakiwa,” alisema Nahodha. Alifafanua kuwa maafisa uhamiaji watakuwa wakifika kwenye hoteli walizofikia na kuwakumbusha wageni kuwa muda wa vibali vyao vya kuwepo nchini umekwisha na kutetea kitendo hicho akisema kuwa si cha unyanyasaji bali na kwamba hata nchi za barani Ulaya hutumia utaratibu huo. “Katika nchi hasa za Ulaya, utakuta kama wewe ni mgeni umefikia hotelini na kibali chako kimebakiza siku moja, maafisa wa Uhamiaji wanakuja kukutaarifu mapema kuwa umebakiza siku mkoja kuondoka.

Huu sio unyanyasaji bali ni utekelezaji wa sheria za nchi,” alisema Nahodha. Aliongeza kuwa katika siku za karibuni kumekuwa na malalamiko kuwa baadhi watu wanaongia nchini kwa vibali vya uwekezaji, wamekuwa wakijishughulisha na biashara ndogondogo badala ya kuwekeza kama maombi yao yalivyo. Waziri Nahodha aliagiza suala hilo kushughulikiwa kikamilifu ili kuondokana na malalamiko ya wananchi. Waziri Nahodha alisema kuwa wizara yake itashirikiana na Wizara ya Kazi na Ajira pamoja na Tume ya Uwekezaji kufuatilia wageni walioomba vibali vya uwekezaji na kuvitumia kinyume kwa kufanya biashara ndogondogo zinazoweza kufanywa na wananchi.

Waziri Nahodha pia alisema wakimbizi wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu watafuatiliwa na kuchukuliwa hatua stahili. Waziri kiongozi huyo wa zamani wa Zanzibar aliwataka wananchi kushirikiana na wizara yake kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kuwatambua wageni wa aina hiyo na wale wanaoishi nchini kinyume cha sheria ili wachukuliwe hatua zinazostahili.

Waziri Nahodha pia alitembelea Idara ya Vitambulisho vya Taifa ambako alihimiza uharakishaji wa mradi wa vitambulisho vya taifa ambao umekuwa ukisuasua kwa muda mrefu sasa. Kesho Nahodha ataendelea na ziara katika Idara za wizara yake atakapotembelea Idara ya Magereza katika Gereza la Keko, Ukonga, Segerea ambapo pia atatembelea Chuo cha Maafisa Magereza Ukonga na Kikosi Maalum cha Kutuliza Ghasia

No comments:

Post a Comment