KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Friday, December 10, 2010

Mkulo: Kilichoenda kwa wahisani si bajeti


Raymond Kaminyoge
SIKU tatu baada ya Kundi la nchi wahisani wa maendeleo ambalo zinachangia kwenye bajeti ya Tanzania (GBS) kuibua kashfa kuwa Serikali iliwapelekea bajeti tofauti na iliyopitishwa na Bunge, Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustapha Mkulo, ameibuka na kusema kilichokua kimepekwa kwao ni makadirio.

Alisema bajeti iliyowasilishwa kwa Shirika la Fedha Duniani (IMF) yalikuwa makadirio ambayo yalibadilishwa katika mchakato wa kuiandaa na kwamba bajeti iliyopitishwa na Bunge ndiyo inayotambulika.

Mkulo alisema hayo jana jijini Dar es Salaam mara baada ya kumalizika mkutano wa kitaifa wa mwaka wa majadiliano ya kisera na bajeti.

“Kuna mchakato mrefu wakati wa kuandaa bajeti, tuliwapa makadirio ya bajeti yetu mwezi Aprili mwaka huu, baada ya hapo bajeti ilipitia kwenye Baraza la Mawaziri ambalo lilifanya marekebisho. Katika kipindi hicho kuna marekebisho yalifanywa hivyo kutofautiana na makadirio tuliyowapelekea wahisani,” alisema Mkulo na kuongeza:

“Ndiyo maana nasema sijawahi kupeleka kwa wahisani bajeti tofauti na iliyopelekwa bungeni. Nasisitiza kuwa bajeti ni moja tu ambayo ndiyo hiyo niliyowasilisha bungeni baada ya kuidhinishwa na Baraza la Mawaziri,” alisema.

Alisema ni utaratibu wa kawaida wahisani kupelekewa makadirio mapema, lakini mambo hubadilika kutokana na gharama eza kuendesha Serikali kubadilika”.

“Msidhani Mkulo ndiye anayeandaa bajeti pekee yake, Baraza la Mawaziri ndilo lenye kauli ya mwisho kuhusu bajeti ya nchi, wanaweza kubadilisha chochote wakati wahisani mlishawapelekea bajeti yenu mapema,” alisema Mkulo.

Jumatatu wiki hii, Mwenyekiti wa kundi la wahisani wa maendeleo ambalo linachangia kwenye bajeti kuu ya Tanzania (GBS), Svein Baera, katika hotuba yake ambayo Mwananchi ina nakala, alisema serikali ilipeleka IMF, bajeti tofauti na iliyopitishwa na Bunge.

Taarifa hiyo ilitolewa huku wahisani hao wakiwa wamezuia theluthi moja ya zaidi ya dola za Marekani 800 milioni ambazo zinatakiwa zichangiwe na wahisani kwenye Bajeti Kuu ya 2010/11, wakiishinikiza Serikali iharakishe utekelezaji wa programu ya mageuzi, yakiwemo ya mfumo wa usimamizi wa fedha za umma.


Baera alibainisha maeneo sita kuwa ndiyo mhimili wa mjadala wao na serikali.
"Napenda kuainisha maeneo sita ya ujumbe wetu ili kuweka sawa jukwaa la majadiliano yetu haya ya mwaka. Kuna tofauti kati ya bajeti iliyowasilishwa kwa bodi ya (Shirika la Kimataifa la Fedha) IMF na ile iliyopitishwa na Bunge Julai 2010," alisema Baera.

Alisema bajeti ambayo serikali iliwasilisha kwa wahisani hao ilibeba matumaini makubwa ya kuzaa matokeo mazuri na kufanywa kama sababu ya kupitisha matumizi makubwa ya fedha zinazotokana na mapato ya ndani".

Baera alisema kukosekana kwa uwazi katika matumizi, vipaumbele, mapato na mfumo mzima wa fedha kunapunguza kuaminika kwa bajeti hiyo mbele ya wafadhili

No comments:

Post a Comment