KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Saturday, November 27, 2010

CAG awapa 'mtihani' wabunge


MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) amewataka wabunge wa Bunge la Kumi kuhakisha wanatumia vizuri ripoti za ofisi hiyo ili waweze kuidhibiti serikali katika matumizi.

CAG alitoa kauli hiyo juzi jioni jijini Dar es salaam wakati akifunga semina ya siku nne ya kuwajengea uwezo makatibu wa kamati za kudumu za Bunge, ikiwa ni pamoja na kuwapa mbinu za kuchanganua ipasavyo maeneo muhimu katika ripoti zake za matumizi ya fedha za serikali.

Kaimu mdhibiti mkuu wa ofisi hiyo, Jumaa Mshihiri alisema pamoja na mambo mengine wabunge wawatumie makatibu wa kamati za bunge kuwafafanulia baadhi ya vipengele wasivyovielewa vizuri wakati wa kujadili ripoti zake.

“Tunataka ufanisi zaidi katika Bunge la Kumi; tumewajengeeni uwezo makatibu ili... muweze kuwashauri wabunge ipasavyo ili waweze kuhoji vizuri matumizi yaliyofanywa na yakatofanywa na serikali kwa lengo la kudhibiti matumizi holela pamoja na kuboresha utendaji wao,’’ alisema Mshihiri

Alisema kutokana na sababu mbalimbali wabunge pamoja na makatibu hao wameshindwa kuzichanganua vizuri ripoti za CAG na kwamba hali hiyo imesababisha kwa kiasi fulani wabunge kushindwa kuibana au kuhoji vizuri matumizi ya serikali.

“Mkazo wetu mkubwa upo kwa makatibu wa Kamati ya Mashirika ya Umma (Poac), Hesabu za Serikali Kuu(Pac) pamoja na Hesabu za Serikali za Mitaa(LAAC)," alisema.

“Kamati hizi ndizo tunashughulika nazo moja kwa moja katika utendaji wetu wa kila siku,’’ Mshihiri aliongeza.

Mkurugenzi wa Bunge, Charles Mloka alisema mafunzo hayo yatakiwezesha chombo hicho cha wawakilishi wa wananchi kuwa na ufanisi zaidi katika kuisimamia serikali na kwamba changamoto kubwa itakuwa katika kuwafafanulia ipasavyo wabunge, vipengele muhimu vya ripoti za CAG.

“Changamoto kubwa ni jinsi makatibu wa bunge watakavyoweza kuzichambua ipasavyo ripoti za CAG na kuwashauri wabunge katika masuala ya kitaalamu wakati watakapotakiwa,’’ alisema Mloka

Mloka alifafanua kwamba wabunge pamoja na makatibu wa kamati za Bunge walikuwa wakipata changamoto nyingi katika kuzipitia ripoti za CAG na kwamba hali hiyo ilisababisha washindwe kufanya kazi yao vizuri.

Awali akizunguza kwa niaba ya makatibu hao, mkurugenzi msaidizi wa Bunge, Anselm Mrema alisema changamoto kubwa waliyoiona ni sheria ya uteuzi wa anayekagua matumizi ya ofisi ya CAG.

Kwa mujibu wa sheria, PAC ndiyo inayoteua mkaguzi wa matumizi ya CAG.

“Pamoja na mambo mengine, tunataka ofisi ya Bunge ihusike moja kwa moja katika kumteua mkaguzi wa matumizi ya CAG,’’ alisema Mrema

Katika mafunzo hayo yaliyogharimiwa na serikali ya Sweden kwa kutumia Shirika la Misaada la Sweden (Sida), makatibu hao walifundishwa wajibu na mamlaka ya Bunge pamoja na kamati zake katika kuisimamia serikali na taasisi zake pamoja na masuala ya ukaguzi wa fedha unavyofanywa, sheria ya ukaguzi wa fedha na kanuni zake

No comments:

Post a Comment