KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Thursday, December 2, 2010

Magufuli amfukuza mkurugenzi Tanroads



WAZIRI wa Ujenzi, John Magufuli, amemfukuza kazi Mtendaji Mkuu Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Bw. Ephraim Mrema.


Uamuzi huo ulifanywa na Waziri huyo jana na kutoa maamuzi hayo juu ya mkurugenzi huyo na kudaiwa kutakiwa kuacha mamlaka hayo mara moja.

Hivyo Dk. Magufuli alimtaka Mrema kukabidhi ofisi hiyo jana mchana na kwa aliyekuwa Mkurugenzi wa Barabara za Vijijini, Bw. Patrick Mfugale.

Kwa habari za kina kuhusiana na maamuzi haya yatawajia



UFISADI TANROADS; Ephraem Mrema nDIYE kINARA
MKURUGENZI Mkuu wa Wakala wa Barabara (Tanroads), Ephraem Mrema ameumbuliwa bungeni, kuwa amepewa wadhifa huo kinyume cha taratibu.

Mbunge wa Kasulu Magharibi, Kilontsi Mporogomyi (CCM) alisema Mrema hana taaluma ya uhandisi ujenzi, huku analipwa mamilioni ya fedha za Watanzania.

Mporogomyi ndiye aliyeweka hadharani habari za Mkurugenzi huyo kuingizwa kwenye madaraka hayo kupitia mlango wa nyuma; huku wataalamu ambao walipendekezwa na jopo la usaili wakiwekwa pembeni.

“Ninavyojua huyu Mrema hakuwa amependekezwa na jopo la usaili, hatujui alikotokea hadi akawekwa pale…naomba waziri useme juu ya ajira ya mkurugenzi huyu,” alisema wakati akichangia katika hotuba ya Waziri wa Maendeleo ya Miundombinu, Dk. Shukuru Kawambwa.

Mporogomyi aliliambia Bunge kuwa sifa za mkurugenzi huyo ni kwamba ni mshauri wa mambo ya ununuzi na kabla ya kushika wadhifa huo, alikuwa anafanya shughuli zake visiwani Zanzibar.

Hata hivyo, Mrema mwenyewe alijitetea kuwa ana shahada ya kwanza ya ukandarasi uchumi (Construction Economics) na shahada ya pili ya Menejimenti ya miradi (Project Management) aliyoipata mwaka 1987. Hata hivyo, hakutaja vyuo alikopata shahada hizo.

Aliwataja wahandisi ambao walipendekezwa na jopo la usaili kuwa ni Boniface Nyiti, Venance Ndyamkama na mwingine aliyemtaja kwa jina la moja la Chacha. “Hawa ndiyo ambao walipendekezwa na ni wahandisi wa siku nyingi pale Tanroads; lakini huyu mkurugenzi alikotolewa na kuwekwa pale haijulikani.”

Mrema alichukua wadhifa wa mkurugenzi aliyekuwa anatokea Ghana ambaye alimaliza muda wake mwaka 2006. Mporogomyi alisema mkurugenzi wa sasa aliingizwa kwa misingi ya ufisadi.

Mbunge huyo aliongeza kuwa mara tu baada ya kupata wadhifa huo, alianza kuwanyanyasa wahandisi hao wenye sifa na akawahamishia wizarani ambako pia walirudishwa na wizara Tanroads. “Wizara ilisema hawa ni mawakala wa ujenzi wa barabara wakawarudisha.”

Alisema Wizara ya Maendeleo ya Miundombinu wakati inawarejesha kwa Tanroads, ilishauri wapewe mikoa ya kuongoza, lakini kuwa tayari nafasi hizo zilishajazwa na watu wengine Mrema hakuweza kutekeleza agizo hilo.

Alisema alibaki nao makao makuu na wanalipwa fedha nyingi huku wakiwa hawana kazi za kufanya. Alisema kuwa mkurugenzi huyo baada ya kuona wahandisi hao ni tishio katika ajira yake, sasa ameingiza utaratibu mpya wa ajira za mikataba.

Mporogomyi alisema mpango huo mpya unafanywa na mkurugenzi huyo kwa nia ya kuwaengua wafanyakazi wote ambao anaona kama ni tishio kwake, hasa wale wahandisi wenye sifa za kushika wadhifa wake huo.

“Kibaya zaidi pamoja na kuingia kwa mlango wa nyuma, lakini ananyanyasa wafanyakazi,” alisema mbunge huyo huku akimtaka Waziri wa Maendeleo ya Miundombinu amweleze namna mkurugenzi huyo alivyoingizwa kwenye nafasi hiyo nyeti na ikiwezekana aondolewe haraka.

Lakini pia alisema mkurugenzi huyo analipwa fedha nyingi kama vile ni mtaalamu ambaye ameajriwa kutoka nje ya nchi.

Aliweka hadharani viwango hivyo kuwa Mrema alipoanza kazi alipewa posho ya kuanza (Commencement allowance) dola za Marekani 9,000 kwa siku 60 (sawa na Sh milioni 10.8), mshahara wake kwa mwezi ni dola za Marekani 8,500 (Sh milioni 10.2), posho ya nyumba kwa mwezi ni dola 2,200 (Sh milioni 2.6), posho ya matibabu dola 400 kwa mwezi (Sh 480,000), posho ya usafiri dola 500 (Sh 600,000).

Pia analipwa pensheni kwa mwaka kiasi cha dola za Marekani 10,200 (Sh milioni 12.4), akienda likizo analipwa dola 3,000 (Sh milioni 3.6), bonasi yake kwa mwaka analipwa dola 102,000 (Sh milioni 122.4) na mwisho wa mkataba wake analipwa dola 10,000 (Sh milioni 12) kama malipo ya kumaliza kazi.

Mporogomyi alisema pamoja na fedha nyingi anazolipwa mkurugenzi huyo; lakini bado anajihusisha na vitendo vya ufisadi zinavyosababisha wakati mwingine awanyanyase na kuwafukuza wafanyakazi ambao wanatenda haki.

Mbunge huyo alitoa mfano kuwa kuna mfanyakazi aliyemtaja kwa jina moja la Mabuye ambaye alikuwa anafanya kazi katika mizani ya Kibaha. Alisema siku moja mfanyakazi huyo alikamata malori ambayo yalikuwa yamezidisha uzito wa bidhaa walizobeba.

Alisema aliyazuia na kuwataka walipe faini ya Sh milioni 18, lakini matajiri wa yale malori walipoambiwa kukamatwa kwa magari yao walimpigia simu na yeye akaamuru Mabuye afukuzwe kazi.

Mporogomyi alisema Mrema alimpigia simu meneja wa Tanroads mkoa wa Pwani ili amfukuze na aliposita alimtishia kwa simu kuwa afanye hivyo haraka, kwani hataki kumwona huyo mfanyakazi akiendelea na kazi.

“Kama siyo ufisadi hiki nini, yaani mfanyakazi ambaye anafanya kazi kwa misingi ya sheria unamfukuza kazi, sababu ni nini hapa? Alihoji mbunge huyo na kusisitiza kutaka maelezo ya kina kutoka kwa Waziri wa Miundombinu

No comments:

Post a Comment