KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Saturday, November 27, 2010

Waziri atoa ushuhuda alivyorubuniwa na fatak



WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk Terezya Luoga Hovisa jana alitoas ushuhuda wa kusikitisha wa maisha yake katika kongamano lililoandaliwa na Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), alipoeleza kuwa alipewa uja uzito na 'Fataki' wakati akisoma Chuo Kikuu.

Waziri Luoga alilazimika kushirikisha vijana hao kuhusu maisha yake kutaka kuwaonyesha alivyomudu kuvumilia na kupambana na maisha hadi kufikia mafanikio aliyoyapata sasa, akisema badala yake sasa anaweza "kuchakachua" hadi wanaume watano lakini "haoni sababu" na kuwataka wanafunzi kuepuka watu wenye tabia za kifataki kwa kuwa wanaweza kuwaharibia mwelekeo wa maisha.

Fataki ni jina maarufu waliopachikwa wanaume ambao wana tabia ya kufuata mabinti wadogo na kuwatelekeza baada ya kuwaharibia maisha kwa kuwapa mimba. Waziri Luoga alieleza jinsi alivyokutana na mwanamume huyo ambaye alimpa uja uzito, lakini akaongeza kuwa baadaye mtu huyo alimsomesha na hivyo kumaliza vizuri masomo. "Sio kwamba muige mfano nilioutoa," alisema Waziri Luoga akiwaambia wanafunzi hao. "Si kwamba na nyie kama wanafunzi mkayafanye haya, la asha! Badala yake ninawapa changamoto kwamba katika maisha silaha mnayopaswa kuing’angania ni elimu peke yake na si vibaka wa mitaani," alisema Dk Luoga. “Acheni kudanganywa na mafataki ambao ni matapeli na ambao huweza kuwapotezea dira ya maisha, badala yake msome kwa bidii, kwa ajili ya mafanikio ya maisha yenu.” Dk Luoga alisema kuwa vijana wengi, hasa wanafunzi wamekuwa wakirubuniwa kutokana na kushindwa kustahimili tamaa za maisha na kuamua kujiingiza kwa vijana wa mitaani ambao aliwaelezea kuwa hawana sera.

Waziri huyo, ambaye ni sura mpya katika baraza lililoundwa hivi karibuni na Rais Jakaya Kikwete, alikumbushia taaluma yake ya ualimu kwa kutumia kalamu na kuwafundisha washiriki wa kongamano hilo masuala ya maisha na athari za ukimwi kwa vijana, huku akijitangza kuwa naye ni mtoto wa mkulima. “Ni bora kuacha kabisa na kuamua kusubiri kwani kwa kuwa mahusiano katika masomo ni hatari... badala yake mzidi kumuomba Mungu na kuwa waadilifu,” alisisitiza “Leo hii, ninamshukulu Mungu kwa Elimu aliyonipa kwa sababu alinijua mimi ni mtoto wa mkulima, hivyo niliamua kutochezea maisha yangu kiholela. "Hapa unavyoniona, kama waziri nina fedha za kutosha; gari la kifahari ninalo ehe! Unadhani nikitaka kuwa na mafataki hata watano, nitashindwa?" “Nikiamua kuchakachua wanaume hata watano, naweza kwa sababu uwezo ninao na fedha ninayo.

Lakini sioni faida yeyote badala yake ni kujitumbikiza mahali ambapo ni hatari zaidi,” alisema. “Cha msingi hapa ni kuhakikisha mnajenga maadili mema mnapokuwa shuleni na nyumbani ili kuepuka kurubuniwa na kupoteza mwelekeo wa elimu mliopata.” Naye mtaalamu wa ushauri wa afya katika kamati ya vijana, Dk Telesphoy Kyaruzi alisema tatizo kubwa linalowapelekea vijana wengi kujiingiza katika ngono zembe na kupata maambukizi ni uchumi mbovu. Dk Kyaruzi alisema kwa kuliona hilo, wanaiomba serikali kuhakikisha inatoa mikopo kwa vijana ili kuwasaidia waweze kujiendesha na kuepuka vishawishi

No comments:

Post a Comment