KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Thursday, December 2, 2010

Mkapa ataka vyuo vikuu kuepuka ufisadi


Raisa Said, Lushoto
RAIS mstaafu wa serikali ya awamu ya tatu, Benjamin Mkapa amewataka wanafunzi wa vyuo vikuu kuzingatia dhana ya uwazi, ukweli na uaminifu ili kuepuka vishawishi vya kutumia ujuzi wao kujipatia kipato kwa njia zisizokubalika kimaadili na kitaaluma.

Akizungumza katika mahafali ya kwanza ya Chuo Kikuu kishiriki cha Sebastian Kolowa (SEKUCo) mwishoni mwa wiki, Mkapa ambaye katika utawala wake alisisitiza juu ya dhana ya uwazi, ukweli na uaminifu aliwataka wahitimu hao kuacha kutumia njia za mkato zinazowasababisha kuwa mafisadi.

Jumla ya wahitimu 132, wakiwemo wanaume 75 na wanawake 57 walitunukiwa shahada ya kwanza ya elimu maalum.

Alisema ufumbuzi wa matatizo na mafanikio ya maisha ni kujifunza utamaduni na kujiwekea malengo ya kila mwezi na hata kwa mwaka.

“Ukishajiwekea malengo na kuyapanga kwa uzito kwa kulingana na umuhimu wake, muda, fedha au rasilimali ulizonazo utaona mafanikio mazuri zaidi kazini kwako na kwa maendeleo yako wewe na jamii nzima ya Watanzania,” alieleza Mkapa.

Mkapa alisisitiza kuwa wataalamu, hasa wa elimu maalumu sharti wawe mfano bora wa kuigwa na jamii ya Watanzania na popote watakapokuwa.

“Utumishi bora unadai mjiepushe na kauli ya ‘njoo kesho’. Nendeni mkawe mabalozi wazuri wa chuo hiki,” alisisitiza.

Akizungumzia juu ya kuongezeka kwa mahitaji ya elimu ya juu katika soko la ajira kutokana na mabadiliko makubwa yanayoendelea duniani, yakiwemo maendeleo ya sayansi na teknolojia, alikipongeza chuo hicho kwa kujiandaa vema katika mwelekeo wa kutoa elimu katika fani mbalimbali ikiwemo fani ya teknolojia ya habari kwa lengo la kukidhi mahitaji ya soko la ajira na kutoa huduma bora kwa jamii katika mazingira mapya ya kiuchumi, soko huru, mabadiliko makubwa ya teknolojia na utandawazi.

Alitoa rai kwa wadau wote wa elimu nchini na duniani kote kuendelea kuunga mkono na kusaidia kwa dhati juhudi zinazofanywa na chuo hicho kutoa elimu yake. Chuo hicho ni chuo kishiiriki Chuo Kikuu cha Tumaini.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Tumaini, Profesa John Shao aliwataka wahitimu kutoridhika na taaluma waliyo nayo na kuwataka kujua kuwa uaminifu na uadilifu katika kazi ni moja wa vigezo vitakavyowafanya wathaminiwe sehemu watakazofanya kazi.

Pia aliwataka kuwa tayari kutumika na kuishi na kufundisha maadili mema na kukabiliana na tamaa ya ufisadi, kuendelea kwa ugonjwa wa ukimwi na mwenendo wa kutopenda kufanya kazi kwa moyo na ubunifu.

Chuo cha SEKUCo kilianzishwa mwaka 2007 na ni chuo pekee ambacho kimeanzishwa na kuendesha mafunzo ya elimu maalum

No comments:

Post a Comment