KARIBU MAISHANI
KARIBU MAISHANI
Saturday, November 27, 2010
MAUAJI YA ALBINO: Polisi lawamani
Elias Msuya
TAASISI inayotetea watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) ya Under The Same Sun, imelilalamikia Jeshi la Polisi kuwa limekalia majina ya watu wanaofadhili mauaji ya walemavu hao bila kuwashtaki.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam jana, Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Peter Ash, amevitaka vyombo vya dola kutaja majina ya watuhumiwa hao na kuwafikisha mahakamani, ili haki itendeke.
Huku akionyesha hukumu ya Mahakama Kuu ya Tanzania kuhusu kesi ya mauaji ya mlemavu wa ngozi iliyotolewa Juni 11 mwaka huu, mkoani Tabora, Ash alisema mahakama imethibitisha kuwa kuna majina ya vigogo wanaofadhili mauaji hayo na kwamba majina hayo yako mikononi mwa Jeshi la Polisi.
Alisema hata hivyo, mahakama haikuyataja kwa kuwa bado watuhumiwa, hawajafikishwa mahakamani.
Hukumu hiyo iliyotolewa na Jaji Mkuu wa Tanzania Augustine Ramadhan, katika mahakama ya Rufani mkoani Tabora, yenye namba 318, 319, 320 ya mwaka 2009, imehusisha warufani watatu waliotuhumiwa kumuua mtoto mwenye ulemavu wa ngozi mwenye umri wa miaka 13.
Mmoja wa watuhumiwa hao waliokata rufani, ametaja majina ya vigogo wanofadhili mauaji hayo, lakini mahakama imeyahifadhi kwa kuwa hawajafikishwa mahakamani.
“Kuna majina ambayo yametajwa katika ushahidi wa Exh P4, katika maelezo ya awali ya mshtakiwa namba moja, lakini hatuwezi kuyatangaza kwa kuwa huenda pia watu hawa wakawa hawana hatia," ilisema sehemu ya hukumu hiyo.
"Tunatarajia kuwa vyombo vya dola vitaweza kutumia ushahidi huu uliopo mikononi mwa polisi, kuiokoa nchi yetu hii ya amani kutoka kwenye vitendo vya ukatili," ilisisitiza hukumu hiyo.
Ash alisema huo ni ushahidi kuwa wanaotekeleza mauaji hayo ni vigogo na watu matajiri na si watuhumiwa wachache wanaokamatwa na kuishauri serikali, kuwakamata watu hao na kuwahukumu haraka.
“Siyo sisi tuliyosema hayo, ni Jaji mkuu. Tunaitaka serikali iwachukulie hatua watu hao, kwa kuwa mtu wa akawaida hawezi kununua mkono kama kwa dola 2000, au mwili wangu wote huu, ni matajiri ndiyo wenye uwezo huo,” alisema Ash.
Hata hivyo, viongozi wa Jeshi la Polisi, walipotafutwa jana kuzungumzia suala hilo, walisita kulizungumzia. Mkurugenzi wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Robert Manumba, alisema anayepaswa kulitolea maelezo suala hilo ni Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora.
“Hilo mulize RPC wa Tabora ndiye anaweza kukupa maelezo zaidi,” alisema Manumba. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora Liberatus Barlow, alisema yuko kwenye kikao na kwa hiyo, hana nafasi ya kulizungumzia.
“Niko kwenye kikao,” alijibu na kukata simu. Hata hivyo Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, Said Mwema alipotafutwa kulizungumzia suala hilo simu yake ilikuwa ikiita bila kupokelewa kwa muda mrefu.
Mauaji hayo yaliyotokea Oktoba 4 mwaka huu, ambapo mlemavu wa ngozi kutoka Tanzania aliuawa na watu waliomteka wakitokea nchini Burundi,
Mauaji mengine kama hayo yaliyotokea mpakani wa Zambia na Tanzania.
Ash alisema ingawa mauaji hayo yamepungua nchini, lakini sasa yamehamia mipakani mwa nchi.
Aliwataka wabunge na mawaziri wapya, kulivalia njuga janga hilo na kwamba huo ni wajibu wao kama viongozi waliochaguliwa na wananchi.
Hivi karibuni, Waziri mkuu Mizengo Pinda alisema kuwa ameshapata ekari 50 mkoani Arusha kwa ajili ya kujenga kituo cha kulelea watu wenye ulemavu wa ngozi.
Tangu mauaji hayo yalipoanza mwaka 2007, walemavu 59 wameshauawa na tisa wengine kujeruhiwa.
mwisho
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment