KARIBU MAISHANI
KARIBU MAISHANI
Friday, November 19, 2010
Majambazi Yawapora Polisi Bunduki, Yaua Abiria?
Majambazi wanane wakiwa na silaha za kivita wameteka na kushambulia gari la abiria na kusababisha kifo cha mtu mmoja na wengine 23 kujeruhiwa kabla ya kupora mali mbalimbali za abiria na kuwapora polisi bunduki mbili.
Tukio hilo limetokea jana katika eneo la Mukugwa wilayani Kibondo mkoani Kigoma kilomita takribani 30 toka mjini Kibondo, Majambazi hayo yalilishambulia basi la kampuni ya Golden Inter City Express lenye namba za usajiri T457 ACR linalofanya safari kutoka Kigoma kwenda Mwanza.
Kwa mujibu wa mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama wilaya ya Kibondo Bw. Dan Makanga ambaye pia ni mkuu wa wilaya hiyo, majambazi hayo hayakuweka kizuizi chochote na kwamba waliibuka kutoka porini na kuanza kurusha risasi mfululizo na kuharibu vibaya basi hilo.
“Majambazi wanne wakiwa na silaha nzito walijitokeza barabarani na kuanza kurusha risasi hali iliyomlazimu dreva wa basi hilo Bw. Method Chang’a kulisimamisha, majambazi hao wakatoa amri kwa askari polisi waliokuwemo ndani ya basi hilo kusalimisha silaha na kadri walivyochelewa kufanya hivyo ndivyo majambazi hao walivyozidi kupiga risasi sehemu mbali mbali na kusababisha abiria wengi kujeruhiwa na risasi hizo” alisema Dan Makanga, Mkuu wa wilaya ya Kibondo
Imeelezwa kuwa kutokana na kuendelea kupigwa kwa risasi hizo kwa fujo huku askari polisi nao wakijaribu kujihami na kuwahami abria bila mafanikio, walilazimika kuzirusha nje ya basi bunduki zao kitendo kilichowapa fursa majambazi kuwateka na kuanza kupora abiria mmoja mmoja.
Kaimu mganga mkuu wa wilaya ya Kibondo Dr. Frolian Ntinuga amebainnisha kuwa abiria aliyeuwawa ni katibu wa jumuiya ya umoja wa vijana wa CCM Musoma vijijini mkoani Mara Wilfred Peter Muga na abiria 23 wamejeruhiwa na kufikishwa katika hospitali ya wilaya ya Kibondo na watatu kati yao hali zao ni mbaya na wanasafirishwa kwenda Bungando kwa matibabu zaidi.
Majambazi hao ambao hawakuwa wameficha sura zao walifanikiwa kutokomea porini bila kukamatwa huku wakiondoka na silaha mbili aina ya SMG zikiwa na magazine nne mali za jeshi la polisi na imetajwa kuwa msako mkali katika pori hilo unaendelea ili kuwatia mbaroni majambazi hayo.
Eneo la Mkugwa lilipotokea tukio hilo lilikuwa kambi ya wakimbizi mchanganyiko kabla ya kufungwa na wakimbizi hao kuhamishiwa wilayani Kasulu na eneo hilo kufunguliwa shule ya sekondari ya juu ya wasichana.
Hili ni tukio baya la pili kutokea eneo hilo, katika kipindi cha miezi minne iiliyopita ambapo majambazi yaliliteka gari dogo la abiria na kumuua mwalimu Deo Kato ambaye pia alikuwa mwenyekiti wa Parokia ya kanisa katoliki Kibondo akiwa njiani kutoka Kasulu kwenda Kibondo.
Juhudi za kumpata mkuu wa jeshi la polisi mkoa wa Kigoma ACP George Mayunga hazikufanikiwa kutokana na simu yake kuwa katika matumizi kwa muda mrefu, hata hivyo Mkuu wa jeshi la Polisi wilayani Kibondo Bw. Innocent Rwelamira amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa askari wawili waliokuwa na Silaha aina ya SMG wakisindikiza basi hilo wameporwa silaha zao na kujeruhiwa
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment