KARIBU MAISHANI
KARIBU MAISHANI
Thursday, December 30, 2010
Tunakumbuka nini 2010?
Leo tunauanza mwaka mpya wa 2011, ikiwa ni jana tu tumeupa kisogo mwaka 2010. Mwaka jana ulikuwa na matukio mengi ya kukumbukwa kama taifa. Miongoni mwake yapo ambayo ni makubwa yaliyoadika historia katika taifa letu.
Rashid Kawawa afariki dunia
WATANZANIA waliuanza mwaka 2010 kwa majonzi kufuatia kifo cha aliyekuwa Mwanasiasa mkongwe nchini na mmoja wa watu waliokuwa mstari wa mbele katika kupigania uhuru wa Tanganyika, Mzee Rashidi Kawawa.
Kawawa alifariki dunia Disemba 31, 2009 saa 3:20 asubuhi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, ambapo siku hiyo hiyo Rais Jakaya Kikwete alitangaza rasmi kifo cha Mwasisi huyo wa taifa hili.
Ajali mbaya yaua 20 Handeni
Mwaka huu haukuandamwa ajali nyingi za barabarani, ingawa ile iliyotokea Februari 2, na kusababisha vifo vya watu 25 na wengine zaidi ya 52 kujeruhiwa haitosahaulika.
Kinachoifanya ajali hiyo kuwa na historia ya kipekee, ni kupona kwa mtoto wa miaka miwili aliyekuwa akisafiri na baba yake. Baba huyo alifariki dunia.
Ajali hiyo ilihusisha mabasi mabasi mawili ambayo ni Mzuri Transport, lililokuwa likitokea Dar es salaam kuelekea Lushoto na Chatco lililokuwa likitokea Arusha kuelekea Dar es salaam, kugongana uso kwa uso katika barabara ya Segera – Chalinze, Kijiji cha Kitumbi kilicho Handeni, Tanga.
Jerry Muro kizimbani
Februari 5, mtangazaji wa televisheni ya Shirika la Utangazaji (TBC1), Jerry Muro alipandishwa kizimbani akishtakiwa kwa kula njama na kuomba rushwa ya Sh10 milioni.
Muro ambaye ni mwandishi bora wa habari wa mwaka 2009, tuzo aliyoipata kutokana na kuripoti habari zilizofichua rushwa inayofanywa na askari wa kikosi cha usalama barabarani, alipandishwa kizimbani na wenzake wawili ambao inadaiwa alishirikiana nao kutenda kosa hilo.
Richmond kwaheri
Katika hali isiyotarajiwa na wengi, Februari 10, bunge lilifunga rasmi mjadala wa mkataba tata wa Kampuni ya Richmond Development (LLC) na Tanesco na kuacha serikali iendelee kutekeleza maazimio ya bunge. Wabunge wote walionekana kunywea isipokuwa wabunge wawili, Christopher Ole Sendeka (Simanjiro, CCM) na Dk Willbroad Slaa (Karatu, Chadema) waliokuwa na msimamo wa kutaka mjadala huo kutokufungwa bila wahusika wa kashfa hiyo kuwajibishwa.
Tofauti na ilivyokuwa kwenye mkutano wa 16 wa Bunge na viapo vya baadhi ya wabunge kutaka kufa na LLC, mjadala huo wa taarifa ya Serikali kuhusu utekelezaji wa maazimio ya LLC ulipooza, kinyume na ilivyotarajiwa.
Askofu Kakobe na Tanesco
Baada ya waumini kulinda majengo ya Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF) kwa takriban miezi mitatu, ili Tanesco waspitishe umeme wenye msongo wa 132KV juu ya eneo la kanisa hilo, serikali kupitia Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, Machi 17 mwaka huu alitoa tamko la serikali ambalo lilitaka shirika hilo la umeme kuendelea na kazi. Waumini wa kanisa hilo, waliitii amri ya serikali na kuacha zoezi la kupitisha nyaya kuendelea, lakini mpaka leo umeme huo haujawashwa.
