KARIBU MAISHANI

KARIBU MAISHANI

Thursday, October 28, 2010

Wanasayansi waunganisha nguvu kutokomeza Ukimwi



Neville Meena, Vienna – Austria

TAASISI kadhaa za kimataifa zinazojihusisha na utafiti wa dawa ya Ukimwi zimekubaliana kuunganisha nguvu zao ili kuharakisha upatikanaji wa tiba ya ugonjwa huo.

Tofauti na mwanzoni ambapo taasisi hizo zilikuwa zinafanya kazi kwa kujitegemea, sasa zimeamua kuungana ili kufanikisha lengo la kupatikana dawa ya kuponya au chanjo ya kinga ya ukimwi.

Wanasayansi hao sasa wanahaha kutafsiri matokeo ya tafiti mbalimbali zilizoonyesha mafanikio katika kukabiliana na ugonjwa wa ukimwi ili zianze kuingia katika upatikanaji wa tiba na chanjo halisi za ugonjwa huo.

Katika mkutano wa Kimataifa wa Ukimwi unaofanyika katika kituo cha kimataifa cha mikutano cha Reed Messe Wien, mjini Vienna, wakuu wa taasisi zinazotafiti tiba ya ugonjwa huo wamekuwa wakitoa kauli zinazofanana kuhusu umuhimu wa kuuganishwa nguvu za utafiti na kuwepo kwa mfumo rasmi unaoziwezesha kubalishana matokeo ya tafiti husika.

Taasisi iitwayo The Global HIV Vaccine Enterprise ya nchini Marekani ndiyo imepewa jukumu la kuwakutanisha watafiti ambao sasa wanayafanyia kazi matokeo ya awali ya tafiti mbili ambayo yameonyesha kuwepo kwa uwezekano mkubwa wa kupatikana kwa dawa na chanjo ya ukimwi, pamoja na utafiti uliowezesha kupatikana kwa dawa ambayo inadhibiti maambukizo ya ukimwi kwa wanawake.

Akizindua mpango wa unaoitwa ‘Njia ya kuelekea katika mafanikio ya kudhibiti Ukimwi’, Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Dk Alan Bernstein alisema: “Kupatikana kwa chanjo salama na yenye uwezo wa kuzuia maambukizi ndiyo changamoto kubwa iliyo mbele ya wanasayansi hivi sasa”.

Kwa mujibu wa Dk Bernstein, mafanikio hayo yanatoa changamoto kwa wanasayansi na watafiti kuharakisha mchakato wa utafiti mwingine utakaowezesha dunia kupata chanjo au tiba salama na ya uhakika.

“Tumefungua ukurasa mpya wa kiutafiti wa chajo ya Ukimwi. Ipo ndani ya uwezo na kwa mtazamo wetu. Lakini ipo haja ya kujitoa mbali na rasilimali zinazohitajika, pia ujuzi wa kisanyansi wa hali ya juu na mwisho lazima tuwe na maono ya pamoja ya kiutafiti katika kulikabili janga la ukimwi,”alisema Dk Bernstein alipozungumza na Mwananchi baada ya kuzindua mpango huo.

Wiki iliyopita wanasayansi wa Marekani waligundua chembechembe yaani antibodies, zenye uwezo mkubwa wa kuzuia virusi wa Ukimwi (HIV) kuingia kwenye seli nyeupe za damu — kwa 90% — hivyo kusitisha mazaliano ya HIV.

Taarifa hizo zilitangazwa na wanasayansi wa Taasisi ya Magonjwa ya Kuambukiza na Mzio (Niaid) ya Marekani, wakisema tiba hiyo inaweza kuzuia virusi vya ugonjwa huo hatari kwa asilimia 90, kiwango kinachoiweka dawa hiyo kwenye uwezekano mkubwa wa kupitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) na kuanza kutumika rasmi.

Dawa hiyo huchochea mwili na kuuongoza katika kujitengenezea aina ya chembechembe za kinga zenye uwezo wa kukabili virusi vya ukimwi. Chembechembe hizo zimepewa jina la kitaalamu la VRCO1 na VRCO2 ambazo utafiti wake umeonyesha kuwa zinaweza kuvikabili virusi vya Ukimwi kwa asilimia 90.

Juzi Kituo cha Utafiti wa magonjwa ya Ukimwi cha nchini Afrika ya Kusini (Caprisa)
kilitangaza kugundua dawa aina ya Tenofovir ambayo ni mafuta (gel) yanayopunguza uwezekano wa wanawake kuambukizwa virusi vya ukimwi wanapofanya tendo la ndoa na wanaume walioathirika.

