KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Saturday, November 27, 2010

Prof Tibaijuka atangaza vita na wenye pesa Ardhi


Nora Damian
WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka ametangaza vita dhidi ya wanaotumia jeuri ya pesa kupora viwanja wakati akiweka hadharani mikakati yake kwenye wizara hiyo iliyojaa migogoro ya ardhi.

Profesa Tibaijuka, mmoja wa mawaziri 24 wapya walioingia kwenye Baraza la Mawaziri, alikuwa akiweka aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana alipokuwa akizungumzia mikakati yake kwenye wizara hiyo.
Wizara hiyo ni moja ya wizara zilizo na tuhuma nyingi za ufisadi kutokana na maofisa wake kusaidia kufanikisha uporaji viwanja, uuzwaji wa maeneo ya wazi, ubadilishaji wa matumizi ya viwanja kwa lengo la kunufaisha mafisadi na kukithiri kwa vitendo vya rushwa katika kuhudumia wananchi.

Lakini Tibaijuka, ambaye anakuwa waziri wa pili kutangaza mikakati yake baada ya Waziri wa Ujenzi, John Magufuli, alisema atapambana na watu wenye fedha ambao wanasababisha migogoro ya viwanja kwenye wizara yake.
Prof Tibaijuka, ambaye alikuwa mwenyekiti wa Baraza la Wanawake (Bawata) lililopigwa marufuku nchini kabla ya kurejeshwa kwa hukumu ya mahakama, alisema watu wenye jeuri ya pesa wamekuwa wakisababisha migogoro katika sekta hiyo kutokana na kupora viwanja vikiwemo vya wazi na vile vilivyotengwa kwa ajili ya huduma za jamii.
“Kama kuna mtu amepora kiwanja, bora akisalimishe angalau tutaongee yaishe kabla hatujamchukulia hatua,” alisema Prof Tibaijuka.


Tibaijuka, ambaye alikuwa mkurugenzi wa Shirika la Makazi la Umoja wa Mataifa (UNHabitat), aliongeza kusema: “Kama mtu akileta jeuri ya pesa, sisi wengine hizi za chakula zinatutosha hivyo hatubabaiki sana.”
Alisema atapambana na migogoro hiyo kwa kutumia sheria kwa sababu bila utawala wa sheria, maendeleo yatakuwa magumu.
Alisema mbali ya kufanya kazi na wizara na wataalamu mbalimbali, pia atafanya kazi na wananchi ili wamsaidie.
Alisema wako watu wachache ambao hawatambui kama ardhi ni muhimu kuliko fedha na kwamba atahakikisha haki inatendeka na kwamba hakutakuwa na tabia ya kuzungusha wananchi katika mazingira ambayo mtu ana haki ya kupewa kiwanja.

Waziri huyo ametoa tamko hilo wakati wizara yake ikikabiliwa na tuhuma nyingi za uuzaji viwanja kiholela unaofanywa na watendaji kwenye ngazi za wilaya, ikiwa ni pamoja na uuzwaji wa viwanja vya wazi na maeneo ya fukwe za bahari na kubadilisha matumizi ya viwanja kwa lengo la kunufaisha wachache.
Tibaijuka, ambaye ni mbunge wa Muleba Mashariki, alisema pia atarudisha ajira ya walinzi wa ardhi ili kumaliza migogoro katika sekta hiyo kwa masuala ya ardhi yasipofanyiwa kazi, sekta nyingine zinaweza kudorora kwa kuwa Sekta ya Ardhi inabeba nyingine zote.

“Migogoro ya ardhi tunaiunda wenyewe kwa hiyo wakati mwingine hatuhitaji pesa yoyote kuimaliza. Tutarudisha walinzi wa ardhi kwa sababu ni kada ya watumishi ambayo ilipotea na imetugharimu sana,” alisema.
Alisema pia katika uongozi wake atahakikisha anailinda miji kwa sababu mingi haiko katika hali inayotakiwa kutokana na kuwepo kwa tatizo la ukuaji na ujenzi holela.

“Kazi hii nimeifanya takribani miaka 10, lakini sasa mtazamo wangu unabadilika kutoka ngazi ya kimataifa na ninajikita katika utekelezaji kwenye ngazi ya taifa langu, hivyo hatutalala,” alisema.
Waziri huyo aliwaomba wananchi kutoa ushirikiano wanapoona mambo mbalimbali yanaenda kinyume na kwamba katika tovuti ya wizara hiyo itawekwa nafasi maalumu ya watu kutoa kero yake.
Naye Katibu Mkuu Patrick Rutabanzibwa alisema kuwa tayari ameanza kupangua watu kwenye wizara hiyo ili kuboresha utendaji kazi na utoaji huduma.
Alisema kati ya watumishi waliohamishwa, baadhi wanahusika na uuzwaji holela wa maeneo ya wazi jijini Dar es Salaam na kwamba amewalazimisha watumishi wengine waliopora viwanja wavirudishe

No comments:

Post a Comment