Lori laua abiria wote
Machi 25 vilio, simanzi na majonzi vilitawala eneo la Kibamba Darajani jijini Dar es Salaam ambako watu kumi, walifariki dunia papo hapo baada ya lori la mafuta kuangukia daladala.
Lori hilo liliigonga daladala hiyo uso kwa uso na kuitumbukiza kwenye mtaro kisha kuiangukia juu yake. Kilichosikitisha sana katika ajali hii, ni mama mjamzito kupasuka tumbo. Alikuwa na mumewe aliyekuwa akimsindiza kwenda kliniki na wote walifariki papo hapo.
Mpendazoe ajiunga CCJ
Chama cha Jamii (CCJ) kikuja kwa kasi na watu kudhani kuwa kingebadilisha upepo wa siasa za Tanzania hasa kufuatia uvumi kuwa, vigogo ndani ya chama tawala, CCM wangejiunga nacho.
Joto lilipanda zaidi pale, aliyekuwa mbunge wa jimbo la Kishapu mkoani Shinyanga (CCM), Fred Mpendazoe alipojiunga na chama hicho, ambacho kabla ya uchaguzi mkuu Septemba mwaka 2010, kilishapukutika.
JK akataa kura za wafanyakazi
Mei 3, zikiwa zimebaki siku mbili kabla ya kufanyika mgomo wa wafanyakazi nchi nzima kama ulivyokuwa umeitishwa na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), Rais Jakaya Kikwete alikutana na wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam na kutoa hotuba kali akiwashutumu viongozi wa (Tucta) kuwa ni wanafiki kwa kuendelea kushinikiza mgomo wa wafanyakazi licha ya mazungumzo baina yao na Serikali.
Alifafanua kuwa kima cha chini cha mshahara cha Sh315,000 kwa mwezi kinachopigiwa debe na Tucta, serikali haiwezi kukitekeleza na kama hilo ni shinikizo kwake ili wafanyakazi wampatie kura kwenye Uchaguzi Mkuu, hahitaji kura zao.
Liyumba jela miaka miwili
Amatus Liyumba mmoja wa vigogo Benki Kuu ya Tanzania (BOT), alihukumiwa kifungo cha miaka miwili jela baada ya kupatikana na hatia katika shtaka la kutumia madaraka vibaya wakati akiwa mtumishi wa umma.
Kwa mujibu wa kesi hiyo, Liyumba anadaiwa kutumia madaraka yake vibaya kwa kufanya mabadiliko katika mradi wa ujenzi wa majengo pacha ya BoT, na kusababisha ongezeko la gharama za mradi kutoka dola za Kimarekani 73.6 milioni hadi 357.6 milioni.
Bajeti ya 2010 ni Sh11.1 trilioni
Serikali ilitangaza bajeti ya Sh11.1 triloni kwa mwaka 2010/11, ambalo lilikuwa ni ongezeko la asilimia 16.8 ikilinganishwa na bajeti iliyotangulia.
Mahakama yafuta
mgombea binafsi
Baada ya watanzania kusubiri kwa muda mrefu, Juni 17 Mahakama ya Rufani lipigilia msumari wa mwisho katika jeneza la hoja ya kuwa na mgombea binafsi.
Awali kulikuwa na matarajio ya kuwepo kwa mgombea binafsi baada ya jopo la majaji saba wa Mahakama ya Rufani kumweka kiti moto mwanasheria wa serikali na kueleza bayana kuwa uamuzi wa Mahakama Kuu wa kuruhusu mgombea huyo utaendelea kusimama wakati rufaa hiyo ya serikali ikisikilizwa.
Lakini hali ilikuwa tofauti wakati Mahakama ya Rufani ilipotengua uamuzi wa Mahakama Kuu ambayo ilikuwa imeamua katika kesi iliyofunguliwa na Mchungaji Christopher Mtikila kuwa sheria inayozuia mgombea binafsi inakiuka katiba ya nchi.
Majaji watatu wa Mahakama Kuu, Amir Manento, Salum Massati na Thomas Mihayo walibatilisha sheria hiyo inayozuia mgombea binafsi katika hukumu yao ya Mei 5, 2006 na kuipa serikali miezi sita kuweka kifungu kinachoruhusu kuwepo kwa mgombea wa aina hiyo.
