KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Thursday, December 2, 2010

Chadema chamlima barua Zitto,wabunge tisa




Sadick Mtulya

SAKATA la wabunge wa Chadema kutoka nje ya ukumbi wa Bunge wakati Rais Jakaya Kikwete akihutubia, limechukua sura mpya baada ya chama hicho kuwaandikia barua wabunge ambao hawakushiriki akiwemo Zitto Kabwe, kuwataka waeleze sababu za kutoonekana.

Uamuzi huo umetolewa takribani siku 20, baada ya Chadema kudhihirisha msimamo wa kutotambua matokeo ya uchaguzi ya urais kwa kutoka nje ya ukumbi wa Bunge na kususia sherehe za kuapishwa kwa Mizengo Pinda kuwa Waziri Mkuu, katika hafla iliyofanyika Ikulu ndogo ya Chamwino mkoani Dodoma.

Akizungunza na Mwananchi jana, Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani bungeni, Tundu Lissu alisema wabunge 10 kati ya 13 ndio wanaotakiwa kujieleza na kwamba, hatua hiyo imefikiwa baada ya kwenda kinyume na maamuzi ya pamoja ya chama na kutotoa taarifa yoyote ya kutokuwepo kwao bungeni.

“Tunachotaka kujua kwa wabunge hawa kumi ni kwamba, kwa nini hawakuja katika kikao cha Bunge siku hiyo,’’ alifahamisha Lissu na kuongeza:
“ Hatua hii imefikiwa baada ya wabunge hao kwenda kinyume na maamuzi ya chama pamoja na kutotoa taarifa ya kutohudhuria kwao’’.

Hata hivyo, Lissu alisema bado hawajawakabidhi rasmi barua hizo, lakini zipo katika hatua ya mwisho na kwamba watakabidhiwa wakati wowote kuanzia sasa.

Aliwataja wabunge hao kuwa ni Zitto Kabwe (Kigoma Kaskazini) ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Said Arfi (Mpanda Mjini) ambaye ni Naibu Mwenyekiti Taifa wa chama hicho, Mhonga Luhwanya (Viti Maalum), Jonh Shibuda (Maswa Magharibi), Maulida Komu (Viti Maalum).

Wengine ni Profesa Kulikoyele Kahingi,(Bukombe), Rachel Mashishanga(Viti Maalum), Raya Ibrahimu(Viti Maalum), Lucy Owenya (Viti Maalum) na Suzan Lyimo(Viti Maalum).

“Lakini wabunge John Mnyika (Ubungo) na Halima Mdee (Kawe), walitoa udhuru kwamba walikuwa wanaumwa na Philemon Ndesamburo (Moshi Vijijini) alikuwa safarini. Hawa hawatapewa barua ya kujieleza, ’’ alisema Lissu.

Lissu ambaye pia ni Mkurugenzi wa Sheria na Haki za Binadamu wa Chadema, alifahamisha kuwa kitendo hicho kikiachwa bila kukemewa, ingeondoa umuhimu wa vikao vya chama na maamuzi.

Alipoliulizwa na gazeti hili jana, Zitto



alisema matatizo ya chama watayamaliza kwenye vikao na si katika vyombo vya habari na kwamba hakuna sababu ya kuendeleza maluimbano juu ya suala hilo wakati Watanzania wana matatizo mengi yanayohitaji kujadiliwa kwa kina ili yaweze kupatiwa ufumbuzi.

“Watanzania wana matatizo mengi ya kujadili. Kuna mgawo wa umeme, madai ya katiba mpya na kero ya maji, hakuna sababu ya kuendeleza malumbano kwa sasa,’’ alisema Zitto na kuongeza:

“Watanzania hawatarajii malumbano, uchaguzi umekwisha, tufanye kazi. Sina la kusema kuhusu kuhojiwa na chama, tutayamaliza kwenye vikao na sio katika vyombo vya habari’’.

Novemba 18, mwaka huu, wabunge wa Chadema wakiongozwa na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe ambaye ni mbunge wa Jimbo la Hai walitoka nje ya ukumbi wa Bunge Rais Kikwete aliposimama ili kuanza hotuba ya kulizindua Bunge la Kumi la Jamhuri ya Muungano.

Wakati wakitoka ukumbini, wabunge walioonekana kuwa ni wa chama tawala (CCM) walikuwa wakizomea huku wabunge wa CUF, ambayo pamoja na CCM imeunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa visiwani Zanzibar, NCCR Mageuzi na TLP wakihamia kwenye nafasi zilizoachwa wazi baada ya wabunge wa Chadema kutoka nje

No comments:

Post a Comment