KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Saturday, November 27, 2010

MCT kuchunguza tishio la Serikali kwa Mwananchi


Salim Said na Jackline Lema
BARAZA la Habari Tanzania (MCT), limeunda Kamati Maalumu ya watu watatu, kuchunguza tuhuma za tishio la Serikali kulifungia na kulifuta Gazeti la Mwananchi, linalochapwa na Kampuni ya Mwananchi Communicatios Ltd (MCL) kwa madai kuwa linachapisha habari za uchochezi.

Hatua ya MCT kuunda kamati hiyo kuchunguza malalamiko ya chombo cha habari, ni ya kwanza katika tasnia ya habari Tanzania, ingawa fursa hiyo ilikuwepo kwa miaka mingi tangu kuanzishwa kwa chombo hicho.

Oktoba 20 mwaka huu, Mwananchi iliiripoti kwa mara ya kwanza taarifa kuhusu serikali kutishia kulifungia au kulifutia usajili gazeti la Mwananchi kwa madai kwamba linaandika habari za uchochezi dhidi ya Serikali ya Awamu ya Nne.

Katika taarifa hiyo Mwananchi iliweka hadharani barua ya serikali yenye kumbukumbu namba ISC/N.100/1/VOL.V/76 iliyoandikwa kwa mhariri mtendaji wa gazeti hili, ikionya kwamba kama gazeti litaendelea kuandika habari ambazo iliziita kuwa ni za uchochezi dhidi yake, haitasita kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria za nchi.

Lakini akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za MCT jijini Dar es Salaam jana, Rais wa Baraza hilo, Jaji mstaafu Robert Kisanga, alisema ameamua kuunda kamati hiyo kwa kuwa ombi lililofikishwa kwake na mhariri mtendaji wa gazeti la Mwananchi lina maslahi kwa umma.

"Leo tumewaita hapa, ili kuwatangazia kuhusu kuundwa kwa kamati maalumu ambayo ni ya kwanza na ya aina yake katika historia ya tasnia ya habari katika nchi yetu," alisema Jaji Kisanga.

"Hii ni kamati maalumu ya kuchunguza tuhuma za tishio la serikali dhidi ya gazeti la Mwananchi na jinsi lilivyoripoti habari za uchaguzi mkuu 2010," alisema Rais wa MCT.

Alisema moja ya malengo ya MCT kama ilivyoainishwa katika Katiba kifungu cha 3(e), ni kuweka jalada la matukio yanayoweza kukwaza usambazaji wa habari za maslahi kwa jamii, kulihuisha na kuchunguza matendo ya watu moja moja, mashirika au vyombo vya serikali katika ngazi zote yanayolenga vyombo vya habari na kuweka hadharani ripoti zake.

"Kifungu 23(1) cha katiba ya MCT kinaongeza kuwa kwa mapendekezo ya Bodi ya Baraza, Rais wa MCT anaweza kuunda kamati ya watu wasiopungua watatu,"alinukuu Jaji Kisanga.

Alisema jukumu la kamati hiyo ni kuendesha uchunguzi katika jambo lenye umuhimu kwa umma, kuhusu mwenendo wa chombo cha habari au madai kuhusu chombo cha habari au jambo lolote ambalo kwa maoni ya bodi, linatajika kutolewa tafsiri katika muktadha wa kanuni za maadili.

Alisema kutokana na maelekezo hayo ya kikatiba, Bodi ya MCT illikutana Novemba 18 mwaka huu na kujadili shauri lililofikishwa na Mhariri Mtendaji wa MCL na kwamba ilijiridhisha kuwa lilihusu suala muhimu kwa umma na uhuru wa vyombo vya habari.

"Kwa hiyo basi, bodi ilinishauri kuunda kamati ya watu watatu ili kufanya uchunguzi wa suala hilo na kutoa ripoti yake, na mimi nikakubali," alisema Jaji Kisanga.

Jaji Kisanga alifafanua kuwa, kamati imeandaliwa hadidu za rejea za kina na inatafanya kazi ndani ya siku 30 na kuwasilisha ripoti kwake.

"Lengo kuu la uchunguzi litakuwa kwanza, kuangalia ikiwa madai ya serikali dhidi ya gazeti la Mwananchi yana uhalali, pili kama tishio la serikali linaingilia isivyostahili uhuru wa vyombo vya habari na uhariri," alisema Jaji Kisanga.

Jaji Kisanga aliongeza kuwa, lengo la tatu la kamati hiyo ni kuchunguza kama uandishi na mwenendo wa gazeti la Mwananchi katika kipindi cha uchaguzi, vilikiuka mwongozo wa maadili katika kuripoti habari za uchaguzi mkuu kama ilivyoafikiwa na Jukwaa la Wahariri Agosti 13, 2010 huko Morogoro.

Alisema mwongozo huo pia uliridhiwa na mkutano wa wadau uliofanyika katika jijini Dar es Salaam Agosti 18, 2010.
Alisema kamati hiyo pia itaangalia ikiwa uandishi na mwenendo wa gazeti la Mwananchi ulikiuka kanuni za maadili ya waandishi wa habari, kama zilivyofanyiwa marekebisho na kupitishwa na mkutano mkuu wa MCT uliofanyika mkoani Tanga, Juni 23 2010.

"Ninayo furaha kutajia majina ya wajumbe wa kamati maalumu ya kuchunguza tuhuma na tishio la serikali dhidi ya gazeti la Mwananchi na jinsi lilivyoripoti habari za uchaguzi wa mwaka 2010,"alisema Jaji Kisanga.

Alisema Kamati hiyo itaongozwa na Profesa Luitfried Mbunda ambaye ni profesa wa sheria aliyebobea katika sheria za uhuru wa habari.

Jaji Kisanga aliwataja wajumbe wengine kuwa ni Gema Akilimali ambaye ni mtaalamu wa masuala ya kijinsia na haki za binadamu na Attilio Tagalile ambaye ni mwandishi na mhariri wa siku nyingi katika vyombo vya serikali na binafsi ndani na nje ya nchi.

Alisema kamati itafanya kazi kwa uhuru bila ya kuingiliwa au kushinikizwa na mtu au taasisi yoyote na kwamba itawasilisha ripoti kwa Rais wa MCT ambaye baadaye, ataifikisha kwa bodi kabla ya kuwekwa hadharani kwa manufaa ya jamii na tasnia ya habari.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga, alisema kazi hiyo ni ya MCT na kwamba baraza limetenga kiasi cha Sh10 hadi 12 milioni kwa ajili ya kufanikisha kazi hiyo.
.
Alisema uteuzi wa kamati hiyo, umezingatia vigezo kama vilivyoelezwa katika kifungu cha 23 kifungu kidogo cha pili na tatu kwamba, miongoni mwa wajumbe wa kamati lazima awemo mwanasheria wa viwango vya juu na aliyebobea katika fani hiyo ambapo alisema ni Profesa Mbunda

No comments:

Post a Comment