Mafanikio ya Caprisa yalitanguliwa na mafanikio mengine ya taasisi ya nchini Marekani inayoshughulikia magonjwa ya kuambukiza na athari zake (NIAID) anbayo wiki mbili zilizopita ilitangaza kugundua chembechembe (antibodies) zenye uwezo wa kuvikabili virusi vya ukimwi kwa asilimia nyingi.

Mwaka jana wataalamu wa afya nchini Thailand kupitia mradi unaofadhiliwa na Jeshi la Marekani walibaini chembechembe katika mwili wa binadamu zenye uwezo wa kuvikabili virusi vya Ukimwi kwa asilimia 30, hatua ambayo iliwatia ‘wazimu’ watafiti wengine duniani kuanza harakati za kutafuta dawa ya tiba ya ugonjwa huo.

Utafiti wa Thailand ulibaini chembechembe za aina mbili zenye uwezo wakukabiliana na virusi vya ukimwi ambazo kitaalamu zinaitwa PG9 na PG16 ambapo katika matokeo mapya ya taasisi ya NIAID pia zimegunduliwa chembechembe mbili ambazio kitaamu zinaitwa VCR01 na VCR02.

Hata hivyo kwa mujibu wa taratibu za kitaalamu, lazima ziwepo tafiti nyingine za kuthibitisha matokeo ya tafiti za awali kabla ya bodi na mamlaka mbalimbali za udhibiti hazijaidhinisha kuanza kutengenezwa na baadaye kusambazwa kwa dawa husika.

Dk Bernstein alisema kazi iliyopo mbele ya wanasayansi na watafiti hivi sasa ni kubainisha maeneo au ajenda za utafiti kwa kuzingatia matokeo ya tafiti za awali pamoja na kuboresha miundombinu ya mawasiliano ili kuwezesha upatikanaji wa takwimu na taarifa nyingine za kiutafiti.

“Pia ni lazima turuhusu watafiti wapya wenye mawazo mapya ya kisayansi huku tukitafuta vyanzo vipya vya fedha kwa ajili ya kugharamia hatua hii mpya inayoweza kutupa majibuya uhakika kuhusu tiba ya Ukimwi,”alisema Dk Bernstein.

Kwa upande wa matokeo ya utafiti wa kisayansi wa nchini Marekani na Thailand, wataalamu wanalazimika kutafiti zaidi ili kufahamu jinsi chembechembe zilizobainika zinavyoweza kujenga kinga dhidi ya virusi vya Ukimwi na matokeo ya tafiti hizo ndiyo yatakayowezesha kutafutwa kwa chanjo husika.

Mmoja wa viongozi na washauri waandamizi katika tafiti za tiba ya Ukimwi duniani Dk. José Esparza alisema: “Pamoja na matoke mazuri ya tafiti hizi, hatuwezi kusema tumekaribia kupata tiba kamili inayoweza kutumiwa na umma dunia nzima”.

Kwa mujibu wa Dk Esparza wajibu wa watafiti ni kuugana sasa na kuhakikisha inapatikana dawa baada ya kupitia katika hatua zote ili kukidhi matakwa ya kitaalamu.

Aliongeza: “Ili kufikia hapo inaweza kutuchukua mika mingine 10 au 15 tukihusisha watafiti wapya na wenye upeo mpya katika masuala ya kisayansi”.

Hata hivyo upatikanaji wa fedha unaweza kuwa kikwazo cha kukamilishwa kwa tafiti hizo kutokana na fedha zilizotolewa mwaka jana dunia nzima kuwa dola za Marekani milioni 800 tu ikiwa ni pungufu ya asilimia 10 ya kiasi cha fedha zilizotolewa mwaka 2007.

Wastani wa mahitaji ya kuwatibu watu wanaohishi na virusi vya Ukimwi duniani pamoja na gharama nyingine zinazotokana na ugnjwa huo ni dola za Marekani bilioni 30 kwa mwaka na watafiti wanaona umuhimu wa serikali za dunia kutoa fedha kwa ajili ya kukamilisha tafiti za tiba ya ugonjwa huo ili kupunguza gharama zinazotumika hivi sasa.

Tangu ugonjwa wa Ukimwi ulipogunduliwa mwaka 1983, umesababisha vifo vya watu zaidi ya milioni 25 duniani na inakadiriwa kuwa hivi sasa watu milioni 33 wanaishi na virusi vya Ukimwi na Ukimwi huku kukiwa na nyongeza ya watu 7,400 wanaoambukizwa kila siku

No comments:

Post a Comment