Ndege ya jeshi
yagonga gari, yaua
Wanajeshi wawili ambao ni marubani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) wa Kambi ya Ngerengere, walikufa baada ya ndege waliyokuwa wakisafiria kugongana na gari la watalii.
Ndege hiyo ndogo yenye namba F59119 iligongana na gari hilo eneo maarufu kwa jina la Zimbabwe katika Kijiji cha Manga, Kata ya Mkata wilayani Handeni.
Uchaguzi Mkuu
Oktoba 31, ulifanyika uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani. Upande wa Tanzania Visiwani pia walichagua Rais wa Visiwa hivyo, wajumbe wa baraza la wawakilishi nja masheha. Kubwa lililotoka na uchaguzi huu ni ongekezo la wabunge wa kambi ya upinzani ambapo Chadema wamefanikiwa kujenga uwezo wa kuunda kambi rasmi ya upinzani bungeni, CUF kupata wabunge wawili Tanzania Bara na NCCR Mageuzi kurejea bungeni kikiwa na wabunge watatu. Visiwani Zanzibar baada ya uchaguzi huo, imeundwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayovishirikisha vyama vya CCM na CUF, huku Seif Shariff Hamad akiteuliwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais.
Chadema wamsusia JK
Katika historia ya Tanzania, uchaguzi mkuu wa 2010 uliweka historia ikiwa ni pamoja vyama vya upinzani kuongeza wabunge bungeni. Chadema wao walitangaza kutotambua kura zilizomwingiza Rais Jakaya Kikwete madarakani pamoja na kudhihirisha hilo wabunge wa chama hicho waliandika historia baada ya kutoka kwenye ukumbi wa Bunge wakati Rais akianza kuhutubia kama ishara ya kuthibitisha msimamo wa chama chao.
Tanesco kuilipa Dowans
Sh185 bilioni
Shirika la Umeme nchini (Tanesco) liliamriwa kulipa fidia ya Sh106 bilioni kwa kampuni ya ufuaji umeme ya Dowans Tanzania Limited baada ya kuvunja mkataba.
Uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Biashara (ICC Court), Novemba 15, mwaka huu chini ya Mwenyekiti Gerald Aksen na wasuluhihi Swithin Munyantwali, Jonathan Parker uliamuru Tanesco iilipe Dowans kiasi hicho cha fidia.
Wahisani waiumbua serikali
Kundi la wahisani wa maendeleo ambalo linachangia kwenye bajeti kuu ya Tanzania (GBS) liliibua kashfa mpya baada ya kueleza kuwa serikali iliwapelekea bajeti tofauti na ile iliyopitishwa na Bunge Julai mwaka 2010.
Taarifa za kashfa hiyo ziliwekwa hadharani na mwenyekiti wa wahisani hao, Svein Baera wa Sweden katika mkutano wa kitaifa wa mwaka wa majadiliano ya kisera na bajeti uliofanyika jijini Dar es salaam.
Wikleaks, Dk Hoseah na siri za JK Mkurugenzu Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Dk Edward Hoseah, anadaiwa kufichua siri za Rais Jakaya Kikwete kwamba kiongozi huyo wa nchi asingependa vigogo serikalini kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za rushwa.
Kadhalika, mkuu huyo wa Takukuru anadaiwa kushindwa kuwafikisha mahakamani vigogo waliohusika na kashfa ya rada kwa sababu anahofia usalama wake, gazeti la The Guardian la Uingereza liliripoti.
Mbali na hofu hiyo, gazeti hilo pia lilieleza kuwa Dk Hoseah alipewa maelekezo maalumu na Rais Kikwete kutoshughulikia kesi za rushwa zinazowahusu vigogo katika serikali yake na hasa marais waliomtangulia.
The Guardian lilitoa taarifa hiyo likiunukuu mtandao wa habari wa WikiLeaks uliojizolea umaarufu duniani kwa kutoa habari za kiuchunguzi hasa baada ya mwasisi wake, Julian Paul Assange, kutiwa matatani.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment