KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Friday, November 19, 2010

Mtikila aenda Mahakama ya Afrika


Nora Damian

MWENYEKITI wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila amesema atafungua kesi katika Mahakama ya Afrika kupinga baadhi ya vifungu vya sheria ili uchaguzi mkuu ujao uwe huru na haki. Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mtikila alisema kuna kasoro nyingi zilizojitokeza wakati wa uchaguzi mkuu lakini hazikuzuilika kutokana na mapungufu yaliyomo kwenye sheria za nchi.

Alisema baadhi ya vifungu ambavyo anataka vitenguliwe ni vile vinavyoinyima nguvu mahakama ya kutengua matokeo ya urais. “Kwa sasa Tume ya Uchaguzi (nec) ikimtangaza mtu kama mshindi wa urais, hata kama kuna kuchakachua matokeo mahakama haina uwezo wa kutengua,” alisema Mtikila. “Mahakama ya Afrika ina uwezo wa kutoa haki hiyo na inapotoa haki za msingi, lazima mataifa yote yatii,” alisema.

Alisema taratibu zote za kufungua kesi hiyo zimeshakamilika na kwamba hadi kufikia mwezi Machi mwakani itakuwa tayari imeanza kusikilizwa na mahakama hiyo. Katika hatua nyingine, Mtikila amemtaka Rais Jakaya Kikwete asahihishe makosa aliyoyafanya katika kipindi chake cha uongozi uliopita kwa kuteua baraza makini la mawaziri.

Mwenyekiti huyo wa DP alisema awamu ya nne iliyokuwa chini ya uongozi wa Rais Kikwete ilikuwa na makosa mengi yaliyosababisha wananchi wengi kuichukia serikali yake. Alisema baadhi ya makosa hayo yalifanywa na watendaji wake ambao ni mawaziri mbalimbali na maofisa wengine na kudai kuwa yalichangia kuzorotesha uchumi wa nchi.

Mwenyekiti huyo wa DP pia alikemea suala la udini kwa kusema kuwa ni hatari katika nchi na kutaka serikali isijihusishe nayo. “Katiba ya nchi inaagiza kuwa kazi ya kutangaza dini, kufanya ibada na kueneza dini itakuwa ni huru na jambo la mtu binafsi na shughuli na uendeshaji wa jumuiya za dini zitakuwa nje ya shughuli za mamlaka ya nchi,” alisema. Alisema udini sasa ni tatizo kubwa nchini na kwamba kama ukiachwa uendelee unaweza kuipoteza nchi hasa unapokosekana uzalendo na busara katika utawala

No comments:

Post a Comment