KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Thursday, December 2, 2010

‘Bosi’ wa Takukuru aivulia kofia rushwa


Hidaya Omary

MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa(Takukuru) Dk Edward Hoseah amesema taasisi yake haiwezi kumaliza rushwa nchini kwa kuwa kazi hiyo ni nzito na kwamba itamalizwa kutokana na uadilifu wa Watanzania.

Dk Hosea pia amewataka Watanzania kuacha kulalamika, badala yake watoe uchambuzi wa kisayansi wenye kuanisha tatizo na kutoa suluhisho la kudhibiti vitendo vya rushwa.

Kauli ya Dk Hoseah inakuja wakati watu wa kada tofauti kwa nyakati tofauti wakilalamika na kudai kuwa Takukuru haiko makini, wakipendekeza ifutwe ili kutoa nafasi ya kuundwa taasisi nyingine huru huku wengine wakitaka iundwe chini ya bunge na kuwajibika moja kwa moja bungeni badala ya serikali ya kuu kama ilivyo sasa.

Lakini, jana akizungumza kupitia kituo cha televisheni cha Shirika la Utangazaji nchini(TBC), Mkurugenzi wa Takukuru alisema ugumu wa kupamba na rushwa unatokana na Watanzania wengi kukosa uadilifu. Dk Hoseah alitoa kauli hizo wakati kesho Tanzania inaungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Kudhibiti Rushwa ambayo huadhimishwa Desemba 9 ya kila mwaka, na kwa mwaka huu kauli mbiu ikisema, “Kukataa kwako rushwa kuna thamani’’.

Hata hivyo maadhimisho nchini yatafanyika Desemba 10 kutokana na Desemba 9 kuwa siku ya Uhuru na kwamba yatafanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam. “Takukuru pekee haiwezi kumaliza rushwa nchini. Kazi bado ni nzito na mazingira ya kupambana na rushwa ni magumu lakini uadilifu wa Watanzania ndio utakaoitokomeza na si vinginevyo, kwa kuwa msingi mkuu wa kuzuia rushwa ni uadilifu,’’ alisema Dk Hoseah Dk Hoseah ambaye alikuwa akizungumza kwa kujiamini alikwenda mbali na kusema kila mwananchi ajiangalie kama ni muadilifu na kwamba mapambano ya rushwa ni ya wote. Alisema kama wananchi watapinga rushwa kivitendo, Tanzania itapata maendeleo na itakuwa ni mahala pazuri na salama kwa kuishi. “Tuache dhana potofu na kuamini kuwa rushwa ni ya watu fulani, kabla ya kumnyooshea mwenzako kidole, angalia uadilifu wako kwanza.

“Naamini kila Mtanzania akisema rushwa basi ,asitoe wala kuchukua, tutatokomeza janga hili linalozidi kuangamiza jamii na si kutegemea Takukuru pekee,”alisema Dk Hoseah Akaongeza: “Tuache kulalamika na badala yake tufanye vitu kwa vitendo kwani kulalamika pekee hakusaidii, tutumie mbinu za kisayansi kuichambua rushwa na kuipatia suluhisho.’’
Hata hivyo, Dk Hoseah alisema kitendo cha watu kuamini Takukuru pekee ndio yenye jukumu la kupambana na kutokomeza rushwa ni upotoshaji.

Alisema mbali na uadilifu, mapambano ya rushwa yatafanikiwa kama kutakuwa na misingi imara ya mahusiano baina ya wadau wote na kwamba ajenda ya rushwa ni ya wote na haitoondolewa na kikundi kimoja. Dk Hoseah alisema kutokana na msingi mkuu wa kuzuia rushwa kuwa ni uadilifu, taasisi yake imeanzisha kamati maalumu za uadilifu kwenye ofisi za serikali, lengo ni kuwafanya watumishi wa umma kuwa waadilifu. Alisema kwa kiasi fulani huduma zitolewazo na watumishi wa umma haziridhishi na huchochea rushwa.

Kuhusu sekta binafsi, mkurugenzi huyo alisema mara nyingi hujihusisha na vitendo vya rushwa wakati wa kuomba tenda na kwamba wamependekeza kuwepo kwa kifungu cha sheria cha uadilifu. Alisema mkakati wao wa kitaifa ni kuangalia sekta zote ikiwamo mhimili wa Bunge na Mahakama jinsi zinavyotimiza wajibu katika kupambana na rushwa. Alizitaka taasisi za dini kuwa na msimamo mmoja wa kupambana na rushwa Akizungumzia umuhimu wa Desemba 9, Dk Hoseah alisema ni siku pekee ambayo watanzania wanatakiwa kujua na kuhamasishana kuwa rushwa ndio kikwazo cha maendeleo nchini.

Alisema tarehe hiyo ilipitishwa rasmi na Umoja wa Mataifa(UN) nchini Mexico mwaka 2003 kutokana na rushwa kuwa ni tatizo kubwa duniani na nikipingamizi cha maendeleo. “Madhumuni mengine ni wananchi wawe na uelewa mkubwa kuhusu rushwa, kujua hali halisi ilivyo na madhara yake pamoja na kuunganisha wadau mbalimbali,’’ alisema

No comments:

Post a Comment