KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Amazon MP3 Clips

Friday, December 10, 2010

Saddam Hussein Alikuwa Akitetemeka Siku Aliyonyongwa


Mtandao wa WikiLeaks umeendelea kutoboa siri za Marekani kwa kuelezea jinsi Saddam Hussein alivyokuwa akitetemeka kabla ya kunyongwa na jinsi maafisa wa Iraq walivyokuwa wakimtukana Saddam na kuchukua picha na video za kunyongwa kwake.
Kwa mujibu wa nyaraka mpya za siri za Marekani zilizowekwa hadharani na mtandao wa Wikileaks, Aliyekuwa rais wa Iraq, Saddam Hussein alikuwa akitetemeka kabla ya kupandishwa kwenye kitanzi disemba 30, mwaka 2006.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotumwa Marekani na aliyekuwa na balozi wa Marekani nchini Iraq, Zalmay Khalilzad kuhusiana na kunyongwa kwa Saddam Hussein, Saddam alionekana mwenye hasira na alikuwa akitetemeka kabla ya kunyongwa.

Taarifa hizo zilisema kuwa Saddam alipelekwa kwenye gereza alilonyongwa na helikopta ya jeshi la Marekani, jukwaa alilonyongewa lilijengwa na Marekani lakini utekekelezaji na usimamiaji wa kunyongwa kwake ulifanywa na serikali ya Iraq.

Saddam aliingizwa gereza hilo huku sura yake ikiwa imefunikwa kwa kitambaa huku mikono yake ikiwa imefungwa kwa nyuma.

Mikono yake ilifunguliwa na Saddam alisomewa mashtaka yake mbele ya watu 13 walioteuliwa na serikali ya Iraq.

Alipoulizwa kama anahofia kufariki, Saddam alijibu "Sihofii kufariki, tangu nilipochaguliwa kuwa Rais nilijua kuwa marais huwa wana maadui wengi".

Baada ya kusomewa mashtaka yake, Saddam alimkabidhi msahafu aliokuwa akiusoma naibu Mwanasheria mkuu wa Iraq, Monqith al-Faroun na kumwomba aukabidhi kwa faimilia yake, al-Faroun aliahidi kuukabidhi kwa familia yake.

Saddam alifungwa tena mikono yake kwa nyuma huku miguu yake ikifungwa minyororo. Saddam alipandishwa kwenye jukwaa tayari kwa kunyongwa, alipokuwa akipanda kwenye jukwaa mmoja wa walinzi alisikika akisema "Nenda Motoni" na kumfanya al-Faroun awaonye watu kuwa hakuna mtu mwenye haki ya kusema chochote.

Saddam alisali sala yake ya mwisho huku baadhi ya maafisa wa Iraq wakipiga kelele za "Moqtada, Moqtada, Moqtada" wakiashiria jina la kiongozi wa Shia, Moqtada al-Sadr aliyepata umaarufu baada ya kuanguka kwa Saddam.

Saddam alikataa kuvalishwa kitambaa cheusi kwenye sura yake na alifariki ndani ya muda mfupi baada ya shimo chini ya kitanzi kufunguka na kuufanya mwili wa Saddam uning'inie.

Mwili wa Saddam ulihifadhiwa na baadae ulioshwa na kuzikwa kwa misngi ya kiislamu.

Al-Faroun alielezea jinsi alivyoshuhudia maafisa wa Iraq wakipiga picha na kuchukua video za tukio hilo kwa kutumia simu zao ingawa ilikuwa ni marufuku kuingia na simu kwenye eneo hilo.

Picha na Video za kunyongwa kwa Saddam ziliingizwa kwenye internet na kusababisha mjadala mkubwa kuhusiana na jinsi Saddam alivyonyongwa.

Mtandao wa WikiLeaks ulimalizia kwa kusema kuwa serikali ya Iraq ililaumiwa kwa kuruhusu kuvuja kwa picha na video za tukio hilo

No comments:

Post a Comment