KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Thursday, December 2, 2010

MGAWO WA UMEME: Mbunge apania kufa na Ngeleja


Ramadhan Semtawa
KERO isiyokwisha ya mgawo wa umeme nchini, sasa itashughulikiwa kwa mtindo tofauti ndani ya Bunge la Muungano baada ya mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila kutangaza kuwa atawasilisha hoja binafsi akitaka serikali iwajibike kwa Waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja kuachia ngazi.

Tanesco, ambayo pia wiki iliyopita ilikumbana na hukumu inayoitaka ilipe fidia ya takriban Sh185 bilioni kwa kampuni ya Dowans kutokana na kukatisha mkataba wake wa kuzalisha umeme mwaka 2008, imetangaza mgawo wa umeme karibu nchi nzima ikidai kuwa mitambo inayozalisha nishati hiyo kwenye baadhi ya mabwawa imeharibika na kwamba kina cha maji kimepungua.

Pamoja na kueleza sababu za kutokea kwa mgao huo, Tanesco haijaweka bayana muda ambao tatizo hilo litaisha.
Kero hiyo imemfanya mbunge huyo wa NCCR-Mageuzi kuamua kutumia jukwaa la muhimili huo wa nchi kutaka Waziri Ngeleja, ambaye wizara yake inahusika na uzalishaji na usambazaji wa nishati hiyo kuwajibishwa.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana huku akitumia takwimu zinazoonyesha athari za umeme tangu mwaka 2006, Kafulila alisema: "Kwa kuwa taifa linaingia hasara kubwa ya mabilioni ya fedha kutokana na udhaifu wa serikali kusimamia mpango mzima wa nishati, nakusudia kupeleka hoja binafsi kwenye Bunge la Februari."

"Hoja itakuwa kwanini serikali isiwajibike kwa kuliingiza taifa katika hasara kubwa kwenye sekta ya umeme?

Pamoja na mambo mengine na vilevile kama Bunge litaona inafaa, nitalitaka liazimie kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri wa Nishati na Madini kwa kushindwa kusimamia utekelezaji wa Sera ya Nishati na Mpango kabambe wa usambazaji umeme (Power System Master Plan). "

Mbunge huyo mpya na kijana alisisitiza azma yake akidai udhaifu huo wa kiutendaji wa Waziri Ngeleja umechangia nchi kuathirika kiuchumi huku mipango mingi ya maendeleo ikisimama na "hivyo kusimamia migawo mitatu ya umeme ndani ya miaka miwili ya uongozi wake".

Alifafanua kwamba Tanesco imekuwa ikitoa ushauri wa kitaalamu, lakini wanasiasa wamekuwa wakishindwa kuheshimu ushauri huo badala yake kuamua mipango yao ambayo mwisho wa siku athari zake huumiza Watanzania.

"Serikali ione suala la mgawo wa umeme linaathiri maendeleo kuliko hata mtikisiko wa uchumi, hivyo ifanye maazimio magumu kwa kutenga fedha za kutosha kutekeleza miradi mikubwa ya umeme wa uhakika, kwa mfano Stigler's Gorge," alisema mbunge huyo anayetazamiwa kuwa miongoni mwa watunga sheria machachari.

Kafulila alihoji mantiki ya wizara hiyo kutoendeleza vyanzo vya uhakika kama mradi wa uzalishaji umeme kwa kutumia makaa ya mawe wa Kiwira ambao una uwezo wa kuzalisha megawati 200 na Mnazi Bay (megawati 300) na badala yake imebaki kusimamia mipango aliyoiita ya kudunduliza kama ya mitambo ya kukodi ambayo huliingiza taifa kwenye hasara kubwa.

Mtendaji huyo wa kambi ndogo ya upinzani bungeni, aliongeza kwamba Wizara ya Nishati na Madini ilipaswa kutafuta fedha kutoka mifuko ya hifadhi ya jamii ili iwekeze zaidi katika miradi ya uhakika na endelevu ya umeme kuliko kujikita kwenye ujenzi wa majengo ya biashara.

Aliweka bayana kwamba, Shirikisho la Wenye Viwanda nchini (CTI) limekuwa likitaja athari ambazo zinachingia hasara ya uzalishaji kutokana na mgawo wa umeme, lakini mamlaka husika hazionyeshi kustushwa na hali hiyo.

"Imekuwa ikitolewa mifano ya viwanda vya simenti ambavyo vinaeleza kuwa mgawo wa umeme unaongeza gharama zaa uzalishaji kwa kiwango cha dola 10 za Kimarekani kwa kila mfuko wa kilo 50, hivyo kuongeza gharama, kupata hasara na kushindwa kulipa kodi serikalini," alifafanua.

Kafulila pia alisema mgawo wa umeme huathiri zaidi pia watu wa kipato cha kati ambao hujitengenezea kipato kutokana na saluni za nywele.

"Gharama za uzalishaji zinaongezeka; vijana wanaojishughulisha na kunyoa nywele jijini Dar es Salaam hupoteza zaidi ya asilimia 45 ya mapato yao kutokana na kutumia majenereta ili kupata umeme wa kuendelea kutoa huduma kwa wateja wao, " alifongeza akinukuu taarifa ya utengenezaji ajira ya mwaka 2010, kutoka taasisi ya Repoa.

Hata hivyo, Ngeleja alipoulizwa kuhusu kauli yake ya siku ya kiapo kwamba mgawo wa umeme utakuwa ni hadithi, alijibu kuwa "ipo mipango ambayo ikitekelezwa ndio mgawo utakuwa hadithi".

Alipoulizwa tena kama mipango hiyo isipotimia atakuwa tayari kujiuzulu, Ngeleja alisita kukubali kujiuzulu

No comments:

Post a Comment