KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Friday, November 19, 2010

Wataka sheria kudhibiti uchochezi kwenye kampeni


Nora Damian SERIKALI imetakiwa kupitia upya sheria ya uchaguzi kwa kuweka kipengele kitakachowazuia wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi kutoa matamshi ya uchochezi yanayoashiria uwezekano wa kuvunjika kwa amani. Mwenyekiti wa taasisi ya kiislamu ya Imam Bukhary, Sheikh Khalifa Khamis alisema baadhi ya wagombea katika uchaguzi mkuu uliopita walikuwa wanatoa matamshi yanayoshiria kutaka kusababisha vurugu na kuvunja amani.

Alisema majukwaa mengi ya kampeni yaligeuzwa kuwa uwanja wa kashfa, chuki binafsi, udhalilishaji na kebehi, jambo ambalo aanadai kuwa ni hatari kwa kuwa linaweza kuvunja amani. “Sheria iweke wazi kuwa wagombea wote wanastahili kujihalalisha mbele ya wapigakura kwa kuelezea sera za chama chake, ilani zao na nini matarajio yao kama watapewa ridhaa ya kuongoza nchi,” alisema Sheikh Khamis. “Sheria ieleze kuwa ni kosa la jinai na kukosa sifa ya kugombea kama ikitokea mtu atatamka maneno ya kashfa na uchochezi,” alisema. Alisema pia wananchi wengi walishindwa kujitokeza kwenda kupiga kura katika uchaguzi mkuu kutokana na kauli mbalimbali za vitisho zilizotolewa na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa.

Alisema kauli hizo nyingi ziliashiria uwezekano wa kuvunjika kwa amani katika kipindi cha kati ya kupiga kura, kuhesabu na baada ya kutangazwa matokeo. “Watu wengi walishindwa kwenda kupiga kura kwa kuhofia usalama wao kutokana na kauli za vitisho zilizotolewa na wanasiasa na wengi walinunua mahitaji yao muhimu na kujizuia majumbani mwao,” alisema. Alisema pia uzembe uliosababishwa na Tume ya Uchaguzi (Nec) ulichangia watu wengi kushindwa kwenda kupiga kura. Kwa mujibu wa Sheikh Khamis, uzembe huo wa Nec ni ule uliosababisha watu wenye shahada za kupigia kura kutoona majina yao katika daftari la wapigakura. Aliitaka Nec kuboresha utaratibu wa kuandika majina ili matatizo hayo yasijirudie katika uchaguzi mkuu ujao

No comments:

Post a Comment