KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Thursday, December 2, 2010

Gaddafi aagiza waandishi 19 waachiwe


TRIPOLI, Libya

KUNDI la waandishi wa habari 19 nchini Libya waliokamatwa mwanzoni mwa wiki limeachiwa huru kwaamri ya kiongozi mkuu wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi.

Mamlaka nchini humo ziliwakamata waandishi hao 19 wa habari na mmoja wa viongozi wa juu wa chombo kimoja cha habari kwa kile kilichoelezwa kwamba inatokana na mvutano wa kimadaraka katika serikali ya Libya.

Waandishi hao wa habari ni wafanyakazi wa shirika la Libya Press News Agency lililoanzishwa na mtoto wa kiume wa Gaddafi, Saif al-Islam ambaye anaonekana mwanamageuzi msomi anayepambana na viongozi wenye msimamo mkali nchini humo.

Katika tangazo la awali la kukamatwa kwao, shirika la habari la Libya, Jana lilieleza kwamba Gaddafi alichukua fursa ya kuzungumza na wanausalama kwa niaba ya waandishi hao.

“Shirika la Habari la Libya, Jana limebaini usiku uliopita kwamba kiongozi wa mapinduzi, Gaddafi ametoa maelekezo ya kuagiza kuachiwa kwa waandishi hao wa kituo cha Libya Press na kuagiza uchunguzi wa kina ufanyike kuhusu tukio hilo,” lilieleza shirika hilo la habari.

Waandishi hao wanatoka katika nchi mbalimbali ikiwemo Libya, Misri na Tunisia na walikamatwa na vyombo vya usalama mjini Tripoli mwanzoni mwa wiki hii.

Naibu mkuu wa kampuni ya habari ya al-Ghad inayomiliki shirika hulo la habari na vyombo vingine kadhaa vya habari, Fawzi Ben-Tamer alisema walipata matunzo mazuri na hakuna mashtaka yoyote rasmi yaliyofunguliwa dhidi yao.

Alisema kwa muda wote walikuwa katika ofisi za idara ya uongozi katika jingo la usalama wa ndani na walipewa magodoro waliyolalia kwa kuyatandika sakafuni, chakula cha kutosha na vinywaji.

Kila mmoja alihijiwa na kutoa maelezo binafsi ambapo Ben-Tamer alisema maswali mengi yalihusu namna wanavyoendesha kazi zao na utaratibu unaotumika katika kutafuta taarifa na habari

No comments:

Post a Comment