KARIBU MAISHANI
KARIBU MAISHANI
Tuesday, October 5, 2010
Marekani Yaomba Radhi Kwa Kuwaambukiza Watu Magonjwa ya Zinaa
Rais wa Marekani, Barack Obama na waziri wake wa mambo ya nje, Hillary Clinton wameiomba radhi serikali ya Guatemala baada ya kugundulika Marekani iliwatumia raia wa Guatemala katika majaribio ya madawa yake kwa kuwaambukiza kwa makusudi watu 1,500 magonjwa ya zinaa.
Serikali ya Marekani imeiomba radhi serikali ya Guatemala baada ya kugundulika wanasayansi wa Marekani waliwatumia raia wa Guatemala katika majaribio yao ya madawa ya magonjwa ya zinaa kwa kuwaambukiza kwa makusudi magonjwa ya zinaa.
Majaribio hayo ingawa yalifanyika miaka 60 iliyopita, kugundulika kwa siri ya majaribio hayo kumepelekea rais Obama ampigie simu rais wa Guatemala kumuomba radhi. Serikali ya Guatemala imesema itaanzisha uchunguzi kuhusiana na majaribio hayo ambayo ilisema yako nje ya ubinadamu.
Imegundulika pia kuwa katika miaka ya karibuni baadhi ya wanasayansi wa Marekani wamekuwa wakienda kwenye nchi masikini ambazo raia wake wana upeo mdogo wa kielimu na kuwatumia watu kujaribu madawa yao.
Katika maongezi yake kwa njia ya simu na rais wa Guatemala, Alvaro Colom, rais Obama alielezea kusikitishwa na majaribio hayo yaliyofanywa na watafiti wa afya wa Marekani nchini Guatemala kati ya mwaka 1946 na 1948.
Rais Obama alisema kuwa serikali ya Marekani inawaomba radhi watu wote walioambukizwa kwa makusudi magonjwa ya zinaa.
Obama aliahidi kuanzia sasa majaribio yote ya madawa yatalazimika kuzingatia sheria za Marekani na za kimataifa.
Watu 1500 waliambukizwa magonjwa ya zinaa kama vile gono, kaswende na kisonono na kisha kupewa madawa ya majaribio kutibu magonjwa hayo. Mtu mmoja alifariki katika majaribio hayo.
Katika majaribio hayo yaliyoongozwa na dokta John Cutler, wanawake wanaofanya ukahaba nchini Guatemala waliambukizwa kwa makusudi magonjwa ya gono au kaswende na kisha wanawake hao kuruhusiwa kufanya mapenzi na wanajeshi na wafungwa.
"Baada ya kugundulika ni watu wachache waliambukizwa magonjwa hayo, watafiti walibadilisha staili na kuamua kuwadunga sindano za maambukizi hayo wanajeshi, wafungwa na watu wenye matatizo ya akili", zilisema nyaraka za majaribio hayo.
Baada ya hapo watu walioambukizwa magonjwa hayo walipewa madawa ya majaribio lakini hakukuwa na taratibu za kuhakikisha kama wamepona magonjwa hayo au la.
Inaaminika kuwa watu walioshiriki majaribio hayo hawakujua kinachoendelea kutokana na kuongopewa na wanasansi hao.
Rais wa Guatemala alisema kuwa alikuwa hajui lolote kuhusiana na suala hilo mpaka alipopigiwa simu ya kuombwa radhi na waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Hillary Clinton.
Taasisi Huru ya madawa ya Marekani itafanya uchunguzi kugundua undani wa majaribio hayo ya madawa nchini Guatemala.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment